CCM sasa chama cha kisultani - Shibuda


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

“NDANI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuna viongozi wanaoilewa vema misingi na maadili ya chama, lakini wapo wanachama wasiojua chochote kuhusu chama chao. Ni wale waliovunwa kwa njia ya ufisadi na uanachama wa papo kwa papo. Hawa ndio wanaokivuruga chama chetu.

“Ni unafiki wa wazi kabisa kusema CCM bado ipo katika mstari wake uleule wa awali. Nikiwa kada ninayekijua vizuri chama hiki, siwezi kusema CCM ipo imara na imebaki katika mstari wake uleule ulioasisiwa na viongozi wetu. Siwezi kuwa mnafiki…”

Hiyo ni kauli ya mwanasiasa John Magale Shibuda (58), mbunge wa Maswa (CCM), Shinyanga, mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM mkoani humo, Mjumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Shibuda ni mmoja wa wanachama wa CCM waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya chama hicho mwaka 2005.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Shibuda anasema ndani ya chama chake kuna ombwe la uongozi linalotokana na chama hicho kuacha mwelekeo wake wa asili.

“TANU (Tanganyika African National Union) kwa upande wa Bara na ASP (Afro Shirazi Party) kwa upande wa Zanzibar, vilikuja na shabaha na malengo ya kukata kiu ya walioitwa watwana mbele ya wakoloni na masulutani,” anasema Shibuda.

Anasema vyama hivi viwili, kwa pamoja, vilisimama imara kupambana na “uyonyaji, usulutani na unyapara ambao ndiyo unaoitwa leo ufisadi.”

Shibuda anasema, “Wenzetu hawa (mafisadi) wameibua upya misingi ya ubepari, ukabaila na unyonyaji kwa kutumia mikataba.” Anasema kwa hali ya sasa, “hakuna mashaka kuwa CCM kipo njia panda.”

Anasema CCM “hakitabiriki wala hakijulikani kinakoelekea. Haijulikani kama dira ya chama ni katiba na kanuni zake au utashi wa viongozi.”

Anasema tayari chama hicho “kimewageuka wananchi. Kimefuata sera za chama cha kisulutani cha Zanzibar (ZNP)” ambacho kilikuwa chama cha kulinda maslahi ya mabwenyenye.

Kwanza, Shibuda anasema, “Natoa angalizo, kwamba CCM inapaganyishwa na viongozi wasio na elimu ya madrasa ya kukijua chama. Wajibu wa kwanza wa mwanachama ni kutii kanuni na imani za chama. Haiwezekani kuhubiri kuondoa unyonge, lakini wakati huohuo unashabikia unyonyaji.”

Kauli ya Shibuda imetokana na uamuzi wa NEC ya chama chake kuzuia wabunge wake kujadili masuala ya ufisadi bungeni, badala yake NEC imeagiza wabunge wajadili suala hilo ndani ya vikao vya chama.

Anasema, “CCM hakitakuwa chama cha siasa tena, utakuwa ni mkusanyiko wa watu waliokutana katika basi moja, lakini wakiwa wanaelekea safari tofauti.”

Shibuda anaonya, “Viongozi wa CCM wasijipe kazi ya Mungu – kuumba na kuhuisha. Ujinga una haki zake za utulivu na kulipuka. Sasa tusifike huko. Tusitumie uongozi kama pango la kutishana kwamba nitakufukuza uanachama.”

Anasema, “Uanachama wa chama cha siasa, si kadi, bali ni imani. Kuhama msikiti si kuondoka katika uislamu, wala kumkataa sheikh si kuukataa uislamu. Vilevile kuhama kanisa si kuhama ukristo, wala kumkataa mchungaji si kuukataa ukristo,” anasema kwa sauti ya kukaripia.

Shibuda ananukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba cheo ni dhamana, na “tusitumie cheo kudhalilisha wale wasionacho.”

Anasema kwa maoni yake, Bunge na CCM ni kama kuku na mayai, “Sote sisi tunahitajiana.” Anahoji, “Je, kutishia Bunge, kuzomea wanaopiga vita maovu, kunajenga ndoto za leo kwa maisha ya kesho?

Anasema kauli za NEC juu ya mapambano dhidi ya ufisadi zimeibua hoja kwamba “CCM kimeshindwa kulinda maslahi ya wananchi.”

Anasema, “Ni lazima chama kifike mahali kiache uchokozi wa kutumia dhamana za madaraka kudhulumu haki za umma.”

“Je, tunataka tuwe na Bunge la kulinda maslahi ya cheo cha mtu na utendaji binafsi wa cheo cha mtu aliyepo serikalini? Je, ni kweli akikosolewa mtu kama huyo na kukemewa, tunadhalilisha serikali?”anahoji.

Anasema katika mazingira hayo, hakuna mbunge hata mmoja anayezijua vema haki zake atakayekubali kuporwa haki zake za kikatiba za kuzungumza bungeni bila kuingiliwa.

“Binafsi niko gizani. Najiuliza hawa wenzetu wanataka kutueleza kuwa Bunge liwe na wajibu kwa maslahi ya umma au Bunge tuwe na maslahi na wajibu kwa mitaji ya makundi binafsi ya unyonyaji wa umma,” anahoji.

Shibuda anasema, “Nguo chafu hufuliwa kwenye mwanga ili uchafu huo uonekane na uondolewe. Nguo chafu huwezi kuisafishia katika giza. Vyeo hivi vya chama visitumike kufukia haki za wanyonge zinazolindwa na katiba ya CCM na ya nchi.”

“Ili CCM iweze kuvutia umma,” anasema Shibuda, “ni muhimu ikajiepusha na kauli zinazojenga uhasama katika kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi.”

Anasema kuna siku itafika, wapinzani wa kisiasa wa CCM watapata mtaji. Watasema, “Hawa wapo kwa ajili maslahi yao binafsi. Tusikifikishe huko chama chetu.”

Akizungumzia matatizo yaliyopo katika jimbo lake, Shibuda anasema wananchi wa Maswa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula; kunahitajika tani 2,209 za chakula cha nafaka ili kukabiliana na hali hiyo.

Anasema tatizo jingine kubwa linalokabili wilaya yake ni kukosekana kwa malisho kwa ajili ya wafugaji, jambo ambalo linasababisha wafugaji kuhama kutoka eneo moja hadi jingine.

Kuhusu elimu, Shibuda anajitapa kwamba jimbo lake ni miongoni mwa wilaya chache nchini zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta ya elimu.

Anasema kila mwaka anapeleka vijana zaidi ya 50 katika vyuo mbalimbali vya ualimu nchini kusomea kazi hiyo, ili mara wakishahitimu mafunzo yao warudi Maswa kuendeleza ndugu zao.

“Hapa napiga ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, ninatoa ajira; pili, ninakabiliana na uhaba wa walimu katika shule zetu,” anasema.

Anasema, “Mimi nimezama kwa wananchi. Mkaa wetu pale Maswa ni wa kinyesi cha ng’ombe. Watu ambao hawakuzoea hayo hawawezi kuja Maswa, ndiyo maana ninatengeneza vijana wa Maswa kufanya kazi hii ambayo haiwezi kufanywa na watu kutoka maeneo mengine.”

Wilaya ya Maswa ina kata 18, na Shibuda anasema amejitahidi kupeleka maendeleo kila kata.

Kuhusu kugombea urais katika uchaguzi ujao, Shibuda anasema atachukua fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.

Anasema, “Hakuna wa kumzuia kuchukua fomu kuchuana na rais wa sasa, Jakaya Kikwete. Nani anasema ana hatimiliki ya urais? Nitachukua fomu na kila anayetaka kugombea akiwamo Rais Kikwete ajue wazi kuwa kuna Shibuda ambaye ni moto wa kuotea mbali,” anasisitiza.

John Paulo Magale Shibuda alizaliwa mwaka 1950 huko Ndanda, wilaya ya Masasi. Ni mtoto wa Paulo Magale, askari wa zamani aliyeshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Ameoa na ana watoto watano.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: