CCM: Mwisho wa nyakati?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version

AGOSTI mwaka 2006, akiwa hata hajatimiza mwaka mmoja madarakani, Rais Jakaya Kikwete alipata mmoja ya mitihani yake ya kwanza.

Mtengeneza filamu maarufu na raia wa Austria, Hubert Sauper, alikuwa ametoa filamu aliyoipa jina la Darwin’s Nightmare iliyoeleza mahusiano baina ya biashara ya silaha katika nchi za maziwa makuu na ile ya samaki aina ya sangara.

Baada ya filamu hiyo kutoka na kuzua mjadala hapa nyumbani na katika bara la Ulaya kwa ujumla, Kikwete akaamua kujibu mapigo.

Akaita mkutano na wazee wa mkoa wa Mwanza –kiini cha filamu ya Sauper na ‘kumpa vidonge vyake’ mzungu huyo katika namna ambayo iliwakumbusha Watanzania wengi enzi za Mwalimu Nyerere.

Kikwete alizungumza kwa kujiamini, kujiachia na nguvu ya mamlaka ikionekana kabisa kuwa nyuma yake. Huyo ni Kikwete wa mwaka 2006.

Peleka mkanda mbele hadi mwaka 2011. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Kikwete alizungumza na wananchi katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi ambapo, pamoja na mambo mengine, alizungumza kuhusu hali ya usalama nchini.

Alitumia sehemu kubwa ya hotuba hiyo kueleza namna chama cha upinzani cha CHADEMA kinavyohatarisha amani nchini kwa kuchochea vurugu.

Wakati nikimtazama Kikwete yule wa Februari 2011, nilimuona ni tofauti mno na yule aliyezungumza Mwanza Agosti mwaka 2006.

Hakuonekana kujiamini. Hakujiachia na ungeweza kugundua haraka kuwa ile nguvu ya kimamlaka iliyokuwa ikimwakia miaka sita iliyopita, imeanza kufifia.

Kwangu, ile ilikuwa picha ya kusikitisha sana ya rais Kikwete. Lakini, zaidi ya lugha ile ya mwili niliyoisoma, nilibaini jambo jingine baya zaidi: hotuba ile haikuwa na kitu.

Mara baada ya Kikwete kumaliza hotuba ile, nilijua wazi kuwa sasa siku za CCM kubaki madarakani zinaelekea ukingoni. Kama imefikia hatua ya kada wa chama anazungumza kwa upole namna ile na tena bila ya kujibu hoja za msingi za wapinzani; ni dhahiri mustakabali wa chama u shakani.

Siku chache baadaye, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, akazungumza. Hakuwa na jipya. Ni yaleyale aliyoyaeleza Kikwete. Bado naye hakujibu hoja za CHADEMA.

Mimi huwa sipendi kutumia kiholela neno kada wa chama. Lakini, Kikwete na Chiligati ni watu wanaostahili kuwa makada wa chama chochote cha kimapinduzi kama CCM.

Wamepikwa katika chama. Wametumika katika majeshi na wanakijua chama chao nje na ndani. Kama CCM ingetakiwa kufufuliwa leo, ni makada wa aina hii ungetaraji watumwe kukitetea chama na serikali yake. Lakini wameshindwa.

Na hili silisemi mimi. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amewaambia CCM kuwa wanachotakiwa kufanya ni kujibu hoja za CHADEMA, si vinginevyo.

Hicho ndio hasa kitendo ambacho hakijafanywa kufikia sasa. Si serikali wala CCM waliothubutu kukabili kisawasawa hoja za kina Dk. Willibrod Slaa, mshindani mkubwa wa Kikwete katika urais mwaka jana.

Badala ya kujibu hoja, Kikwete akaamua kuwa mlalamishi akiomba huruma kwa Watanzania wanaofahamika kuwa wanapenda sana amani na utulivu na hawapendi vurugu.

Watanzania wangefurahi kama angetumia fursa ile kujibu hoja ambazo CHADEMA wanazitoa kwa wananchi dhidi yake, serikali yake na chama chake kipenzi – CCM.

Ni kweli Watanzania kwa hulka yao si watu wa vurugu. Lakini, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, huwa mara nyingi anasema kwa lugha ya kiingereza:

“A hungry man is always angry (Mtu mwenye njaa, siku zote huwa na hasira).”

Imekuaje CCM inashindwa kushindana kwa hoja na CHADEMA? Ina vyombo vingi vya propaganda, ina fedha zaidi, ina wanachama zaidi na ina mtandao mkubwa zaidi. Inashindwa nini kama si ukweli kuwa mwisho wake umekaribia?

Nimewahi kukutana na wana CCM wengi katika maisha yangu. Mara zote, nimekuwa nikivutiwa sana na makada wa chama hicho kama vile Aggrey Mwanri angalau kwenye mazungumzo yasiyo rasmi.

Kama makada wote hawa wanazidiwa nguvu na wanashindwa kukisaidia chama chao kwenye ujenzi wa hoja, tena katika kipindi kifupi sana tangu umalizike uchaguzi mkuu uliokirudisha madarakani, dalili si nzuri kwake.

Chama cha siasa na serikali kinapoamua kumtumia mtu kama Steven Wassira kujibu hoja za wapinzani hakielekei kuzuri. Huyu watu wanamfahamu kwa jina la utani la Tyson. Ni lini Tyson bondia alizungumza mambo ya maana zaidi ya kubonda watu?

Inawezekana akina Wassira wanapata nafasi kwa vile wale ambao wangeweza kufanya kazi hiyo vizuri wamejiweka pembeni. Labda wamesusa au wamesoma alama za nyakati.

Watanzania hawawezi kubadilishwa mawazo kwa vitisho na u-Tyson. Kizazi hiki cha sasa ni cha watu werevu ambao wanaweza tu kulainishwa kwa maneno matamu na utatuaji wa kero zao.

CCM imedumu muda mrefu madarakani kwa sababu viongozi wake waanzilishi walikuwa wakizungumza lugha ya wananchi walio wengi. Wananchi wakawaamini na wakawapa dhamana ya kuwaongoza tena na tena.

Hakukuwa na vitisho wala hadaa. Vitisho ni hatua ya mwisho ya mtu anayeshindwa. Kama mwanao umemuahidi kitu na anakudai sana na umeona huwezi kutimiza ahadi yako, utaanza kumpiga mkwara.

Na nadhani hapo ndipo mahali ambapo CCM imefikia. Inajua na viongozi wake wanajua hawawezi tena kutimiza ahadi walizowapa wananchi. Wanajua hawawezi kujibu maswali yao magumu. Hawawezi kukidhi matumaini yao.

Nini kilichobaki baada ya hapo? Kilichobaki ni mikwara. Lakini mikwara ni hatua ya mwisho kabisa kwa anayeshindwa.

Ni sawa na kumsikiliza Muammar Gaddafi akizungumza hivi sasa. Anatumia vitisho na kujiamini. Lakini kama kuna jambo lililo dhahiri kwa sasa basi ni kwamba naye, siku zake za kubaki madarakani zinahesabika.

Utawala wa CCM na ule wa Gaddafi ni vitu viwili tofauti. Lakini sasa wanafanana kitu kimoja: wote wanaelekea ukingoni.

Katika hali kama hiyo, hakuna wanaloweza kulifanya kuepuka muanguko. Maandishi yapo ukutani tayari. Mwisho wa nyakati umewadia.

0718 81 48 75
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: