CCM Mwanza sherehe, Dodoma uasi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

PICHA mbili kinzani zilionekana mwisho ni mwa wiki iliyopita kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Moja nzuri saaaana na nyingine inatisha.

Jijini Mwanza kulikokuwa na kila aina ya shamrashamra za CCM kutimiza miaka 35 tangu kizaliwe, ilionekana katika picha ya kusisimua, kuhamasisha, kukonga nyoyo na kuvutia hata wasio wanachama.

Uwanja wa CCM Kirumba ulitawaliwa na rangi ya kijani na njano. Wapo waliocheza, walioshangilia kwa nguvu, waliopiga vigelegele na mbinja wakafurahia umri wa miaka 35.

Sherehe za jijini Mwanza zilizoanza kwa matembezi ya mshikamano, zililenga kukijenga chama na kuimarisha mshikamano wa wanachama. Walihamasishana, waliimba na kucheza miondoko ya Kwaito ya Afrika Kusini.

Lakini kule Dodoma ulinukia uasi. Wakati wenzao wa Mwanza walikuwa na shauku ya kumwona Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete; wabunge Dodoma walikaa kwenye vikao vya chama – Party Caucus – wakafikiana kutoonana na Rais Kikwete kwa madai amewasaliti kwa kukubaliana na wapinzani juu ya marekebisho mengine ya sheria ya marekebisho ya Katiba.

Picha ya Mwanza inaonyesha nguvu na uhai wa chama wakati ile ya Dodoma inaonyesha hofu, kukata tamaa, chuki, kunyoosheana vidole, kuzomeana na kutokuwa na imani na Rais Kikwete – mpasuko.

Usaliti

Miaka yote, wabunge wa CCM wametekeleza maagizo ya Rais Kikwete bila usaliti. Mwaka 2007 wakala njama kumfungia Zitto Kabwe alipomuumbua Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kutia saini mkataba mpya wa madini nje ya nchi.

Halafu wakatetea kama hawana akili nzuri watuhumiwa wote wa ufisadi. Novemba mwaka jana walipitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba bila wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha NCCR-Mageuzi.

Wabunge hao wa upinzani walitoka nje ya Bunge baada ya kuona CCM walikula njama kupitisha sheria dhalimu hivyo ingeathiri mchakato wa kupatikana katiba bora. Wakati wapinzani wakitoka nje, CCM walizomea na kutoa kila aina ya kejeli. CHADEMA na NCCR-Mageuzi hawakukata tamaa, waliamua kumfuata Rais Kikwete na kuikosoa sheria hiyo mbele yake.

CHADEMA, NCCR, CUF na asasi za kiraia walifanikiwa kumlainisha Rais ambaye sasa ameagiza yafanyike marekebisho katika baadhi ya vifungu vya sheria hiyo kwa kuzingatia maafikiano yake na CHADEMA.

Wabunge wa CCM wanaona wamesalitiwa na mkuu wa nchi, eti nao wanapanga kukwamisha marekebisho mengine. Wanaona kukubali mapendekezo ya CHADEMA ni kulamba matapishi yao. Wanajiuliza watatetea kwa hoja zipi?

“Sisi tumekaa hapa (bungeni) kwa zaidi ya siku mbili na akili zetu timamu, tukapitisha muswada ule, anakutana (Rais Kikwete) na CHADEMA dakika chache anatuletea marekebisho! Hiyo ni dharau na hatuwezi kukubali,” alilalamika mbunge mmoja wa CCM.

Katika sherehe za Mwanza, Rais Kikwete alisema eti na wao wana mapendekezo manane katika marekebisho hayo.

Maswali

Kama Rais alijua muswada haukukamilika kuwa sheria na kuna mambo ya msingi hawakuyaingiza, kwanini alitia saini haraka wakati wapinzani walimsihi asiusaini? Atawaambia nini wale wazee wa CCM aliowaita Diamond Jubilee ili wamsikilize anavyowanga CHADEMA? Busara ya kujua mambo hayo manane imekuja lini?

Tatizo ndani ya CCM ni hilo. Asubuhi wakati wanaanza vikao wabunge huomba dua:

“Ewe Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Dunia; umeweka katika Dunia serikali za wanadamu na mabunge ya mataifa ili haki yako itendeke. Twakuomba, uibariki nchi yetu idumishe uhuru, umoja, haki na amani. Umjalie Rais wetu hekima, afya njema na maisha marefu ili pamoja na wanaomshauri, wadumishe utawala bora. Utuongezee hekima na busara, sisi wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utupe uwezo wa kujadili kwa dhati, mambo yatakayoletwa mbele yetu leo, ili tufanye maamuzi sahihi yenye manufaa kwa watu wote na ustawi wa nchi yetu. Amina.”

Baada ya dua hiyo, wakikaa chini hekima na busara waliyoomba inapotea kwa kulinda maslahi ya CCM na kutii maagizo ya Rais. Haya ni makosa ya kujitakia.

Katika sheria ya marekebisho ya katiba, kuna kifungu kinazuia kufanya kampeni dhidi ya masuala yaliyoitwa ya msingi na atakayethibitika mahakamani kufanya hivyo, atahukumiwa kifungo cha hadi miaka saba jela au faini au adhabu zote mbili.

Lakini wabunge haohao wa CCM, wakati wanapitisha Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha Haramu adhabu ni kifungo chini ya miaka mitatu. Kosa kubwa la uhujumu uchumi wa nchi kifungo ni kidogo kuliko cha mtu anayetumia demokrasia kueleza udhaifu katika sheria. Hapa wamelenga upinzani.

Kenya inaweza kuwa mfano mzuri wa namna udhalimu unavyowarudia watunzi wa sheria dhalimu. Viongozi wa serikali ya Kenya hawafikiri kwamba sheria dhalimu waliyoipitisha ya kuzuia watu kutoa maoni tofauti kuhusu marekebisho ya Katiba ingeweza kuwauma hata wao.

Lakini mara walipoanza kuinadi Katiba iliyorekebishwa baada ya mapigano na mauaji ya wao kwa wao baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, ‘wapinzani’ wa marekebisho hayo wakawa kikaangoni.

Mawaziri, wabunge na wafuasi wa kambi ya Hapana wakaonja shubiri. Naibu Waziri wa Barabara, Wilfred Michage pamoja na wabunge Fred Kapondi na Joshua Kutuny walijikuta kwenye mikono ya polisi kwa madai ya kutoa kauli za chuki.

Tabia ya kutunga sheria kwa kuangalia watakaoathirika ndiyo inawatafuna CCM. Rais amegundua udhalimu, wabunge wake wanatahayari.

Wanapinga adhabu kubwa dhidi ya watakaokamatwa kwa matumizi ya fedha haramu kwa vile wanajua, kwa kiasi kikubwa wanashiriki uhalifu wa matumizi au utoroshaji wa fedha haramu wengi ni makada wa CCM.

Ushahidi upo kwamba mafisadi, wahujumu uchumi, wezi, walarushwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya ni makada wa CCM na Rais Kikwete, mwaka 2006 alisema anawajua. Hata hivyo aliwasamehe kama alivyowasamehe mafisadi wa EPA, walarushwa ya rada, na hakuwawajibisha waliofanya ufisadi kupitia kampuni ya Richmond.

Kama wabunge wa CCM wanataka kujitazama upya walivyotumiwa vibaya kulinda mfumo wakati hadhi yao mbele ya jamii imeshuka, wapinge pia mshikamano wa kifisadi katika masuala mengine.

Serikali imewalipa posho kubwa wabunge ili wawe wanapitisha mapendekezo ya serikali ambayo baadhi ni ya ovyo na pia kuwaziba wasipigie kelele mishahara na posho kubwa za watendaji wa serikali.

CCM ndio mwaka 2005 walipitisha Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu iliyoweka matabaka ya viwango kati ya watoto wa matajiri na maskini. Hakuna aliyepinga vigezo.

Matokeo ya sheria ile, watoto wa viongozi, mawaziri na vigogo wanapewa mikopo ilhali wa maskini wanakosa. Bodi inashindwa kudai fedha kwa sababu miongoni mwa wadaiwa sugu ni watoto wa Rais.

Je, kuna mbunge aliyetayari kumwambia Rais, “Sasa inatosha?” Kama wamekosa imani naye, basi wapige kura ya kutokuwa na imani naye kwa mujibu wa Katiba, maana yeye anaweza kuvunja Bunge. Akithubutu, wengi wao hawatarudi mjengoni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: