CCM wakikuchukia wanakuvua uraia


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version

SIWEZI kudai kwamba mimi ni miongoni mwa watu wanaomfahamu vizuri Hussein Bashe. Kwa hiyo, sijui alizaliwa lini na wapi.

Lakini ninachojua, katika kipindi kifupi nilichofanya naye kazi katika Kampuni ya Mwananchi hakuwahi kuhisiwa wala kukumbwa na kashfa ya uraia.

Hata pale baadhi ya wafanyakazi katika kampuni hiyo raia wa Kenya walipobainika kutokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini, Bashe hakuhisiwa wala kuguswa. Bashe baadaye akahamia kampuni ya New Habari 2006 Ltd.

Ni katika kipindi hicho pia ambapo Bashe alikuwa anashiriki masuala ya siasa nchini kabla hajaukana uraia wa asili ya baba yake kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ambako alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM.

Katika uchaguzi mkuu uliopita wa viongozi wa UV-CCM, Bashe aliwania nafasi ya mwenyekiti. Alibaki yeye, Zainab Kawawa na Benno Malisa.

Tuliarifiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete ‘alipindua meza’ katika kikao cha Halmashauri Kuu; akapitishwa Hamad Masauni Yussuf kutoka Zanzibar aliyekuwa anawania umakamu ilhali Bashe na Benno wakashushwa katika nafasi ya makamu.

Katika uongozi wake wa takriban mwaka mmoja na nusu, Masauni hakuelewana na Ridhiwani Kikwete kwa sababu mbalimbali. Hamad akaishi kwa mashaka.

Wapinzani wake walipopata sababu, Mei mwaka huu ‘wenye chama’ wakapindua tena meza. Masauni akakabwa hadi akajiuzulu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni utata wa umri wake.

Alipokuwa anazungumza na baadhi ya vijana mkoani Iringa, wiki ileile ambayo Masauni alijiuzulu, Rais Kikwete alisema Masauni amejimaliza mwenyewe.

Kwa hiyo, majungu na fitina ndiyo chanzo cha Masauni kufikishwa mahali pa kujiuzulu na kukiacha chama kwenye mikono ya makamu wake Malisa anayeongozwa kwa ‘remote control’ ya Ridhwani.

Baada ya Masauni kung’olewa, waliofuatia ni wapambe wake akiwemo Bashe, ambaye alikuwa anapinga njama za kumwondoa mwenyekiti wao. Katika kipindi hicho hicho, naye akaundiwa zengwe kwamba alifanya njama za kutaka kumpopoa mawe Katibu mkuu, Yussuf Makamba.

Bashe aliachwa apumue, wakisubiri wakati mwafaka na hakika baada ya kuruhusiwa kuingia kwenye mchakato wa kuomba kuteuliwa kuwania ubunge, akatumia fedha kupiga kampeni hadi akashinda, wakamshushia rungu la majungu kwamba si raia wa Tanzania.

Wakati Uhamiaji wametoa nyaraka kuonyesha Bashe ni Mtanzania (aliyeukana uraia wa Kisomalia na kuomba uraia wa Tanzania kwa kabila Mnyamwezi; kabila la mama yake), Rais Kikwete alikuwa na nyaraka mfukoni zinazodai si raia.

Wakati sote tunajua anayepaswa kumtangaza mtu si raia ni Uhamiaji au Waziri wa Mambo ya Ndani, katika suala la Bashe, mwenyekiti wa CCM Kikwete anajipa madaraka ya kumvua uraia Bashe.

Wakati wanasheria ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wanasema kwa nyaraka zilizopo Bashe ni raia, Kikwete anampa jukumu John Chiligati kutangaza eti CCM ina ushahidi. Wamempokonya kadi na kumvua nyadhifa zote.

Hapa Rais Kikwete anataka kutueleza kwamba Idara ya Uhamiaji inawajibika kwa CCM na siyo Wizara ya Mambo ya Ndani.

Uko wapi utawala bora? Kama CCM imejipa madaraka ya kumvua mtu uraia, ina maana ina madaraka pia ya kumfukuza au kumpiga PI (Prohibited Immigrant) au kumtangaza mtu asiyekubalika nchini (Persona non grata).

Kama CCM hawana uwezo wa kumfukuza nchini, kwa nini basi tusiamini kwamba mtu akikorofishana na Ridhiwani atashughulikiwa kwa nguvu zote? Hivi si Ridhiwani aliyehusika kumvuruga Francis Kifukwe kuwania uongozi Yanga?

Hivi ndivyo walivyo CCM, wakikuhitaji watakukweza na wakikuchoka watakutokomeza. Masauni hakuomba uenyekiti wa UVCCM, lakini walimkweza, alipopinga maslahi ya wakubwa wamemwondoa kwa aibu.

Bashe mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM ni raia wa Tanzania, lakini Bashe anayewania ubunge si Mtanzania ila Msomali. Asingewania ukubwa huu, NEC ingekaa kimya.

Bashe alikuwa anapigania fursa ya kwenda kusikika kwenye ‘mjengo’ wa Bunge Dodoma lakini sasa anabaki akipigania haki yake ya kuishi nchini vinginevyo itabidi aende Somalia ambako hakujui.

Waziri wa Utumishi, Oscar Kambona alikimbia nchi alipohitilafiana na Mwalimu Nyerere, alipotaka kurudi mwaka 1993 aliambiwa si raia.

Mwaka 1995, CCM walimpitisha Azim Suleiman Premji kugombea kiti cha ubunge Jimbo la Kigoma Mjini huku wakijua alikuwa na utata wa uraia wake. Alishinda lakini matokeo yake yalitenguliwa kutokana na utata huo.

CCM ‘wakafanyafanya maarifa’ akapewa uraia akawania tena ubunge kupambana na mgombea wa CHADEMA wakati ule Dk. Aman Wallid Kabourou. Premji leo ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma.

Kuna jamaa (jina linahifadhiwa) aliingia matatani magari yake yalipokamatwa na meno ya tembo, Morogoro, leo ni mwenyekiti wa CCM mikoa ya Kusini.

Mwaka 2001 CCM iliwavua uraia mwandishi mkongwe, mchambuzi mahiri wa masuala ya kisiasa na kijamii, na mwanasheria Jenerali Twaha Ulimwengu.

Serikali ya CCM ikawavua pia makada wake, katibu mwenezi wa CCM Zanzibar, Moudeline Castico, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Anatory Amani na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Timoth Bandora. Viongozi hao wote walikuwa na uongozi uliotukuka.

Ulimwengu, alivuliwa uraia licha ya ukweli kwamba amezaliwa, amesomea na kufanya kazi nchini kuanzia miaka ya 1970. Amekuwa na hati ya kusafiria ya Tanzania, akawa kada, akashika vyeo TANU Youth League, akawa katibu mkuu wa Umoja wa Vijana Afrika (Pan African Youth Movement), mjumbe wa NEC, mbunge na mkuu wa wilaya za Hai na Ilala.

Februari 2001, Benjamin Mkapa akiwa kwenye Jengo Jeupe (baada ya kushinda tena mwaka 2000), eti Jenerali aliyemsindikiza kuchukua fomu kwa mara ya kwanza mwaka 1995 anatangazwa si raia.

Kisa cha yote hayo ni kukosoa ukatili na mauaji ya wafuasi wa CUF walioandamana kupinga matokeo ya urais mwaka 2000.

Kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2005, wenye CCM walitumia vyombo vya habari “kumvua uraia” mwana diplomasia Dk Salim Ahmed Salim alipojitosa kuwania urais.

Dk. Salim alianza kuwa balozi wa Tanzania nchini Misri hadi kuiwakilisha nchi katika Umoja wa Mataifa, akapigiwa debe kuwania nafasi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (1981), Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU sasa AU), lakini aliporudi kuwania urais Tanzania ikadaiwa ndugu zake wako Oman.

Halafu CCM wakadai ni Hizbu. Dk Salim alilalamika kwamba amehukumiwa kwa sababu ya uarabu wake.

Walipomchukia Elisa Mollel wakamtumia Takukuru akidaiwa kutoa rushwa, aliposhinda uchaguzi wa NEC ukawa umeisha. Safari hii kuna DC, mawaziri pamoja na wabunge kibao wamekamatwa na Takukuru, lakini Takukuru imemng’ang’ania Frederick Mwakalebela ili apishe nafasi kwa Monica Mbega.

Hao ndio CCM, kama hawataki uwe miongoni mwao watakuzushia jambo ubaki unahangaika nalo wakati wao wanakula nchi. Wakikutaka utakula nchi hata kama umeoza ndani na nje.

Nchi nzima imelalamikia viongozi walioingiza mitambo ya kuzalisha umeme chini ya kampuni ya Richmond, lakini CCM wameziba masikio wanakula nchi wote.

Bashe atakuwa amejijua kuwa yeye si miongoni mwao ndiyo maana NEC imeamua kumvua uraia badala ya serikali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: