CCM wajipanga kumzuia Dk. Slaa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Waandaa mamluki ‘kumdhamini’
Waomba msaada wa vyama vidogo
Dk. Willibrod Slaa

MKAKATI umesukwa na viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuzima safari ya Dk. Willibrod Slaa kwenda ikulu, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema, kwa kushirikiana na vyama vidogo vya upinzani, CCM imesuka njama za kumkwamisha Dk. Slaa katika hatua ya kurejesha fomu za kuwania urais.

“Kama hatukufanikiwa kumkosesha wadhamini halali, basi tutakwenda mahakamani…lakini hapiti,” kimeeleza chanzo cha gazeti hili kikimkariri mmoja wa viongozi waliopewa jukumu la kumzamisha Dk. Slaa.

MwanaHALISI lina taarifa kamili juu ya njama hizo zinazodaiwa kuhusisha baadhi ya viongozi wa CCM, serikali na vyama vya upinzani.

Dk. Slaa aliibuka wiki tatu zilizopita, pale alipotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwa mgombea urais kwa tiketi hiyo.

Kuingia kwa Dk. Slaa ulingoni kulibadili upepo wa kisiasa nchini, kuleta kiwewe CCM na hata kufanya viongozi wastaafu wa chama hicho kutamka hadharani kuwa “Slaa ni makini…hashikiki.”

Hatua ya kwanza ya mkakati wa kumwangamiza Dk. Slaa kisiasa inahusisha kumchomekea “wadhamini feki” katika fomu zake za kutaka kuwania urais.

Hatua hii inahusisha maandalizi ya genge la vijana ambao uraia wao una utata. Hawa watapelekwa mikoa mbalimbali nchini ili watie saini fomu zake za udhamini.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, wadhamini hao “feki” watafika kwa maofisa wa CHADEMA wanaoendesha zoezi la kuandikisha wadhamini wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura, kwa lengo la kutimiza jukumu walilopewa.

“Vijana hao wakimaliza kujiandikisha, wataripoti kwa maofisa wa chama chao ambao watarekodi kadi zao. Kwa kutumia kadi hizo za wasio Watanzania, Dk. Slaa atawekewa pinganizi,” ameeleza mtoa habari.

“Nakuhakikishia, CHADEMA wasipokuwa makini, Dk. Slaa hawezi kuwa mgombea urais. Tayari vijana wametumwa mikoani kutimiza azma ya kumkwamisha,” ameeleza kiongozi mmoja wa CCM ambaye hakutaka kutajwa gazetini.

Sheria ya uchaguzi inamtaka kila mgombea urais, awe na wadhamini 200 kutoka mikoa 10 nchini, ikiwamo miwili ya Tanzania Visiwani.

Kwa taarifa za juzi Jumatatu, jukumu la kumwekea pingamizi Dk. Slaa litakabidhiwa kwa “wagombea urais wa vyama vya upinzani.” Haijafahamika ni nani hasa watapewa jukumu hilo.

Lakini Cristopher Mtikila, mwenyekiti wa Democratic Party (DP) aliliambia gazeti hili Jumatatu kuwa naye anatarajia kuweka pinganizi kwa Jakaya Kikwete wa CCM na Dk. Slaa wa CHADEMA.

Mtikila, kama Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa wanadai CHADEMA imefanya kampeni kabla ya muda wake. Lakini Mtikila anasema pia kuwa hata CCM walivunja sheria.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itapokea fomu za wagombea wote wa ubunge na urais, Alhamisi wiki hii (19/8/2010).

Muda wa kampeni wa siku 71 kuanzia tarehe 20 mwezi huu, utaisha 30 Oktoba na kesho yake, 31 Oktoba ndiyo itakuwa siku ya uchaguzi.

Kwa mtiririko huu, si Msekwa wala Mtikila mwenye hoja ya kutuhumu CHADEMA; wala hakuna misingi ya pingamizi, kwa Tume au mahakamani, ameeleza kiongozi mmoja wa CCM.

Kabla ya kusukwa njama hizo mpya, kulikuwa na mpango wa kutumia kisingizio cha “kuanza kampeni mapema” kumuwekea pingamizi mgombea huyo wa CHADEMA.

Kubadilishwa haraka kwa tuhuma, kutoka kufanya kampeni mapema hadi kutumia “wadhamini mamluki,” kumetokana na waandaaji njama kuambiwa kuwa walichofanya CHADEMA siyo kitendo cha kuvunja sheria ya uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili juzi Jumatatu, kwa njia ya simu, mmoja wa mawakili wanaounda jopo la kisheria ndani ya CHADEMA, Mabere Marando alisema, “Hakuna kosa lolote ambalo Dk. Slaa amefanya mpaka sasa.”

Alipoelezwa kwamba kuna mpango wa kumchomekea wadhamini feki katika fomu zake, alisema hilo ndiyo kwanza analisikia na hivyo akashauri mwandishi kuwasiliana na mwenyekiti wa timu ya kampeni, Profesa Mwesiga Baregu.

Naye Profesa Baregu alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema chama chake kinafahamu njama zote zinayofanywa na wapinzani wao wa kisiasa na kwamba wamejiandaa kukabiliana nazo.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba hakupatikana kuzungumzia suala hilo. Simu yake ya mkononi iliita mara kadhaa, lakini haikupokelewa.

Wakati hayo yakifumuka, imefahamika kuwa kampuni yenye uhusiano na mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani, imefunga televisheni katika mabasi kadhaa yaendayo mkoani kwa ajili ya kuendeshea kampeni za CCM za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ambazo MwanaHALISI imefanikiwa kuziona, kampuni hiyo inayoitwa PWT Company Limited, imefunga televisheni 500 katika mabasi 350 yatokayo Dar es Salaam kwenda mikoani.

Katika baadhi ya mabasi zimefungwa televisheni mbili – moja mbele na nyingine katikati. Katika mabasi mengine imefungwa televisheni moja.

Baada ya kufunga televisheni hizo, kampuni hiyo sasa inajipigia debe kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikitaka kitoe fedha za kuweka matangazo ya kampeni zake kwenye mabasi hayo.

“PWT imefunga runinga zaidi ya 500 katika mabasi yasiopungua 350 na yanayofanya safari kati ya Dar es salaam na mikoani.

Taarifa ya kampuni hiyo inasema televisheni hizo zitatoa fursa kwa wasafiri kusikia na kuona vizuri kile kitakachokuwa kikionyeshwa – matangazo ya kampeni.

Kwa mujibu wa maelezo ya PWT, vipindi vya kawaida vinavyorushwa na stesheni mbalimbali, vitakuwa vikikatizwa kila baada ya dakika 25 ili kupisha wagombea wa CCM kujitangaza.

PWT imesema kwa kila basi ambalo CCM itaamua mgombea wake wa urais atangazwe, chama kitahitaji kulipa kiasi cha Sh 3.5 milioni.

Kwa wagombea wa ubunge, PWT imeweka kiwango cha Sh. 7.5 milioni kwa watakaotaka kutangazwa kuanzia mwezi huu; lakini wale watakaotaka kutangazwa kuanzia mwezi ujao, watalazimika kulipa Sh. 10 milioni ili ‘warushwe’ hewani hadi Oktoba 28.

Iwapo CCM itakubaliana na mpango huu, abiria wote katika mabasi husika, watalazimika kuwasikiliza wagombea wa chama hicho wakijinadi wakati wako safarini.

Katika historia ya Tanzania, hii itakuwa mara ya kwanza kwa chama cha siasa kufanya kampeni za namna hii na hili linaweza kuzua mizozo ndani ya mabasi.

Kwa kawaida, televisheni zilizofungwa kwenye mabasi zimekuwa zikionyesha miziki na filamu kwa kipindi kirefu, na uwekaji huu wa kampeni za CCM safarini unaweza kuzua migongano.

Kama CCM itakubali dili hilo, chama kitahitaji kulipa kiasi cha Sh. 1.75 bilioni kwa ajili ya malipo ya kampeni hizo.

Kwa wabunge, PWT imeahidi kuweka matangazo hayo ya televisheni kwenye mabasi yanayokwenda kwenye majimbo ya wabunge hao.

Kwa mujibu wa PWT, mkoa wa Morogoro ndio utakaofikiwa na mabasi 26. Abiria zaidi ya 270,000 wanakadiriwa kusafiri kwa mwezi mmoja katika mabasi hayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: