CCM sasa yatota Tarime


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Makamba atuma Makongoro kwa JK
Atakiwa kumkabili Enock Chambiri
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kupasuka wakati huu kinapoelekea katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani wilayani Tarime mkoani Mara.

Taarifa mpya zinasema, Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba baada ya kutuhumiwa kwamba ni yeye aliyechochea mpasuko huo, mwishoni mwa wiki alimpa ujumbe mwenyekiti wa mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere uwasilishe kwa Rais Jakaya Kikwete.

MwanaHALISI limefahamishwa kwamba Makongoro, mtoto wa muasisi wa chama hicho, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amemfuata Kikwete Dar es Salaam ili kumjulisha athari za mpasuko huo kwa chama chake na hatua ambazo anatakiwa kuchukua.

Kwa mujibu wa habari hizo, makundi yaliyoko Tarime na mkoani Mara kwa ujumla, yanahusishwa na viongozi maarufu wa chama hicho Christopher Gachuma na Enock Chambiri.

Gachuma ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Chambiri aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo.

Ilikuwa ni NEC iliyowaengua Chambiri na Gachuma katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa CCM mkoani Mara kwa kile kilichoitwa, “kumaliza makundi ya Chambiri na Gachuma.”

Inaelezwa kwamba hatua ya Makamba kufikia nyumbani kwa Gachuma na kumbeza Chambiri imerudisha upya uhasama huo.

Katikati ya mvurugano ndani ya CCM polisi wanasemekana kuamriwa kukamata mgombea ubunge na mgombea udiwani wa Chadema “kwa shabaha ya kuwadhahalisha mbele ya wapigakura.”

Juzi Jumatatu, polisi walimkamata mbunge wa Chadema, Chales Mwera, mgombea udiwani John Heche, Mkurugenzi wa Vijana John Mnyika na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) Dk. Beny Kapwani baada ya kuwavizia wakitoka katika mkutano wa hadhara.

Inaelezwa kwamba mgombea na timu yake ya kampeni walikuwa wanatoka katika kijiji cha Buhemba kufanya kampeni.

Taarifa kutoka ikulu na katika timu ya kampeni ya CCM mjini Tarime zinasema, ujumbe wa Makongoro kwa Kikwete ulimwomba Kikwete “kumuagiza Chambiri aache mara moja kuhujumu mgombea wa chama chake.”

Inaelezwa kwamba Chambiri amekerwa na hatua ya wapambe wa Gachuma kutamba kuwa hatua yao ya kumpitisha Christopher Kangoye inalenga kufuta enzi za Chambiri mkoani Mara.

Upande unaopingana na Chambiri unadaiwa kuweka vijana mitaani ambao wanapita na kusema kuwa “Chambiri anataka kuzikwa kisiasa.”

Taarifa zinasema ni kauli hizo za kejeli ambazo zimemfanya Chambiri kusinyaa na kuondoa moyo kwenye kampeni za mgombea wa CCM. Inadaiwa pia kwamba Makamba amebariki hali hiyo iendelee.

Lile linaloitwa kundi la Chambiri, habari zinaeleza, linasema mgombea wa CCM hakubaliki na linamwona mgombea wa Chadema, Charles Mwera Nyanguru kuwa ndiye anayefaa.

Mwera anatajwa kama mtu anayekubalika kwa wengi kwa kuwa katika uongozi wake kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, kwa mwaka mmoja tu, ameleta mabadiliko makubwa katika maendeleo.

Moja ya mambo makubwa ambayo wananchi wengi wanakiri amefaulu kufanya ni halmashauri hiyo kumudu kulipia karo za wanafunzi wanaoingia sekondari za serikali.

Taarifa zinasema, Makongoro amefanikiwa kukutana na Kikwete na kumkabidhi ujumbe wa Makamba.

“Ndiyo Makongoro amekutana na rais na kumwambia kuwa kampeni za CCM zinahujumiwa na kundi la Chambiri na Kikwete asipoingilia kati, hali itakuwa mbaya zaidi,” kimesema chanzo kimojawapo.

Lakini wakati Makamba ametuma ujumbe kwa Mwenyekiti Kikwete, mwenyewe anakabiliwa na tuhuma nzito za kupendelea kundi la Gachuma wakati anajua fika kuwa hatua yake hiyo inasononesha kundi la Chambiri linalotuhumiwa kuhujumu kampeni za mgombea wa CCM.

Inasadikiwa kuwa Makamba, ambaye yuko wilayani Tarime kutia nguvu kampeni hizo, kwa sasa amehamia kimakazi kwenye nyumba ya Gachuma, iliyoko kilomita chache kutoka Tarime, badala ya kuishi hotelini kama anavyoishi Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa.

Msekwa ambaye ndiye aliyezindua rasmi kampeni za kumnadi mgombea wa CCM, Kangoye, amekuwa akiishi katika hoteli mjini Sirari.

“Ukweli huu unashangaza na kutia shaka sana kama ni kweli Katibu Mkuu anataka kutatua tatizo la mpasuko ndani ya chama ambalo linavuruga kampeni za mgombea tuliyemteua wenyewe kugombea,” amekaririwa akisema mwana CCM aliye karibu na timu ya kampeni ya mgombea huyo.

“Kwanini yeye ( Makamba) akae kwenye nyumba ya Gachuma ambaye anaongoza kundi linalopingana na kundi jingine linalotajwa kuhujumu mgombea… mbona Makamu (Makamu Mwenyekiti, Msekwa) anaishi hotelini?” anauliza.

Habari hizo zinafichuka wakati huu CCM ikisemekana imekumbwa na mgawanyiko mkubwa unaotishia uimara wa kampeni zake kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani katika jimbo la Tarime.

Zipo taarifa za kuashiria kuungwa mkono kwa muono wa Katibu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) wa Mkoa wa Mara, Chacha Waitara, aliyesema kwamba kampeni za CCM zimepoteza mwelekeo kutokana na mgawanyiko uliopo ndani ya chama chenyewe.

Katibu huyo wa UV-CCM amehamishiwa mkoani Dar es Salaam ambako amesema hayuko tayari kuhamia kwani hawezi kuwa mtumwa wa Mwenyekiti wa UV-CCM, Emmanuel Nchimbi, na amesema atarudi Tarime kusaidia kampeni.

Hata hivyo, mwelekeo wake katika kampeni hizo ni kutaka wananchi wa Tarime wampigie kura mgombea wanayemuona anafaa, badala ya kukubali kuchagua mtu ambaye hawawezi kumtarajia kuwaletea maendeleo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: