CCM mipasuko, CHADEMA mivutano


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na mipasuko wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinakabiliwa na mivutano.

Bali CCM ilipasuka tangu 2005. Jitihada za Jakaya Kikwete kuingia ikulu hazikuiacha ikiwa moja. Je, leo hii anaweza kuwa suluhisho la mipasuko hiyo?

Ndani ya CCM, waislam na wakristo hawaaminiani tena; mafisadi na wazalendo wanapikika chungu kimoja lakini hawaivi; wanamtandao na wasio wanamtandao wanachunguzana na kufitiniana.

Katika CCM, wenye fedha na wasio na fedha hawatakiani heri; kuna wanaoona Chadema ndicho chama kikuu cha upinzani wakati wengine wanaona ni CUF.

Kiitikadi wapo wanaoona kuwa umaskini wa Watanzania unatokana na ufisadi uliokithiri nchini wakati kuna kundi linaloamini umaskini huo “unatokana na uvivu.”

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ambaye yuko kundi linalojulikana rasmi kama kundi la mafisadi, aliwahi kuniambia wazi kuwa, Baba wa Taifa, Julius Nyerere, ndiye chimbuko la umaskini wa Watanzania.

Fisadi huyo alinambia, tukiwa ndani ya ndege kwenda Ulaya, kuwa Nyerere aliasisi “fitina za kitaifa” kupitia Azimio la Arusha na kuziboresha kwa kuimarisha mfumo wa chama kimoja.

Alisema wenye akili na ubunifu wakazuiwa na kudhibitiwa wakati, wajinga na wachimvi wakiimarishwa na kuthaminiwa. Matokeo yake, nchi ikaingia katika umaskini na mfumo unaoendelea kulitafuna taifa hili mpaka leo.

Aliendelea kunieleza kuwa, Rais Benjamin Mkapa alijaribu na kufanikiwa kuutikisa mfumo huo na kuwafanya Watanzania waanze kujibidisha kufanya kazi badala ya kupiga soga na siasa.

Lakini kwa masikitiko yake, alisema Rais Kikwete hana ubavu wa kuendeleza fikra hizo za Mkapa na badala yake akiamka asubuhi “anafikiri kama Nyerere;” na kabla ya kufunga ofisi jioni “anacheza kama Mkapa.”

Ndani ya Kamati Kuu, Kikwete hana uwezo wa kuanzisha mjadala huu na kuusimamia kwa ufanisi kwa sababu amebanwa.

Upande mmoja wapo mafisadi wenye nguvu na ushawishi wa fedha; na upande wa pili wako wanaodai ni wafuasi wa Baba wa Taifa, lakini wanaoongozwa na tamaa ya kushika madaraka baada ya Kikwete kumaliza kipindi chake.

Kutokana na kukosekana kwa mjadala wa wazi kuhusu itikadi rasmi ya CCM, mipasuko imetokea na itaendelea kutokea. Katika hali kama hii, jumuia za chama huwa zinakuwa na fursa ya kubadilisha mwelekeo ndani ya chama kikongwe kama hiki.

Lakini kwa sasa, vijana wengi nchini na ndani ya CCM, hawavutiwi tena na sera na mwelekeo wa chama hicho. Uanaharakati huwa ndio kikolezo muhimu cha vijana ndani ya vyama vya siasa, lakini kufanya uanaharakati ndani ya CCM kwa sasa ni sawa kupingana na sera “rasmi” ya CCM –  ufisadi.

Kundi dogo la vijana waliobaki ndani ya CCM ni wale wenye matumaini ya kupata vyeo au wanaolipwa ujira maalum kwa ajili ya kufanya operesheni fulani ndani au nje ya chama.

Jumuia ya wanawake imepoteza umaarufu na badala yake vikundi vya ujasiriamali ndivyo vyenye maslahi na hivi ni kwa vyama vyote si kwa CCM peke yake.

Wanawake wengi, hasa wa vijijini, wamebaini hilo na siyo siri kuwa, katika uchaguzi uliomalizika, CCM haikupata kura nyingi za akina mama kama katika chaguzi zilizopita.

Jumuia ya wazazi ni kama haipo ama ipo kwa sababu za kihistoria. Hata vigezo vinavyoifanya iwepo ndani ya CCM havina uhakika tena. Mtu yeyote anaweza kuwa mwanachama wa jumuia hii, wakiwamo hata wasio na familia rasmi au wanaoongeza idadi ya watoto wa mitaani.

Jumuia hii sasa inadaiwa kutumika kuwasaidia “marafiki” walioshindwa kuchagulika katika chaguzi za kawaida. Hapa sharti pawe na mpasuko.

Mwathirika mmoja wa mchakato wa uchaguzi katika jumuia hii aliwahi kuniambia kuwa aliwasilisha mbele ya chama mpango mkakati wa kufufua jumuia ya wazazi, lakini akaambulia kuitwa fisadi na mafisadi halisi.

Hivyo, jumuia ya wazazi ambayo kwa historia ndicho chungu cha hekima ya chama, haiwezi hata kidogo kunusuru mipasuko iliyo ndani ya CCM.

Nikienda Chadema, ni wazi chama hiki kinakabiliwa na mivutano kadhaa, tena iliyo hatarishi.

Kwanza, hakijawa na itikadi rasmi inayoeleweka; na pili, ukuaji wake umekuwa wa ghafla mno na kwa kasi ambayo muundo wake hauwezi kustahimili. Kasi isiyodhibitiwa, hata katika gari, husababisha gari kuacha njia na kuleta ajali.

Kuna mivutano mikubwa miwili ndani ya Chadema. Kwanza, ni ule unaotokana na wale wanaoitwa waasisi dhidi ya wanaodaiwa ni wa kuja ndani ya chama.

Chama cha upinzani, kinachotafuta kukiondoa chama kikongwe madarakani, kinaweza kupoteza fursa ya kuhangaisha chama tawala, na badala yake kukuta kinajihangaisha chenyewe.

Mvutano wa pili ni kati ya vyombo vya maamuzi na wabunge. Chadema kama chama kina vikao vya maamuzi; lakini kwa kuwa kimebahatika kuwa na idadi kubwa ya wabunge, kinajikuta kinafanya maamuzi fulani kwa kutumia kundi la wabunge.

Ikitokea wabunge wameamua vizuri, amani itakuwepo; lakini pale watakapoamua vibaya, mivutano itaongezeka. Mivutano ikiongezeka na kukua, huitwa mipasuko.

Mipasuko ndani ya CCM kwa sasa, ilianza kama mivutano lakini ikaachwa na hatimaye kufikia hatua hii, ikikuzwa na vyombo vya dola vikisaidiwa na vyombo vya habari.

Kama Chadema itavipa mwanya vyombo hivi – dola na habari – kwa njia ya kujianika, itakuza mivutano na hatimaye kijidhoofisha. Nayo CCM inaelekea kutota.

Na kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kuwaletea watu maendeleo isipokuwa kwa kupitia njia za kisiasa, tukubaliane kuwa ikiwa marubani wetu wawili – CCM na Chadema –  wanakabiliwa na mipasuko na mivutano, basi safari yetu itakuwa na dosari kubwa.

Wanasayansi ya siasa wanadai mipasuko na mivutano ni afya kwa vyama. Sikubaliani nao. Hapa kwetu, mivutano na mipasuko haileti afya kwa vyama; ndiyo maana CCM wanatumia muda mwingi kutimuana baada ya uchaguzi kwa sababu hawawezi kustahimili migawanyiko ndani yake.

Natamani vyama vyetu vingekuwa na uwezo huo wa kugawanyika pasipo kusambaratika.

 

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: