CCM na vita vya shingo upande


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kilipotangaza kuwa kitajivua gamba la ufisadi, tulitabiri kuwa hilo haliwezekani kwa sababu kadhaa. Tuliona ni mizaha iliyozoeleka katika kilele cha sherehe na kwamba ilikuwa sehemu ya shamrashamra.

Kwa sasa, ufisadi umezama mno katika CCM kiasi kwamba kuuondoa ni sawa na kuua chama. Ni CCM yetu iliyolea na kustawisha ufisadi ndani ya nchi; kwa hiyo, kuubomoa ufisadi, kwa namna fulani, ni sawa na kubomoa msingi iliposimama. 

Mathalani, ukidhamiria kuondoa rushwa katika uchaguzi au kuharamisha rushwa, waweza kujikuta huna madiwani na wabunge; na hata rais wa kushikilia chama hiki.

Lakini pia ukiharamisha mhimili huu – Bunge – kwa msingi kuwa ulichaguliwa kifisadi, waweza kujikuta ukiharamisha pia mihimili mingine – serikali na mahakama. Hakutakuwa na dola.

Waweza kujikuta unahoji teuzi zote za majaji wa mahakama, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakuu wa vyombo vya dola na wateule wote wa rais. Kuthubutu kuondoa ufisadi na rushwa katika CCM laweza kuwa “janga la kitaifa.”

Kwa uchache, tulipofikiria haya, tuliona Rais Jakaya Kikwete anafanya utani aliposema CCM, kupitia vikao vyake vya maamuzi, ilikuwa inajiandaa kujivua gamba la ufisadi na viongozi walio mzigo kwa chama.

Tuliona ni utani kwa sababu mbili kuu: Kwanza, tulidhani hawezi kulikashifu titi linalomnyonyesha. Unahitajika ujasiri usiomithilika kulipiga teke titi linalokunyonyesha.

Atake asitake, Kikwete kama wengine, ni tunda la mfumo wa kifisadi. Atakuwa anajua na hata kukiri kuwa hawezi kukana rafu za kifisadi katika kupaa kwake.

Kikwete atakuwa anatambua pia kuwa kuna mafisadi wawezao kusaidia   kukupandisha ngazi na hata kukunyonga. Mara nyingi hali za wengi kiuchumi, naye anajua, si tunda la mshahara anaopata mtu, bali mchanganyiko wa dhuluma ya kifisadi na hisani za mafisadi.

Hili ndilo linaleta ugumu kwa Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kupambana na ufisadi.

Pili, viongozi wa vyombo vya dola, kwa kiapo na matarajio ya wananchi, hawatarajiwi kuwa watamtegemea rais katika utendaji kazi wao. Yaani kama ni waadilifu hawahitaji maoni ya rais kujua kama mtu fulani ni fisadi au si fisadi na wafanye nini naye.

Tumeshuhudia mkurugenzi mkuu wa Takukuru, mkurugenzi wa mashitaka (DPP), mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), mkuu wa jeshi la polisi nchini (IJP) na wengineo, kuwa katika vita dhidi ya ufisadi, wao ni matarishi wasio na utashi katika kutenda kazi zao.

Wanahitaji ruhusa kuwagusa mafisadi. Kwa hiyo rais akijifanya kukaa kimya kwa kisingizio cha kutowaingilia katika kazi zao, basi nao hukaa kimya kwa kisingizio kuwa hawapaswi kuingiliwa na yeyote. Lakini kimya hicho cha rais na wateule wake kitakuwa na maana ya kuwalinda mafisadi.

Vikao vya CCM vilipotangaza kuwa chama hicho kimevunja Kamati Kuu, kimesambaratisha sekretariati yake na kisha kuwapa siku 90 watuhumiwa wa ufisadi; baadhi yetu tuliona ni mkwara wa kawaida kisiasa ili kujaribu kuchelewesha wana CCM waaminifu kukata tamaa.

Kwani maamuzi hayo yalijaa kasoro nyingi na kukosa mwelekeo wa utekelezaji. Wote tumeshuhudia mathalani, sekretariati nzima ikijifungia ndani siku kadhaa kuandika barua tatu kwa watuhumiwa. Watu wazima na akili zao wanashindwa au wanasitasita kuandika barua na kuishia kulumbana katika vyombo vya habari.

Mara barua ziko mezani kwa makamu mwenyekiti Bara, Pius Msekwa. Mara zipo kwa katibu mkuu Wilson Mukama anayesita kuzisaini na kudai apelekewe mwenyekiti wa chama.

Taarifa zinasema mara mbili ushauri ulitafutwa kutoka kwa viongozi wastaafu kuhusu suala hili. Baadhi ya wastaafu wamenukuliwa wakikataa kuchonganishwa na watuhumiwa.

Wakati hayo yanatokea, mwenyekiti wa chama alikuwa katika shinikizo kali la kukutana na watuhumiwa wa ufisadi ambao ni maswahiba wake wa siku nyingi.

Katika hali hii, mwenyekiti akajikuta ana sekretariati mbili – moja ikiwa ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM; na sekretariati nyingine ikiwa ni ile ya watuhumiwa ambao nao walifaulu kumyumbisha mwenyekiti anayefurahia sana kuyumba.

Kama kawaida yake alifanikiwa kuwatia moyo wote ili wasiudhike. Aliwaambia watu kuwa sekretariati ya chama, ina ridhaa yake ya kusema chochote bila kumung’unya maneno. Lakini wakati huohuo inadaiwa aliwaambia watuhumiwa wa ufisadi kuwa wasiwe na wasiwasi maana Watanzania ni mafundi wa kupiga kelele.

Huu ni mchezo wa hatari sana kwa wote watatu – sekretariati zote mbili na mwenyekiti mwenyewe. Ni hatari kwa sekretariati ya chama kwa sababu itajidanganya sana ikidhani mwenyekiti wao anaweza kuwasimamia wao watakapobanwa na hoja za wanachama juu ya upotoshaji walioufanya. 

Sekretariati licha ya kuwa na maamuzi ya vikao halali vya chama, wajumbe wake wanatakiwa “kuchanganya na yao” katika utekelezaji wa maagizo ya vikao na hasa kama maamuzi hayo yanaweza kugusa maslahi binafsi ya mwenyekiti au kundi lake.

Aidha, ni hatari kwa sekretariati ya watuhumiwa kumwamini mwenyekiti pale wanapowasiliana naye; iwe ana kwa ana au kwa ujumbe wa simu. Mwenyekiti huyu anaamini sana katika falsafa ya “mafisadi wanajimaliza wenyewe” na kwa hiyo tuwaache wajimalize bila kuwapa msaada wowote wa kujimaliza.

Ni mwenyekiti huyuhuyu anayeweza kuchelewesha kikao tangu asubuhi mpaka jioni akiruhusu watu waongee bila mwelekeo wa mapatano ili wapumue.

Kwa hiyo, anaweza kuwaruhusu watuhumiwa wamwone ili kupumua hisia zao. Kimsingi watuhumiwa mbele ya mwenyekiti ni kama wafungwa wa kifungo cha nje; anaweza kuwageuka kama alivyowageuka mara kadhaa tangu alipoingia madarakani.

Salama ya watuhumiwa kwa sasa ni kujipanga kupambana na mwenyekiti asiye na msimamo au anayepanga msimamo kutegemea upande gani alilalia.

Kuna muono mwingine kuwa, kwa CCM kupambana na ufisadi kikweli, ni sawa na kufagilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hili ni eneo jingine la shingo upande.

Nina maana kuwa licha ya kuwa agenda hii ilianzishwa na CHADEMA na kupuuzwa na CCM kwa muda mrefu, lakini kupambana na ufisadi ndani ya CCM kutaidhoofisha CCM na kuijenga CHADEMA mbele ya wananchi.

Kimsingi, ili CCM iweze kuaminika kuwa inapambana na ufisadi, itabidi ipitie hatua ya kudhoofishwa na vita hivi; maana watendaji wake wengi itabidi wafukuzwe; na hili litaleta tetemeko.

Ikifanya hivyo bila kuyumba, ndipo itaweza kujipanga na kuanza kuaminika tena. Kwa maoni yangu, chini ya uongozi wa mwenyekiti wetu, sioni hilo likitokea maana lina gharama kubwa hata kwa mwenyekiti mwenyewe.

Watuhumiwa wa ufisadi wamemwonya mwenyekiti na kukionya chama kuwa kung’ang’ania vita hivi kutaisambaratisha CCM. Sasa mwenyekiti amejifikisha njiapanda: Kumeza anataka lakini ni moto; na kutema anataka lakini ni tamu.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: