CCM ni wachovu, wamefilisika kifikra


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version

VIONGOZI na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanashangaza. Huweza kushupalia kupinga, kwa nguvu zao zote, ushauri fulani kwamba haufai, lakini huiga na kutekeleza kesho yake.

Viongozi kuwaaminisha wanachama wao kuwa jambo lililopendekezwa na wapinzani halitekelezeki au linalofanywa na wapinzani halifai, lakini baada ya siku chache hulamba matapishi yao.

Mifano ipo mingi. Katika kampeni za uchaguzi mwaka 2000, Chama cha Wananchi (CUF), kikiungwa mkono na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika ilani yake, kilisema kitafuta ada na michango kwa shule za msingi ili kitoe elimu bure.

CCM, kwa ubishi tu, walidai haiwezekani, hakuna pesa kiasi hicho. Lakini mwaka uliofuata yaani 2001, serikali ya CCM ikatekeleza sera ya upinzani kwa kufuta ada kwa shule za msingi na kuahidi kumpa kila mwanafunzi dola 10.

Kwa kuwa CCM ilichukua sera hiyo bila mandalizi ya kutosha, imeishia kutoa dola chini ya 5 huku baadhi ya shule, hasa zinazoshughulikia wenye ulemavu kama wa otizimu, zikiachwa.

Mwaka huu ilani za CUF na CHADEMA zimepiga hatua zaidi kwamba, wakishinda serikali watakazounda zitatoa bure huduma za afya na elimu hadi chuo kikuu. Hii ni neema.

Lakini wanachama wa CCM, ambao wengi ni maskini na hulalamikia watoto wao kushindwa kupata elimu ya juu kutokana na kukosa ada, wanaruka mdundiko kufurahia fikra zilizogota za mgombea wao wa urais kwamba haiwezekani.

Wanafurahia kuzidi kukamuliwa na sera ya CCM ya kuchangia huduma.

Hivi ni kweli wananchi hawataki huduma bure za afya kwa kila Mtanzania na elimu bora kwa watoto wao? Ni kweli wanafurahia ahadi za kujengewa viwanja vya ndege kuliko afya bure?

Wananchi wanapata fursa ya kusikiliza sera za upinzani na kwa utashi wao wakakataa badala yake wanapenda sera ya CCM ya kuchangia gharama?

Hivi wananchi hawana uwezo wa kugundua viongozi wao wamefilisika kifikra?

Wanataka wadanganywe hadi lini ili waerevuke wafikie kuwakataa CCM?

Wamesahau ghiliba za mgombea wao mwaka 2000 kwamba haiwezekani kutoa elimu bure lakini mwaka 2001 wakafuta ada? Nini kimewapata wana CCM hadi hawaoni, hawasikii wala hawahisi?

Wapinzani walipoibua wizi wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT), viongozi wa CCM walipinga na kudai ni uongo.

Baadaye ilibainika kuwa kweli umefanyika wizi, serikali ikalazimika kuweka mambo hadharani.

Je, huo si ushahidi mwingine wa kuonyesha viongozi wa serikali ya CCM waongo kwa asilimia 100 na watu wanaojali maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya nchi na raia wake?

Hadi katikati ya miaka ya 1990 mgambo wa serikali walikuwa wakifukuzana na wananchi mijini na vijijini wakidai kodi ya kichwa.

Wapinzani wakasema wakipata ridhaa ya kuongoza nchi watafuta kodi na michango mingine ya kinyonyaji, lakini serikali ya CCM ikadai haiwezekani kuendesha nchi bila kodi.

Baada ya uchaguzi mkuu mwaka 1995, serikali ya CCM ikalamba matapishi yake ikafuta kodi ya kichwa, ushuru wa magari barabarani (Road Tolls) na hatua kwa hatua ikafuta michango isiyo na tija. Wananchi wajiulize nani mwongo wapinzani au CCM?

Katika Bunge lililopita, mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Zitto Kabwe alizua tafrani alipodai kwamba katika Ilani ya CCM ya mwaka 2005, hakuna mahali popote palipoandikwa chama tawala kitajenga Chuo Kikuu cha Dodoma.

Zitto alisema CCM iliiga sera ya CHADEMA. Lakini mbunge wa Ukerewe (CCM), Dk. Getrude Mongela alimtaka Zitto aombe radhi kwa madai amelidanganya Bunge kwani mpango wa ujenzi chuo hicho umo ndani ya ilani yao.

Hata hivyo, Dk. Mongela alikiri ni kweli hakuna mahali panapokitaja chuo, lakini kimeainishwa katika mipango ya uboreshaji wa elimu ya juu.

Hivyo hoja ya Zitto inabaki kuwa CCM inatekeleza sera ya CHADEMA tena iliyopendekeza katika waraka mwaka 1993 kwamba mji wa Dodoma uendelezwe kwa kujenga taasisi za elimu ya juu kabla ya serikali kuhamia Dodoma.

Hivi sasa serikali inaimba wimbo wa CHADEMA kwamba haiwezi kuhamia Dodoma kwa vile mji huo, hauna miundombinu ya kutosha na taasisi nyingine zikiwemo za elimu ya juu. Wananchi wajiulize nani wababaishaji CCM au wapinzani.

Katika Ilani yake, CHADEMA inasema ikipewa ridhaa ya kuongoza itafuta nafasi za wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, itabaki na halmashauri na katika ngazi ya juu itaunda serikali za majimbo.

CCM wanapinga serikali za majimbo wakidai zitaleta ukabila na ubaguzi.

Lakini CCM (kama wataunda serikali) wamesaliwa na siku kugota ukingoni na kuukubali mfumo huo kwani nchi tatu kati ya tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatumia mfumo wa majimbo.

Mfumo wa majimbo hautaepukika nchi hizo zitakapoanza kujadili shirikisho la siasa la jumuiya hiyo.

Uganda, ni nchi nyingine iliyogawa nchi katika mikoa kama Tanzania lakini ina muundo wa majimbo. Ina mikoa ya Kati, Mashariki, Magharibi na Kaskazini.

Rwanda ina mfumo wa majimbo inayoyaita ‘intara’ na chini ya majimbo kuna wilaya (akarere) na halmashauri (umujyi).

Kabla ya 1 Januari 2006, Rwanda ilikuwa imegawanywa katika majimbo 12, lakini serikali ya chama cha Rwanda Patriotic Font (RPF) cha Pual Kagame iliunda majimbo matano tu (Mashariki, Magharibi, Kaskazini, Kusini, Kigali) yenye mchanganyiko wa makundi ya makabila.

Burundi imejigawa katika majimbo 17 wakati Kenya iliyoidhinisha katiba mpya hivi karibuni imegawanywa katika majimbo 18. Jiulizeni nani hawaoni mbali wapinzani au CCM?

Viongozi wa CCM ni kama nguruwe, huchafua huku na kule kule, lakini punde anageuka kula kule alikochafua awali na mfumo wake uko hivyo kimaisha. Kwa nini wana CCM wote wanalazimishwa wasione kichefuchefu hicho?

CHADEMA walipotumia helkopta katika kampeni za mwaka 2005, CCM walidai ni matumizi mabaya ya pesa na ni ghali kuliko mamia ya mashangingi waliyokuwa wanatumia.

Miaka mitatu baadaye yaani mwaka 2008 wakawa wamesahau walichosema mwaka 2005.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Tarime, chama hicho kilitumia helkopta mbili, na mwaka huu wamempa mgombea urais wao helkopta tatu.

Kwa nini wana CCM wanakuwa watumwa na uongo, ghiliba, udanganyifu na uzandiki wa viongozi wao?

Kwa uwezo huu wa wapinzani wa kubuni mambo yakatekelezwa na CCM ni ushahidi, vyama vya upinzani vimekomaa kiumri na kisera; vimeonyesha uchungu kwa nchi yao, raslimali zao, sasa viaminiwe kuongoza nchi. Tanzania bila wachovu, walafi, mafisadi CCM inawezekana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: