CCM, mafisadi hadi kufa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kujua kwamba kile wanachokisema wakubwa wao sicho wanachomaanisha.

Aidha, wameanza kujua kuwa kile wanachoamua wakuu wao sicho wanachokiamini. Kada yeyote atakayejitosa kichwakichwa kuunga mkono matamko na maazimio ya vikao vya wakubwa kama walivyofanya wabunge Idd Azzan, James Lembeli na diwani Denis Lupala ‘itakula kwako’.

Hawa wanajuta kuunga mkono na kushadidia viongozi mafisadi ndani ya CCM wajivue gamba.

Baada ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM katika mkutano wao mjini Dodoma kuazimia kujivua gamba, Azzan (Kinondoni), alifunga vipaza sauti asikike nchi nzima akiunga mkono kwa kuitaka Kamati ya Siasa mkoa wa Dar es Salaam ijivue gamba.

Loo, wenye chama walipomsikia, wakamweka kitimoto. Mwishowe, wakamfungia asigombee uongozi wowote ndani ya chama kwa miezi 18.

Amekata rufaa makao makuu ili wakubwa aliowaunga mkono watengue adhabu hiyo.

Lembeli alibaki na kinyongo tangu alipochezewa rafu katika uchaguzi mkuu mwaka jana kwa kupangiwa kugombea ubunge jimbo hewa la Ushetu wilayani Kahama.

Aliposikia tamko la kujivua gamba, akatumia mwanya huo kuisema kamati ya siasa ya mkoa wa Shinyanga ijivue magamba. Wee! Makada wa chama mkoani wanatarajia kumweka kitimoto. Kama Azzan, Lembeli naye ni mbunge.

Lupala, diwani wa kata ya Mgama, Iringa Vijijini, naye ameponzwa na ujasiri wake kumtaka naibu katibu mkuu Bara, John Chiligati, ajivue gamba. Tayari amesimamishwa uanachama.

Lupala alidhani kuwa kama sekretarieti chini ya katibu mkuu Yusuf Makamba ilikuwa gamba na ikaondolewa, haoni sababu kwanini Chiligati, aliyekuwa katibu wa Itikadi na Uenezi, arejeshwe katika sekretarieti mpya.

Matukio haya machache ni ushahidi kuwa viongozi walioshikamana na mafisadi ndani ya CCM ni wengi na wana nguvu katika ngazi zote za chama. Makao makuu ya CCM hawajatoa tamko lolote kuwanusuru Lembeli na Azzan.

Sekretarieti mpya chini ya katibu mkuu Wilson Mukama imekimbia moto wa mafisadi na kuanzisha malumbano na CHADEMA, chama kilichosumbua CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.

Ushahidi mwingine kuonyesha CCM imetekwa ngazi zote na mafisadi ni kusudio la halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ikishirikiana na mkoa kutaka kumfukuza mbunge wao, Dickson Kilufi.

Sababu za mbunge huyo kufanyiwa njama na viongozi wa chama chake ni msimamo wake kuunga mkono wananchi wanaomlalamikia mwekezaji mmoja wilayani.

Makada hao wako matatani kwani walifuata kauli rejareja za NEC ya Jakaya Kikwete wakasahau kiapo kwamba hawapaswi kutenganisha ufisadi na CCM kwa vile mafisadi ni mhimili wa chama.

Sekretarieti mpya ilianza kiinimacho, ikatoa matamko makali, ikawapa mafisadi muda kujivua gamba. Lakini hata kabla ya mwezi kwisha, imegeuza maazimio kuwa porojo.

Kwanza Mukama amegeuza kuwa ni porojo za katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye mafisadi kupewa muda wa siku 90. Anadai ni siku 120, yaani hadi kikao kijacho cha NEC. Pili alimpinga Nape kuhusu majina ya mafisadi aliowataja.

Naye Chiligati ameongeza utata akidai kuwa mafisadi wamepewa muda mpaka mwakani, siyo siku 120, na Nape akaanza kupigana mieleka na CHADEMA.

Kwa kawaida, Katibu wa Itikadi na Uenezi ni kiongozi wa kueneza sera, itikadi, maazimio, maelekezo, matamko na maamuzi yote ya chama na kujibu hoja dhidi ya uzushi kutoka upinzani.

Kwa hiyo, alichopaswa Nape kueneza ni uamuzi wa kujivua gamba utakavyosaidia kuirejesha CCM kwenye umaarufu wake si kuwa kinu cha uzushi na porojo. Anachofanya ni kukwepa hoja ili waendelee kuishi na mafisadi hadi kufa.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: