CCM na Tanzania tuitakayo


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

SIFA moja kubwa kwa serikali hii inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuacha aibu ipite bila kutolea majibu.

Nchi imeshuhudia hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete akitofautiana na kumkana Waziri mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda. Haya yamefanyika hadharani.

Ongezeko la posho za wabunge ndilo lilisababisha ofisi hizo tatu kujiumauma na kutofautiana wazi. Spika na Waziri mkuu walidai posho hizo ni halali, lakini ikulu baada ya kusoma kasi ya upepo wa upinzani ikasema ni haramu.

Katika umri wa miaka 50 nchi haijawahi kushuhudia aibu kama hii. Mbaya zaidi aibu hii imeachwa ipite hivi hivi au kimya kimya kana kwamba lilikuwa jambo la kawaida.

Serikali inaweza kuinyamazia aibu hii kama ilivyofanya kwa aibu nyingine kadhaa viongozi walipotuhumiwa kwa ufisadi, lakini mgongano huu unawaacha wananchi wasiwe na uchaguzi mwingine ila kujiunga na harakati za kudai uwajibikaji.

Uongozi huu unawarejesha wananchi enzi za zamani ambazo wapambanaji wa aina hii waliitwa wapigania uhuru. Nchi yetu chini ya uongozi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa kinara duniani wa kusaidia wapigania uhuru popote. Tuliwasaidia wapigania uhuru bila kujali rangi zao, jinsia zao dini zao wala utaifa wao!

Siku huja na hupita huku mambo nayo yamebadilika. Zama hizi za waliopo katika mapambano si wapigania uhuru tena bali wanaharakati.

Kazi iliyokuwa ikifanywa na wapigania uhuru na ile inayofanywa na wanaharakati sasa ni moja ileile. Wakati wapigania uhuru walikuwa wanapambana na wageni waliojitwalia madaraka, wanaharakati wanapambana na watawala wazawa wenzao ambao ama wamejitwalia madaraka kwa hila ama wamewageuzia wananchi mgongo na kuwatawala kwa maslahi yao binafsi.

Haya ni mapambano magumu zaidi kuliko mapambano ya kudai uhuru yaliyofanywa na waliokuwa wapigania uhuru!

Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Vita hivi ni vigumu zaidi, maana wakoloni sasa ni hawahawa wenzetu. Wakoloni wenyewe walikuwa na kwao. Maji ya shingo yalipowafika walikimbilia kwao. Hawa kwao ni hapahapa. Kwa hiyo watapambana kwa nguvu zote, na ikibidi kufa watafia hapahapa!”

CCM wamejichanganya na sasa wamechanganyikiwa. Maamuzi yao hayalengi tena taifa wala wananchi. Wanalengana wao kwa wao katika vikundi vyao.

Hatuwezi kuupuuza mkanganyiko uliomo ndani ya CCM kwa sababu hawa ndio waliopaswa kuonyesha mustakbali wa nchi yetu. Hakuna kinachofanyika na CCM na serikali yake kinachoonyesha kuwa nchi inaongozwa!

Masuala yanayohusu nchi yameonekana kuwekwa pembeni. Kinachoonekana kutawala ndani ya CCM ni urais 2015. Nani awe rais na nani asiwe rais. Ukitaka kujua kuwa wamejichanganya na wamechanganyikiwa, hawaoni tena wala hawakumbuki kuwa kuna watu ambao ni tishio zaidi kwa urais wa 2015 ambao hawako CCM. Hawawashughulikii kabisa. Wanashughulikiana wao kwa wao.

Hali hii haipaswi kupuuzwa na Wananchi kwa sababu kadri tunavyoisogelea 2015 ndivyo misuguano ndani ya CCM inavyozidi. Makombora yanatupwa kutoka kundi hili kwenda kundi lingine na mbinu chafu zinasukwa kundi moja kwenda kundi lingine.

Tukiwaacha wapasuke hawatapasuka kwa amani kwa sababu sasa wanaundiana visasi. Watatuchafulia nchi. Lazima katika umoja wetu tutafute suluhisho. Mwaka wa tano sasa nchi imesimama. Dhambi iliyotendwa na wanamtandao 2005 inawatafuna, wananchi wanaambulia maumivu..

Mwaka 2005 CCM ya Mwenyekiti Benjamin William Mkapa na Katibu Mkuu wake Phillip Mangula ilipinduliwa na kundi lililojiita wanamtandao. Mtandao hakikuwa chama cha siasa, na kwa kuwa hakikuwa kikundi kilichosajiliwa rasmi, mtu akisema lilikuwa genge la kihuni nitaipata wapi hoja ya kupingana naye?

Kilichofanyika katika nchi hii mwaka 2005 ni sawasawa na kilichofanyika katika Bustani ya Edeni Adam na Eva walipokula tunda la mti wa katikati.

Mtandao wakati ule alikuwa nyoka na kwa sababu hiyo Watanzania wanateswa na dhambi ya mtandao kama ambavyo wanadini wengine wanavyoamini kuwa kila mtu huzaliwa na dhambi ya asili kutokana na kosa la  Adamu na Eva.

Mipango ya Mungu haijulikani. Richmond ikatua nchini na tangu sakata lile lifumuke wenye Richmond hawajawahi kupata amani katika mioyo yao hata siku moja. Kuwasukumia wengine mzigo ndiyo kumezua balaa kubwa mpaka leo. Waliouona udhaifu wa mwenye Richmond wakamtumia kwa maslahi yao! Nao sasa wamekwama. Walidhani wanamtumia wamejikuta wametumika wao!

Richmond ilizua vita hewa dhidi ya ufisadi lakini baada ya kujulikana kuwa vita hiyo haikuwa na maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja, vita hiyo ‘ilishindwa’. Leo wapambanaji wanatembea vichwa chini.

Richmond hiyohiyo ikazua gamba ambalo Mzee wa Upako alisema aliyeileta dhana hiyo hakufikiri vizuri, nayo ikaonekana haina maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja. Pia nayo imeshindwa. Wahubiri wake ndimi zao zimegandana na mataya yao! Ni Richmond hiyohiyo ambayo sasa yameletwa marekebisho ya Katiba ya CCM.

Wamewatoa rasmi Mwenyekiti mstaafu Mkapa na Katibu mkuu wake Mangula na wazee wenzao kwenye Halmashauri Kuu (NEC). Hawa si wenzao. Hawa ni CCM asilia waliopinduliwa 2005.

Mjumbe aliyekuwa ndani ya kikao alinukuliwa akisema, “Mzee Kingunge Ngombare Mwiru ametueleza wazi kabisa kwamba marekebisho hayo hayana maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja. Aliuliza sekretarieti imepata wapi kwamba Halmashauri Kuu ina uwezo wa kufanya marekebisho haya?”

Kama mawazo ya Kingunge ni yenye maana watatokea wanachama japo wachache watakaoyaeleza mawazo hayo vizuri na hivyo kuleta mabadiliko. Nukuu mojawapo ya Baba wa Taifa inasema, “Maana wale wachache wenye mawazo tofauti lazima wafahamu kuwa kama wanayo mawazo yenye maana na kama wakiyaeleza mawazo hayo vizuri, wanaweza kubadili mawazo ya wengine walio wengi”

Basi kama marekebisho haya ya katiba ya CCM nayo hayana maudhui zaidi ya kumlenga mtu mmoja pia hayatashinda. Hayatashinda kwa sababu historia ya dunia hii inaonyesha kuwa chuki,  fitina au uovu wowote kwa wengine havijawahi kushinda popote toka kuumbwa kwa ulimwengu.

0713334239
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: