CCM sasa wamevuna walichopanda


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version

JOSHUA Nasari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha ubunge Arumeru Mashariki.

Wakati Arumeru wakitafuta mbunge, kata saba nchini zilikuwa zinatafuta madiwani. Katika kata hizo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangazwa kushinda katika kata tatu tu.

CHADEMA wameshinda katika kata tatu na Chama cha Wananchi (CUF) wameshinda katika kata moja.

Hata hivyo, kwa aliyekuwa anafuatilia kampeni za chaguzi hizi kwa makini, alikuwa anatarajia anguko la chama hiki kinachozeekea madarakani.

Katika siku 30 za kampeni, CCM imeshindwa kunadi sera zake. Imeshindwa kueleza mipango yake ya sasa na ile ya baadaye. Imeshindwa kuonyesha kwa vitendo kuwa hiki ndicho chama kinachoongoza serikali.

Badala yake, CCM ilitumia siku za kampeni kuporomosha matusi, uwongo, ghiliba, vitisho na kufadhiri makundi ya wahuni kushambulia wafuasi wa upinzani.

Ni CCM iliyomtuma rais mstaafu Benjamin Mkapa kuvurumisha matusi na kumwaga ahadi ambazo alishindwa kutekeleza akiwa rais.

Ni Mkapa huyuhuyu ambaye, badala ya kueleza sera za chama chake na kile ambacho chama chake kimefanya katika miaka 50 ya utawala, alianza kuvurumisha kejeli na matusi kwa viongozi wa upinzani na wafuasi wao.

Mkapa alikuwa amepata fursa nzuri ya kujibu tuhuma za ufisadi; tuhuma za kuuza raslimali za taifa kama karanga na kwa “bei ya bure” na kuongeza umasikini; na tuhuma za kuuza nyumba za serikali kwa “bei ya sigara.”

Atakuwa amejuta. Kwanza, kwa chama chake kushindwa; lakini pili, kwa kutwishwa tuhuma nzito kuhusiana na kifo cha kipenzi cha wananchi, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Vitendo vya Mkapa katika kampeni vilifanya aonekane mtu wa shari na aliyekwenda Arumeru kufanya ulaghai. Wananchi wamemwadhibu – yeye na mwenyekiti wake wa CCM aliyemtuma.

Chaguo la CCM lina walakini. Watapelekaje kwenye kampeni Mkapa na Steven Wassira? Ni Wasira aliyepatikana na hatia ya kushiriki vitendo vya rushwa hadi akafungiwa kugombea ubunge kwa miaka mitano jimbo la Bunda.

Wasira, badala ya kujitafakari na kutazama alikotoka, aliamua kuporomosha matusi, kama moshi mchafu wa treni, kwa yeyote anayeunga mkono upinzani au kuushabikia.

Naye Livingstone Lusinde ambaye, kama alivyo Wassira, tayari amemaliza vyama – akitoka huku na kwenda kule, alijiingiza katika matusi.

Hata kile anachoita sera za CCM, chama alichodandia juzijuzi tu hazifahamu; akaishia kuwa kinara mkuu wa mporomosho wa matusi kwenye majukwaa.

Lakini funga mwaka ni pale Edward Lowassa, naye alipojitokeza jukwaani kumnadi mgobea wa chama chake, Sioi Sumari – mkwe wake.

Nani hajasikia jina la Lowassa? Yule anayetuhumiwa kushiriki kutoa, kwa upendeleo, mkataba wa kufua umeme kwa kampuni ya Richmond Development Company.

Ni yuleyule Lowassa ambaye alilazimika kujiuzulu nafasi ya waziri mkuu, kutokana na mkataba wa Richmond.

Ni mkataba wa Richmond uliozaa kampuni nyingine ya kufua umeme ya Dowans; kampuni iliyoingia kinyemela na inayoendelea kutesa wananchi kwa madai ya fidia na gharama kubwa za umeme.

Ni Lowassa wa historia hiyo, aliyejiuzulu lakini anatajwa kuwa alistaafu – na yeye hataki kusahihisha upogo huo kwa kuwa unamnufaisha kimaslahi – aliyesimama jukwaani kumnadi mgombea wa CCM.

Akihutubia mkutano, katika eneo la Patandi, Lowassa pamoja na lundo la tuhuma zinazomkabili, alijifanya hamnazo na kusema, “Mimi ni mtu wa vitendo, sitaki porojo.”

Hata kama ingetokea kwa bahati mbaya ikawa kweli, kwamba yeye ni mtu wa vitendo; aliyekuwa anaombewa kura Arumeru hakuwa Lowassa. Alikuwa Sioi. Je, alitaka kueleza kuwa mkwe wake akichaguliwa, basi ataendesha jimbo hilo kwa maelekezo ya Lowassa?

Akasema wananchi wa Arumeru Mashariki wakimchagua Sioi, watakuwa wamemaliza “mjadala wa matizo ya ardhi, maji na umeme kwa sababu CCM imetambua na kusikia matatizo yao katika uchaguzi huu mdogo.”

Lowassa anajua kuwa tatizo la ardhi, maji na umeme limekuwapo Arumeru kabla ya Tanganyika kupata uhuru. Anajua kuwa huu ni uchaguzi wa 20 tangu uhuru; na uchaguzi wa tano tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Lakini anasema CCM imetambua tatizo hili na kulisikia kutokana na uchaguzi huu! Na huyu amekuwa waziri wa maji kwa miaka mitano; waziri wa ardhi kwa miaka mitatu na waziri mkuu. Hakuna alichofanya.

Kama alichukua maji Arumeru na kuyapeleka Monduli, kwa nini hakusambaza kwanza maji hayo Arumeru?

Kwa kauli zake, Lowassa alikuwa anawaomba wananchi wakazi wa Arumeru, wasikichague chama chake – CCM, kwa kuwa kimeshindwa kutatua matatizo hayo kwa miaka 50 ya uhuru.

Lakini Lowassa anapata wapi ujasiri wa kupanda jukwaani na kuwaomba wananchi wamchague mgombea wa CCM?

Leo hii, Tanesco wanahaha kutafuta fedha za kununulia mafuta ya majeneta ya umeme wa dharula; kulipa wanasheria wa kupambana na makampuni ya swahiba wake mkuu, Rostam Aziz.

Badala ya Tanesco kutumia fedha inayopata kuboresha maisha ya wafanyakazi wake na miundombinu yake ya umeme, inalazimika kuingia kwenye mikataba mingine ya kinyonyaji kwa kuwa mradi wa Lowassa ulioitwa wa “umeme wa dharula,” umekuwa mradi wa kudumu wa kulinyonya taifa.

Inawezekana Lowassa amesahau haya. Chama chake kimesahau. Rais wake, Jakaya Kikwete kasahau pia. Lakini wananchi wengi, wakiwamo wa Arumeru, bado wanakumbuka.

Wanakumbuka jinsi Lowassa alivyopindisha maamuzi halali ya bodi ya zabuni ya Tanesco na kuamuru kuipa kazi kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na ofisi, sifa, fedha wala ujuzi wa kufanya kazi iliyoomba.

Hivyo basi, ukiangalia kwa makini jinsi CCM ilivyoshindwa vibaya katika chaguzi hizi, utaona kushindwa kwake, pamoja na mengine mengi kama dharau, kutotimiza ahadi, mchoko, kunatokana na watu ambao kiliwabeba ili wakakisemee.

Wengi waliotumwa hawakuwa wasafi. Wachache waliosalia, ama hawapewi nafasi au wakipewa wanazitumia nafasi hizo kujijenga binafsi. Huku ni kuishiwa na kutafuta ujana uzeeni.

Ndiyo maana CCM sasa, kwa kuwa imeishiwa sera, imeamua kuendeshwa kwa kushabikia matusi, ufisadi, vitisho, hujuma, vurugu na umwagaji damu. Hoja za kukitetea zinajengwa kwa poropaganda chafu – uwongo, hila, wizi na uzushi.

Hii ni kwa sababu, kukirejesha chama hiki katika misingi yake ya asili – ‘rushwa adui wa haki, ni mwiko kutoa au kupokea rushwa; cheo ni dhamana; na nitasema kweli daima’ – ni jambo ambalo haliwezekani tena.

Yote haya wananchi wanayaona. Wanayaelewa hasa pale wanapokuwa wamepata msaada wa kufafanuliwa jukwaani au katika mijadala mbalimbali. Arumeru ni mfano.

Kwa mwendo huu, CCM ijiandae kuaga, angalau kwa miaka mitano au kumi, kukaa pembeni na kujifunza jinsi nchi inavyoweza kutawaliwa kidemokrasi.

0
Your rating: None Average: 3 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: