CCM waanza kugombania mbao


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version

HATA kabla mashua yao haijapasuka kabisa, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaonekana kuanza kugombania mbao za mashua yao hiyo.

Kauli mchanganyiko zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa CCM hivi karibuni zinaacha mashaka makubwa kwa mustakabari wa chama hicho.

Wengi wa viongozi hao wamekatishwa tamaa na uongozi wa chama chao kilichokosa nguvu ya Mwenyekiti.

CCM walidakia mradi wa CHADEMA wa vita dhidi ya ufisadi, ukawashinda. Walipogundua kosa, wakaanzisha wa kwao wakaupachika jina kujivua gamba ambao sasa umewatumbukia nyongo.

Hakuna mtu timamu anayependa ufisadi, hivyo wana CCM walipodandia hoja wengi waliwaunga mkono, mimi nikiwa mmojawapo. Niliwaombea hata kwa Mwenyezi Mungu ili wafanikiwe, kwa matarajio kuwa walikuwa na moyo wa huruma kwa maskini wa nchi hii.

Kadri vita ilivyokuwa ikiendelea kupiganwa ndivyo sababu za vita zilivyofunguka. Kumbe hakukuwa na vita dhidi ya ufisadi bali vita ya kuupigania urais 2015! Mapambana yakawa “niwe mimi au mtu wangu” lakini “fulani asiwe!”

Baada ya wajanja kugundua hili vita vikakosa mwelekeo na tukashuhudia makamanda wakiacha vita halisi ya ufisadi. Lugha ikawa mbio za urais.

Mbio za urais zimewafanya wengi kujiingiza katika fikra za kijingajinga. Hivi, kuna ubaya gani mtu akianza kuusaka urais hata kama angali tumboni mwa mama yake? Watu wamepumbazwa waone kuusaka urais sasa ni dhambi huku wenyewe wakimtengeneza mtu wao hivyo waendelee kutawala.

Kashfa ya Richmond imetumika na mafisadi kufanya ufisadi mkubwa. Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea alipochunguza na akatoa ripoti kuwa serikali haikupoteza hata shilingi moja, tulimshangaa.

Kumbe wahuni walitumia ujinga wa wananchi wakadai kuwa Richmond walikuwa wanalipwa Sh. 152 milioni kila siku, kitu ambacho hakikuwa kweli. Mkataba wa Richmond ulisema wangelipwa Sh. 152 milioni kwa siku baada ya umeme kuanza kuzalishwa. Richmond haikuzaliza hata uniti moja.

Tukiendelea kuwasikiliza wahuni nchi yetu itazama! Ripoti ya Mdhibiti mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeripoti kuwa Wizara ya Fedha peke yake chini ya Mustafa Mkulo ilifuja Sh. 1.3 trilion kwa matumizi binafsi bila ridhaa ya Bunge. Fedha na raslimali zilizofisidiwa na mawaziri nane waliotuhumiwa ni karibu sawa na bajeti ya serikali ya mwaka mzima. Kuna ufisadi gani mkubwa kuliko huu uliokwisha fichuliwa mpaka sasa?

Nawauliza Watanzania wenzangu, ni nani kati ya wale makamanda au manabii au mitume kumi na mmoja waliojiita wapambanaji wa ufisadi aliyesaini karatasi ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kuilazimisha serikali kuwachukulia hatua mawaziri waliohusika na ufisadi huu? Wote walikuwa radhi mawaziri wale waendelee na nyadhifa zao na ubadhilifu wao. Ni wenzao.

Waulizeni kina mawaziri Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Stella Manyanya, Ana Kilango, Christopher ole Sendeka na wenzao nani kati yao alisaini fomu ile? Je, huu kwao siyo ufisadi?

Tukitaka kwenda mbele tuache unafiki. Tuelezane ukweli hata kama watasema mwandishi au gazeti limenunuliwa na mafisadi kwa maana kama kununuliwa au hapana Mwenyezi Mungu anajua. Wanafiki ni hatari kuliko nyoka.

Hata hivyo, nakubaliana na Sitta kuwa taifa linakabiliwa na viongozi wenye sura mbili. Sitta aliyasema haya wakati akitoa mada katika maadhimisho ya siku ya sheria kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, alipozungumza na jumuiya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, mjini Iringa (IUCo).

Lakini natofautiana naye kwa aina ya sura hizo mbili. Sura ya kwanza ni viongozi mafisadi  halisi ambao wako radhi kujiuza kwa vyeo vya duniani hata kama wanajua kuwa kwa kufanya hivyo kutawaumiza wananchi na hasa maskini.

Hawa wako radhi kutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi maskini kujenga Jumba la Spika kwao hata kama Spika anatoka Njombe. Wamechukua mamia ya mamilioni ya fedha za wananchi wakiwaahidi kuwa wanaenda duniani kuwatafutia ukweli kuhusu Richmond.

Nao wakishakuizunguka dunia na kuupata ukweli wote, wakawasilisha nusu, nusu wakawaficha wananchi walewale waliowachukulia fedha zao! Ufisadi maana yake ni nini? Wana udhu gani hawa wa kusimama mbele ya waja wa Mwenyezi Mungu na kuwaonyesha wengine kuwa ndio mafisadi?

Sura ya pili ni viongozi ambao ni mafisadi lakini kwa ziada ni wanafiki pia. Amenukuliwa akisema, “Lakini wapo viongozi ambao wanatumia ubongo katika kufikiri jinsi ambavyo watatumia uwezo wao wote katika kuwatumikia wananchi, mimi ni miongoni mwa hawa.” Mtu safi, mwadilifu hajisemi mwenyewe! Tapeli wa siasa ndio zake.

Tuna mifano hai ya viongozi aina hii hapa kwetu. Kwa kuinyonga kihuni hoja ya Richmond bungeni, wakawa wamewasukumiza wananchi kwa Dowans. Dowans walipotaka kujilipa, viongozi haohao kwa unafiki wao wakawataka wananchi waandamane kupinga malipo.

Kama walipaji ndio walipwaji, Dowans watalipwa tu. Siku ya kulipa Watanzania watalipa aghali zaidi kama riba kwa kuwasikiliza wanafiki wachache. Hivi ndivyo vikundi vya viongozi waliomo ndani ya CCM ambavyo sasa vinaipasua vipandevipande!

Ugomvi wa urais unaisambaratisha CCM lakini wanaopata mateso ni wananchi. Mfumko wa bei hasa wa vyakula unawatesa wananchi lakini wao wamekazania upuuzi wa magamba ambayo hayamsaidii lolote mwananchi.

Sasa CCM wanataka kutoana roho. Katibu mkuu mstaafu Yussuf Makamba amemng’ang’ania koo Katibu wa Uenezi na Itikadi Nape Nnauye akidai kuwa ndiye anayekiharibu chama kwa kukiendesha kama mali yake.

Tangu ujinga wa gamba ulipoingia, mahubiri ni chuki tupu. Mwingine akasema Katibu Mkuu Wilson Mukama ni mzigo mzito kwa chama na kwa uzito wake chama kinazama.

Watu wanaulizana haya yote yanatokea CCM haina Mwenyekiti akakaripia na kuelekeza njia iliyo njema? Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete akajibu, “Anayetaka kuhama CCM ruksa!” Ah! Hii kweli bahati mbaya! Nahodha anasema mashua yake kupasuka na kuzama sasa ruksa?  Je, si kweli kwamba tatizo la CCM ni uongozi ?

0713 334239
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: