CCM na sera za unyang’anyi Ngorongoro, Loliondo


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 May 2013

Printer-friendly version

KAMBI rasmi ya upinzani bungeni imefumua pango la ufisadi katika Wizara ya Utalii na Maliasili na kutuhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya viongozi wake, kutumia sera ya uporaji wa maliasili za taifa, udhalilishaji wafugaji na ufukarishaji Wamaasai katika Ngorongoro na Loliondo. Ifuatayo ni sehemu tu ya hotuba ya Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini na Msemaji wa Kambi ya upinzani katika wizara hiyo kama ilivyowasilishwa bungeni Jumanne hii:

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 27 Aprili 2006, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo aliunda kamati maalum ya uchunguzi ili kubaini matatizo ya tasnia ya uwindaji wa kitalii nchini.

Kamati ya Bw. Diallo iligundua, pamoja na mambo mengine, licha ya biashara ya uwindaji wa kitalii kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni, biashara hiyo inaingiza fedha kidogo nchini Tanzania – wastani wa dola za Kimarekani milioni tisa tu kwa mwaka, wakati Zimbabwe, inaingiza dola milioni thelathini.

Aidha, Kamati iligundua makampuni mengi ya uwindaji hayaajiri wataalam wa ndani ila huwatumia wananchi kwa kazi ndogondogo wakati wa msimu wa uwindaji. Makampuni haya pia yanawatumia wawindishaji kutoka nje ya nchi badala ya kutumia wawindishaji bingwa wa Kitanzania.

Vilevile, kamati ilibaini licha ya kuwepo makampuni mengi yanayomilikiwa na raia wa Tanzania, makampuni machache ya kigeni yanamiliki idadi kubwa ya vitalu vya uwindaji ambavyo vina wanyama wengi ukilinganisha na vitalu vya makampuni ya wananchi ambavyo viko kwenye maeneo ambayo hayana wanyama wengi.

Kwamba idara ya Wanyamapori haisimamii kikamilifu tasnia hii; na haina taarifa muhimu kuhusu vitalu na thamani yake halisi. Taarifa ya kamati hii, kama ilivyo kwa ripoti nyingine, haijawahi kutolewa hadharani na wala kuwasilishwa bungeni.

Kamati ya Diallo ilitokana na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010, ambayo iliahidi wananchi kuwa serikali ya chama hicho itaekeza nguvu zake katika kuhifadhi, kulinda, kuendeleza, kudumisha na kuvuna maliasili kwa manufaa ya taifa. Ahadi hiyo ilirudiwa katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/2015.

Tuliambiwa pia kwamba CCM katika Ilani yake ya 2005 itahimiza “... miji ianzishe bustani za ufugaji wa wanyamapori (zoos) kwa maonyesho.”  Hadi sasa, hakuna bustani ya wanyamapori hata moja iliyoanzishwa; na kwamba ahadi hiyo ilipotea kabisa katika ilani ya mwaka 2010!

Kama tutakavyothibitisha hapa, serikali ya CCM imeshindwa kabisa kutekeleza mapendekezo ya kamati ya Diallo. Badala yake, imeelekeza nguvu katika kudidimiza na kudhoofisha uhifadhi, ulinzi na uendelezaji wa maliasili za nchi.

Serikali ya CCM sio tu imeelekeza nguvu kubwa katika uvunaji haramu wa maliasili za nchi, bali pia imefanya hivyo kwa manufaa ya wafanyabiashara wa kigeni wakishirikiana na wafanyabiashara wachache wa ndani ya nchi na viongozi waandamizi wa chama hicho na makada wake.

Mwaka 2009 Bunge hili liliunda kamati nyingine ya uchunguzi wa matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wananchi wa Liliondo, ambapo wananchi walidai kuchomewa nyumba zao moto na wanawake kudhalilishwa na jeshi la polisi.

Taarifa ya Kamati hiyo, iliyoongozwa na Naibu Spika wa sasa wa Bunge, Job Ndugai, nayo haikuwasilishwa bungeni; na kwa kadri ya ufahamu wetu, nayo imezikwa kwenye kaburi la ofisi ya spika.

Matokeo yake, mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo kwa upande mmoja; na Serikali ya CCM na kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomilikiwa na mfanyabiashara wa kutoka Oman kwa upande mwingine, umezidi kuwa mkubwa.

Hii imethibitishwa na maasi ya wananchi wa Loliondo dhidi ya CCM yaliyovyoshuhudiwa mwezi uliopita na viongozi na makada wa chama hicho waliopo ndani ya bunge hili.

Mheshimiwa Spika,
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, 28 Julai 2007, alipokea taarifa ya kitafiti juu ya uwindaji haramu katika pori Tengefu la Selous na maeneo yanayolizunguka.

Taarifa hii iliandaliwa na Bw. Baruani Mshale wa kutoka shule ya masomo ya misitu na mazingira ya chuo kikuu cha Kale nchini Marekani.

Bw. Mshale anasema katika taarifa yake, kumekuwa na “maslahi haramu” – vested  interests - kati ya serikali na wafanyabiashara wa uwindaji wa kitalii wa nje; na ambayo yamesababisha serikali kufanya maamuzi yasiyofaa kwa wananchi ikiwamo kuwanyima wanavijiji faida zitokanazo na utajiri wao wa maliasili.

Mtafiti anataja viashiria vya maslahi hayo haramu, ni pamoja na mvutano kati ya mkurugenzi wa wanyamapori na aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii; na uamuzi wa rais kupangua baraza lake la  mawaziri ambapo waziri husika aliondolewa kwenye wadhifa wake.

Kinachoonekana kuwa maslahi haya haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu wachache yanajulikana serikalini, Bw. Mshale alimueleza ifuatayo waziri huyo: “...inawezekana nakukumbusha kitu ambacho tayari unakifahamu!”

Kambi rasmi ya upinzani inaamini kuwa maslahi haya haramu ya kisiasa katika sekta ya uwindaji wa kitalii, yamekithiri mno ndani ya CCM na serikali yake; na kwamba yanahusisha viongozi na watendaji waandamizi ndani ya chama na serikali.

Kwa mfano, mwaka 2009 shehena ya pembe za ndovu zenye uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya zilizoripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya Vietnam. Shehena iliyokamatwa  ilisafirishwa na kampuni ya wakala wa meli ya Sharaf Shipping Co. Limited.

Kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA), Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana ndiye anayemiliki robo tatu ya hisa za Sharaf Shipping Co. Ltd., wakati robo iliyobaki ya hisa hizo inamilikiwa na mtu aitwaye Rahma Hussein.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ina taarifa kwamba Rahma Hussein ni mke wa Bw. Kinana! Sio tu kwamba kampuni ya katibu mkuu wa CCM na mkewe imehusishwa na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kutoka Tanzania, kampuni hiyo inaelekea kutoa ajira haramu kwa wageni.

Wakati shehena ya meno hayo ya tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena hiyo zilionyesha kibali cha kusafirisha shehena kilisainiwa na raia wa India, anayeitwa Samir Hemani, tarehe 13 Novemba 2008. Hemani alikuwa Meneja wa Fedha na Utawala wa kampuni ya Sharaf Shipping.

Nazo nyaraka za Idara ya Uhamiaji zinaonyesha wakati Hemani anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya meno ya tembo hayo kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali chake cha kuishi nchini kilikuwa kimeisha tangu 7 Mei 2008.

Kutokana na hali hiyo, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali hii ya CCM, itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu ushiriki wa katibu mkuu wa CCM katika kusafirisha kiharamu nyara za serikali ambazo kwa vyovyote vile zinathibitisha kuwepo kwa ujangili wa kutisha unaohusu wanyamapori nchini.

Tunaitaka serikali pia itoe kauli juu ya kuhusika kwa katibu mkuu wa CCM katika kuajiri wafanyakazi wa kigeni ambao walikuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Spika,
Tume ya rais ya kuchunguza kero ya rushwa iliyoongozwa na Joseph Sinde Warioba ililalamikia kile ilichokiita “ukaribu wa wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa” ambao ulianza kujitokeza mwanzoni mwa kipindi cha pili cha serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Tume ya Warioba ilitoa mfano wa makampuni ya Kigoma Hill Top Hotel, Shenis Commercial Ltd., Tile and Tube Ltd., Royal Frontier (T) Ltd., Game Frontier (T) Ltd. nee MNM Hunting Safaris Ltd., ambayo yanamilikiwa na mfanyabiashara Mohsin Abdallah, mkewe Nargis Abdallah, pamoja na washirika wao wengine kibiashara.

Mohsin ni kada maarufu wa CCM aliyewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho. Kada huyu maarufu ameendelea na ushawishi mkubwa ndani ya serikali na hasa hasa katika wizara ya maliasili na utalii.

Zaidi ya hayo, kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya tume ya Warioba miaka 17 iliyopita, inaelekea ushawishi mkubwa alionao kada huyu wa CCM unatoa uvundo na harufu mbaya ya ufisadi.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamati ndogo ya mazingira, kampuni tatu zenye majina yanayoelekea kufanana na zenye ofisi katika jengo moja ni Royal Frontiers of Tanzania Ltd., Game Frontiers of Tanzania Ltd., Western Frontiers of Tanzania Ltd.

Wanahisa wake ambao wananasaba za kifamilia; na  hivyo kuleta hisia kuwa lengo la sheria na kanuni ya kuzuia mtu mmoja kumiliki vitalu zaidi ya vitano, linapuuzwa kwa ujanja wa kusajili makampuni mapya na yenye majina tofauti.

Mohsin Abdallah ametajwa pia na Shirika la Upelelezi wa Masuala ya Mazingira (Environmental Investigations Agency - EIA) kuwa ni mmoja wa majangili wakubwa wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo, lakini serikali haijamchukulia hatua.

Mohsin siyo mfanyabiashara na kada pekee wa CCM mwenye maslahi yenye mashaka katika sekta ya uwindaji wa kitalii. Ripoti ya kamati ya Diallo, imetaja makada kadhaa waandamizi wa chama hicho wenye maslahi ya aina hii na baadhi yao wako humu ndani ya Bunge.

Ripoti imetaja makampuni ya Coastal Wilderness (Tz) Ltd., ambayo wakurugenzi wake, ni Napono Edward Moringe Sokoine na Namelok Edward Moringe Sokoine.

Nyingine ni Enzagi Safaris (Tz) Ltd., ambayo wakurugenzi wake ni Makongoro Nyerere na Muhamed Seif Khatib; huku kampuni ya Said Kawawa Hunting Safaris, ikiwa na wakurugenzi Chande Kawawa na Hassan Kawawa na M.S.K. Tours & Hunting Safari Co., ikimilikiwa na Muhamed Seif Khatib.

Mheshimiwa Spika;
Eneo jingine ni hili la hifadhi za Ngorongoro na Loliondo ambayo yanakaliwa na jamii ya Wamaasai. Kwa mujibu wa taarifa za kitafiti, ni kwamba Wamaasai wameishi katika maeneo hayo tangu karne ya 18.

Kabla ya mwaka 1959 eneo hili lilikuwa ni sehemu ya maeneo ya Serengeti – Ngorongoro ambayo yalikuwa yakikaliwa na wafugaji wa Kimaasai.

Ushahidi wa suala hili ni taarifa ya tume ya uchunguzi ya CCM iliyoundwa na katibu wake mkuu, Abdulrahman Kinana ambayo iliongozwa na Mwigulu Nchemba, naibu katibu mkuu, Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa ya tume ya Nchemba, ukosefu wa ardhi ya kuendeshea shughuli za kiuchumi, ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha wakuu wa kaya kukimbia familia zao.

Ukosefu wa ardhi unaosabisha kukithiri kwa umaskini ni wa kutengenezwa na CCM na serikali yake, kwani kati ya km 14,036 ambazo ndio eneo lote la wilaya, km  8,281 au 59% zimechukuliwa na eneo la hifadhi; km2 870 au 6 asilimia limechukuliwa na hifadhi ya Misitu ya Nyanda za Juu Kaskazini.

Maeneo ya wanyamapori na malisho ya mifugo ni km2 3,916 au 30 asilimia; wakati maeneo ya kilimo ni km2 435 au asilimia 3 ya eneo lote la wilaya ya Ngorongoro.

Matokeo ya sera hizi za kuwanyang’anya wananchi wa Ngorongoro ardhi kwa ajili ya mifugo yao na kupiga marufuku kilimo yamekuwa tatizo sugu la njaa isiyoisha katika tarafa ya Ngorongoro.

Taarifa hiyo inafafanua kwamba wananchi wa Ngorongoro wana njaa ya muda mrefu ambayo haijapatiwa ufumbuzi. Hawaruhusiwi kulima ndani ya hifadhi na hivyo hutegemea mgawo wa chakula toka mamlaka ya hifadhi.

Ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kuwa serikali ya CCM itashughulikia suala la kilimo cha kujikimu ambacho kingewasaidia Wamaasai kujipatia chakula, haijatekelezwa licha ya ukweli kwamba mamlaka ya Hifadhi imeshindwa kuwapatia chakula.

Loliondo, Waraabu na CCM

Mheshimiwa Spika,
Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii.

Kufuatia kuondolewa kwa Wamaasai huko Serengeti mwaka 1959, baadhi yao walihamishiwa katika tarafa za Loliondo na Sale, huku wengine wakihamishiwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Licha ya ahadi za Serikali ya kikoloni kwamba haki za ardhi za Wamaasai zitaendelea kulindwa katika maeneo hayo, serikali imeanza kwa kasi kuhujumu haki hizo.

Kwa mfano, mwaka 2011 serikali ya CCM “ilivitangazia vijiji vyote kurudisha hati miliki za ardhi…” Amri hii ilikuwa ni sehemu ya mwisho ya maandalizi ya kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale ardhi zao.

Tarehe 26 Machi 2013, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliitembelea Ngorongoro na kutangazia wananchi na wakazi wa wilaya ya Loliondo kwamba ameagizwa na Rais wa Jamhuri, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kugawa eneo hilo na kisha kuligawa katika sehemu mbili.

Kwanza, kilomita2 2,500 zimeachwa kwa ajili ya matumizi ya kilimo, ufugaji, makazi na kadhalika na pili, kilomita2 zilizosalia zimechukuliwa na serikali.

0
No votes yet