CCM Ulanga waanza kunyosheana vidole


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro wameanza kunyosheana vidole. Ni kuhusu nafasi za ubunge katika majimbo mawili ya wilaya hiyo.

Katika wilaya hiyo kuna majimbo mawili-Ulanga Magharibi linaloongozwa na Dk. Juma Ngasongwa ambaye alipata kuwa waziri wakati wa awamu ya pili na tatu ya uongozi; na Ulanga Mashariki linalowakilishwa na Celina Ombeshi Kombani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI).

Katika jimbo la Ulanga Magharibi makada wawili wa CCM wanapimana “vifua” kabla ya kuvaana na Dk. Ngasongwa.

Hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Alfred Luanda na kada mwingine aliyetangaza nia ya kugombea ubunge mwaka 2005 katika jimbo la Ulanga Magharibi, Yassin Njayaga. Ameishi Marekani kwa miaka 16 akifanya biashara.

Hao wawili wamekuwa wakisutana kuhusu nani hasa ametoa msaada wa vifaa katika Kituo cha Afya cha Lupiro kilichopo wilayani humo.

Wakati Luanda akisema misaada ya kituo hicho imetokana na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), habari zilizozagaa zinasema misaada hiyo inatokana na hisani ya Nyayaga.

Kwa vyovyote vile, kila mwamba ngoma huvutia kwake. Katika mazingira haya ya kuelekea uchaguzi inawezekana misaada hiyo imetoka sehemu zote mbili. Maofisa wa kituo hicho wanajua siri hiyo.

Luanda mwenyewe anasema watu wanaodaiwa kuwa wapambe wa Njayaga ndio wanatangaza kuwa vifaa hivyo vimetolewa na mgombea wao kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Lupiro.

“Vifaa vilivyotolewa ni vitanda 20, magodoro 20, darubini na baadhi ya dawa. Hivi vimetolewa na halmashauri kupitia Mfuko wa Bima ya Afya na siyo mtu mwingine,” anasema Luanda.

Mkurugenzi huyo anaeleza hayo baada ya kuwapo utata miongoni mwa wananchi wengi juu ya nani hasa kanunua vifaa vya Lupiro.

Utata huo unatokana na baadhi ya wananchi, wakiwamo wapambe wa Njayaga kutangaza kuwa ndiye aliyenunua vifaa hivyo kwa ajili ya wananchi wa Lupiro.

Luanda anasema wilayani kwake kumekuwa na watu wanaowarubuni wananchi ili waonekane wema na wanafaa kugombea ubunge, lakini halmashauri yake imesimama kidete na itahakikisha inapeleka maofisa wake kuwapa ukweli wananchi wa Lupiro.

Nayo wilaya ya Ulanga imevamiwa na wanasiasa ambao wanadai kuwa wametumwa na mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, wakagombee ubunge, jambo ambalo limezua mtafaruku kwenye chama hicho.

“Watu wanatishwa na kuna wengine wanadiriki hata kumtaja Rais Kikwete kuwa kawatuma kugombea ubunge, kitu ambacho sio kweli. Wananchi wa Ulanga wanatakiwa kuwa makini na watu wa aina hiyo,” anasema Luanda.

Kutokana na hali hiyo, katibu wa CCM Wilaya ya Ulanga, Letisia Mtimba, ametoa onyo kwa wanachama wao wanaotaka kugombea uongozi katika jimbo hilo kuacha tabia ya kusingizia viongozi wakubwa kwa manufaa yao binafsi.

Kwamba kitendo cha wagombea hao kutangaza kuwa wametumwa na rais ni kumdhalilisha kiongozi huyo na kumfanya hajui majukumu yake.

“Kweli inemiuma sana kusikia kuwa kuna watu wanafanya hivyo lakini naahidi kuwa tutawashughulikia kama tukisikia mtu anasimama jukwaani kutangaza ametumwa na Rais Kikwete kugombea ubunge au udiwani,” anasema Mtimba.

Wanaotajwa kugombea ubunge Ulanga Mashariki ni mbunge wa sasa Celina Kombani na mpinzani wake mkubwa wa mwaka 2005, Aziz Chimetule, mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, na Michael Maganga ambaye pia anafanya biashara Dar es Salaam.

Kwa hiyo wanaotarajiwa kumenyana Ulanga Magharibi ni Dk. Ngasongwa, Yassin Njayaga, Joseph Ngonyani na Juma Mponda.

Kabla ya kutangaza nia ya kugombea Ulanga Magharibi, Njayaga alikuwa akiishi nchini Marekani ambako alikuwa akifanya biashara.

Ngonyani ni mhandisi katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji; na Mponda anafanya kazi kituo cha mradi wa kudhibiti malaria cha Ifakara.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: