CCM msipodandia katiba mpya, mtaachwa na historia


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

NINGEKUWA nina uwezo wa kukishauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu mjadala unaoendelea nchini juu ya haja ya kuwa na Katiba Mpya ningesema “mmechelewa.”

Ningewashauri kwamba kama wana uwezo wa kudandia treni hili liendalo kasi basi wangebeba magwanda yao na kuanza kuandamana kuunga mkono “Azimio la Katiba Mpya.” 

Ni kwa sababu, CCM isipoongoza mazungumzo na hatimaye kuandikwa kwa Katiba Mpya nchini, itaweza kujikuta inafuata wengine na huo ndio utakuwa mwisho wa chama chenyewe.

Kauli za muda mrefu za kuwa “hakuna haja ya kuwa na katiba mpya,” na kwamba “Serikali haijapokea hoja rasmi,” zimepitwa na wakati na hazina mvuto wa ukweli wala ushawishi mbele ya wananchi.

Kwa sasa, hata mtoto mdogo aliyefuatilia matukio ya uchaguzi mkuu uliopita, anaweza kueleza kuwa uchaguzi haukwenda vema. Hata kama atashindwa kuanisha kitu gani ambacho hakikwenda sawa, lakini atasema alikuwa anamaanisha kutokuridhika na mfumo wa uchaguzi.

Kwa mara nyingine tena CCM kinajikuta katika nafasi ya kuonewa wivu ya kihistoria. Hiki ndicho chama kinachounda serikali zote mbili – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hiki ndicho chama kinachoongoza mabunge yote mawili – Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo basi, kwa kipimo chochote kile, hiki ndicho chama ambacho kwa kila kipimo kina uwezo na nyenzo za kuweza kuongoza mjadala huu wa katiba mpya.

Nafasi hii ni nafasi ya kuonewa wivu kwa sababu badala ya kulazimishwa kwa maandamano, na msukumo kutoka nje chama hiki kinaweza kabisa kukaa chini na  kusema kimesikia hoja za kuwapo kwa katiba mpya na inakubaliana na hoja hiyo.

Katika hili hakuna mtu mwenye nafasi ya pekee kama rais Jakaya Kikwete.

Wakati mtangulizi wake, rais mstaafu Benjamin Mkapa alijua kuwa taifa lake linahitaji katiba mpya kwa muda wote wa miaka 10 ya utawala wake, yeye alishindwa kusimamia mchakato wa kupatikana katiba hiyo.

Matokeo yake amemkabidhi mrithi wake, rais Kikwete nchi ambayo imejaa lundo la malalamiko yanayotokana na kukosekana kwa katiba mpya.

Ni vema Kikwete ambaye historia imemuangushia mabegani mwake mzigo ambao marais wawili nyuma yake wameshindwa kuubeba – Mkapa na Ali Hassani Mwinyi – akaondokana na mzigo huo kwa kuanzisha na kusimamia mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.

Hata hivyo, hatuna budi kutambua kuwa katiba mpya ikiandikwa bila kushirikisha maoni ya wananchi na kugusa mambo yote muhimu ya kitaifa na ikageuka kuwa katiba ya CCM, basi tatizo hilo litazidi kuongezeka.

Hivyo, tunapozungumzia katiba mpya ni lazima iwe ni katiba ya Watanzania ambayo chama chochote kitakachoingia madarakani hakitalazimika kuigusa au kuichezea.

Tunapozungumzia katiba mpya, hatuzungumzii katiba itakayonufaisha wapinzani na kukandamiza CCM, ama  kuinufaisha CCM na kukandamiza upinzani; la hasha! Tunapozungumzia uwapo wa hitaji la katiba mpya, tunazungumzia katiba itakayonufaisha wananchi wote.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kikongwe na chenye uzoefu wa utawala wa serikali kuliko chama kingine kinajikuta kinatakiwa kufanya uamuzi.

Uamuzi ambao kwa sisi wengine ni uamuzi mwepesi ambao hautakiharibia chama hicho heshima yake au ujiko wake zaidi ya kukipa ushujaa wa bure.

Uamuzi wa kukumbatia hoja ya Katiba Mpya na mara moja kukaa na vyama vingine na wadau wengine ili kuweza kujenga mfumo wa kwenda kuandika katiba hiyo huku lengo kuu likiwa kuwa katiba hiyo ndiyo itakayotumika katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa vile ndio tunaanza mapema miaka mitano ya pili ya rais Kikwete ninaamini huu ni wakati muafaka kwa CCM kujipima na kuona kuwa nafasi hii ya kihistoria haipotezwi.

Wasipofanya hivyo, aidha kwa sababu ya kiburi cha madaraka (ambayo wameanza kuyapoteza) au kwa sababu ya kutotaka kuwapa nguvu wapinzani (kitu ambacho hawawezi kuzuia tena), basi CCM kijue mapema kuwa historia haizuiliwi kwani hutiririka kama mto wa maji yakienda yanakokwenda na hayarudi yalikotoka.

Tanzania itakuwa na Katiba Mpya; kama hilo litatokea miaka hii mitano au miaka ishirini baadaye sijui, lakini kwamba litakuja mapema zaidi hili nina uhakika nalo.

Kama chama hicho na wanasiasa hawataanza mchakato huu katika hali ya umoja na utengemano, basi nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa kuona tukilazimishwa kufanya hivyo wakati wa vurugu.

Ni vema CCM idandie treni hili ya Katiba Mpya. Isiliache vinginevyo chenyewe kitaachwa!

Angalau sasa baadhi ya viongozi wake wakuu na wakongwe wameanza kuzungumza wazi; lakini hawa hawako madarakani.

Ni mpaka wale walioko madarakani watakapoanza kuzungumza suala la Katiba Mpya hapo CCM itajikuta inaongoza kweli mjadala huu. Wabunge wa CCM ni lazima waanze kuzungumzia hoja ya Katiba Mpya wakianza kupinga wataachwa na treni hili ambalo linabehewa moja tu – mabadiliko.

Hoja ya Katiba Mpya siyo hoja ya wapinzani tena; hoja ya mabadiliko ya Katiba siyo hoja ya nchi za kigeni; hii ni hoja ya Watanzania. Hakuna sababu ya mtu kuandika barua kwenda kwa waziri kumuambia ati tunahitaji katiba mpya!

Hakuna haja ya mbunge yeyote kuleta hoja mahsusi ya kutaka Katiba Mpya! Nchi nzima, vijana na wazee, watoto na vikongwe, mabibi na mabwana, waislamu kwa wakristu, wahindu na wasioamini wote waanze kuimba wimbo huu mmoja na kilio kimoja kisicho na woga “tunataka Katiba Mpya.”

Naam, wapinzani na chama tawala wote waanze kusema wakati umefika tunataka Katiba Mpya.

Historia imepiga kelele, ni wajibu wetu kuitikia, vinginevyo tutapiga kelele, na historia ikapita huku hatuna cha kushikilia. Tuukamate wakati, tuukumbatie sana na tuutumie kwani historia ya nusu karne ya Tanzania inayokuja, yumkini inaanza kuandikwa na sisi wenyewe.

Tuwarithishe watoto wetu na watoto wao kitu kizuri; tuwatengenezee mfumo ambao watajivunia. Iweje mababa wa Marekani miaka zaidi ya 200 waweze kuandika mojawapo ya katiba nzuri kuandikwa na wananchi?

Iweje Afrika Kusini nchi iliyotoka kwenye ubaguzi wa rangi waweze kuandika Katiba nzuri dunia kote? Leo hii, Kenya wameandika katiba yao wenyewe wakajivunia, iweje taifa hili tulioongoza harakati za ukombozi na tuliokuwa kilele cha diplomasia ya Afrika tushindwe au tuogope kuandika kitu chetu wenyewe? Tuukamate wakati, tusiuachie! Tuukamate wakati!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: