CCM na urais wa makanisani


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

BAADA ya vikao vya Chama cha Mapinduzi vilivyomalizika mjini Dodoma wiki mbili zilizopita, taarifa ilitolewa na wasemaji wa chama hicho kuwa mojawapo ya matatizo yanayokikabili chama hicho ni minyukano inayotokana na mbio za kuusaka urais wa mwaka 2015.

Mapema mwaka huu, baadhi ya wanaohisiwa kuwa tayari wameanza harakati za kuusaka urais, waliitwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara, Pius Msekwa na kuonywa kuwa wasiendelee na harakati hizo.

Aidha, taarifa ya kamati ya wazee watatu walioteuliwa na chama kutafuta suluhu ya minyukano ndani ya chama – rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi, Abdurahman Kinana na Msekwa pia ilibainisha harakati za kusaka urais wa 2015 zilikuwa zinakitesa chama hicho.

Moja na ya maeneo maarufu ambayo wale wanaousaka urais wanapendelea ni kwenye nyumba za ibada. Nyumba hizi hujumuisha makanisa, misikiti na masinagogi. Maeneo mengine, ni kwenye mahafali ya taasisi mbalimbali za elimu. Tamaa ikiwa mbele, usishangae kumwona mwanasiasa maarufu akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya kuhitimisha watoto wa darasa la awali (vidudu)!

Mpaka ninapoandika makala hii, tumemsikia na kumwona Edward Lowassa akiwa mgeni rasmi katika matukio ya makanisa kadhaa. Tulimsikia akifanya harambee katika kanisa Anglikana jijini Dar es Salaam na Askofu Mkuu Valentino Mokiwa akarusha kijembe chenye utani, lakini kilichotoboa siri aliposema Lowassa atakapokuwa ikulu asimsahau!

Baadaye tulimsikia Lowassa akiwa Kanisa Katoliki jijini Mwanza kwenye harambee ya kuchagia ujenzi wa kanisa la Nyakato. Hali kadhalika, kasisi wa kanisa hilo akaashiria kuwa waumini kwa kanisa lake mmoja mmoja ni sawa na matofari yanayoweza kumjenga Lowassa tofauti na kumbomoa!

Baadaye, tulimsikia Lowassa akiwa mkoani Singida katika Kanisa la Kilutheri (KKKT), ambapo alishuhudia na kuwashukuru sana viongozi wa dini kwa kumwombea wakati wa migogoro iliyomkabili na akatamka kuwa sasa mambo yameisha. Askofu wa kanisa hilo akabainisha kuwa matatizo ni sawa na mawingu yasiyoweza kuzuia jua lisiwake!

Yako matukio mengine yenye harambee na yasiyo na harambee ambayo kwa mwanasiasa yeyote mwenye nia ya kugombea urais, hawezi kupewa nafasi akatoka bila kusema neno lenye ama kumjenga au kubomoa mpinzani wake.

Mbali na Lowassa kwa muda, yuko Benard Membe mmoja wa wanaotajwa kutaka kumrithi rais Kikwete kwa udi na uvumba. Naye hayuko nyuma katika kuyatumia makanisa.

Jimboni kwake siyo tu ametoa michango mikubwa kwa makanisa mbalimbali, bali pia amejenga makanisa na kuyakamilisha na tayari anawasiliana na uongozi wa makanisa kadhaa na kuyapatia viongozi wakuu kuyazindua.

Hatuna mashaka na uumini safi wa Membe kwenye dini yake ya kikirsto, lakini harakati zake hizi za kujenga kanisa kila pembe ya jimbo lake, zimeanza kunitisha.

Mwingine ambaye anatumia makisa, tena kwa nguvu, ni yule anayejiita mpambanaji wa ufisadi. Samwel Sitta. Siku za karibuni amekuwa katika hafla mbalimbali za makanisa akinadi sera yake ya kuchukia ufisadi.

Wakati mwingine Sitta huonekana kuwa na chuki binafsi na mafisadi badala ya kuchukia ufisadi, lakini kwa kuwa hayo huyasemea makanisani, basi huonekana kuwa anapambana na ufisadi.

Kwa bahati mbaya sijawahi kumsikia Sitta akinadi sera yoyote ya kiuchumi zaidi ya kupambana na ufisadi. Wiki iliyopita, alikuwa mjini Arusha kwa mwaliko wa Kanisa Katoliki na huko pia alijibainisha kuwa mtu muhimu wa kutatua matatizo ya taifa letu.

Mpaka sasa, ametembelea makanisa ya Roman Catholic (RC), Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moraviani na Pentekoste.

Naye Fredric Sumaye anatajwa kama msaka urais kwa mwaka 2015. Huyu ni mtu aliye kanisani daima, iwe wakati wa kuusaka urais au hata wakati vuguvugu la kuusaka halipo.

Katika wote anaonekana mwangalifu sana wa harakati zake na itakuwa vigumu kumhukumu katika mbinu za kutumia makanisa.

Kingine ambacho kinamtofautisha Sumaye na wenzake katika kundi hili, ni ukweli kuwa inasemekana yeye huwaambia viongozi wa makanisa wamualike aje kwao.

Uchunguzi wengi katika maeneo ambamo yeye amepita umebainisha ukweli huu na hata wakati mwingine kukuta malalamiko ya watu waliomualika lakini akakosa muda na kuwashauri watafute mwingine.

Hawa wengine wanatafuta na kushawishi waalikwe hata wakati mwingine kupitia kwa viongozi walei wa makanisa husika.

Kuna madai kuwa hata wanapopelekewa mialiko na kukuta nafasi imejaa, wako tayari kuwabembeleza waandaaji wa harambee wahairishe na kusogeza mbele ili kuhakikisha nafasi inapatikana mbele ya safari.

Mpaka hapa kuna jambo moja muhimu: Waliotajwa si kwamba ni wao peke yao na pia siyo walioanzisha utamaduni huu wa kuusaka urais kwa kutumia nyumba za ibada.

Hata rais aliyeko madarakani alifikia hatua ya kujigeuza mhubiri wa injili ili kuwakoga nyoyo wakiristo katika harakati zake za kuusaka urais kwa zaidi ya miaka 10.

Ninachojaribu kuonyesha ni unafiki wa wanasiasa wetu wanaposhika madaraka na kudiriki kusimama hadharani kukemea vitendo vya wanasiasa kutumia makanisa wakati wao pia wamepita huko huko.

Binafsi nilisikitika nilipomsikia Rais Kikwete akilihutubia Bunge baada ya uchaguzi wa mwaka jana na kudai uchaguzi ulikumbwa na udini. Baada ya kuwa yeye ametumia makanisa na misikiti kujipatia kura ambazo nazo hazikutosha aliona ni bora aamue afanye usanii wa kukemea udini.

Sasa hivi dalili za udini katika uchaguzi wa mwaka 2015 zimeanza mapema na yeye yuko kimya wakati wanasiasa wanaotumia makanisa wanatoka chama chake. Kwa bahati mbaya nyingine niliowataja wote ni wakiristo.

Je, waislamu wanaoutaka urais wakiamua kutumia misikiti itakuwaje? Mbona tumekuwa tunasikia kejeli nyingi dhidi ya Dk. Wilbroad Slaa na CHADEMA kuwa ni chama cha wakiristo wakati sasa wanaoonekana kuyavamia makanisa kufanya kampeini ni wale wa kutoka CCM?

Kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama cha waislam, mbona wanasiasa wanaenda kutafuta kura makanisani badala ya misikitini? Dk. Slaa amesingiziwa sana kwa ama kutumia makanisa au kutumiwa na makanisa wakati ambapo ni nadra sana kumwona hata akienda kanisani?

Je, kama angeenda na kuongoza harambee ingekuwaje? Hii kofia ya udini ambayo CCM imekuwa kinara wa kuitumia itakuja kuigeuka CCM na kutuletea rais anayetumwa ama na makanisa au rais anayechukiwa na misikiti.

0
Your rating: None Average: 3.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: