CCM wakiri gamba limekwama


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version

KWA mwaka mzima uliopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kinaimba na kurudia kibwagizo cha wimbo wa kuvuana magamba.

Wimbo ukapamba. Korasi ikashika, lakini hatujaona mwisho, wala matunda yake. Tumejengewa matumaini makubwa katika falsafa hii ya kuvuana magamba. Baadhi wameiamini wakidhani kutakuwa na mabadiliko, wengine walikataa kuamini.

Walioamini ni kwa sababu kuna watu walitamba kwamba watuhumiwa wa ufisadi wa Richmond, rada, EPA, Meremata, Kagoda na wengineo walikuwa wamefika mwisho. Wangefukuzwa kwenye chama na pengine kuchukuliwa hatua. Kumbe haikuwa hivyo, wameendelea kutamba na kujiimarisha kwenye chama.

Dhana ya kujivua gamba ilipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika vikao vyake vilivyofanyika kati ya Aprili 10 na 11 mwaka 2011 kwa kuwataka wale wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi, kujiondoa wenyewe kwenye nafasi zao, vinginevyo chama kingetumia nguvu kuwaondoa.

Tuliambiwa na Mwenyekiti wa CCM, mwasisi wa falsafa ya kuvuana magamba, Rais Jakaya Kikwete, kuwa chama kimepata sabuni na dodoki, kinaanza kujisugua kuondoa gamba lililochafuka.

Aliibatiza shughuli hiyo kuwa ni kuvua gamba kama afanyavyo nyoka. Aliifafanua na kuipamba maua. Mara ilianza kuimbwa kila kona na makuwadi wa kuvuana magamba kana kwamba ni jambo la kweli.

Baada ya kauli hiyo kutolewa, hoja nyingi ziliibuka. Kila upande ulikuwa na maelezo yake, ya kuvutia na ya kuudhi.

Wengi walisema falsafa hii haiwezekani. Kwanza, walidai mwasisi wake haaminiki na makuwadi wa falsafa hiyo waliozunguka nchi nzima kuieneza ni wasanii, wanatamka mdomoni lakini moyoni hawaamini.

Sisi wachache kina Thomaso, tulisubiri kuona nini kitatokea. Tulidhani baada ya Rostam Aziz kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama, kuanzia ujumbe wa kamati kuu, halmashauri kuu na ubunge wa Igunga, wengine wangefuata –akina Edward Lowassa, Andrew Chenge waliobebeshwa tuhuma za Richmond na rada, na wengineo.

Lakini hadi ninapoandika makala hii, hakuna gamba lililodondoka na hakuna kilichoendelea. Waliobatizwa jina la maganba wamegoma kung’oka kwa madai kuwa hawajui tuhuma zinazowakabili, na chama kimeshindwa kuwang’oa.

Kwa ufupi, ni kwamba magamba yamekwama kuvuka. Yameota mapya na yamekuwa sugu kuliko ilivyokuwa kabla.

Magamba ya sasa yametengeneza makundi yenye nguvu ambayo kuyang’oa ni tatizo na kuyabakiza ni tatizo. Yameunda mawimbi yanayumbisha chombo, huku bahari akitabasamu bila kujua la kufanya.

Tumesubiri kwa hamu kwa muda mrefu kuona jinsi uchafu unavyoyeyuka kwenye ngozi ya chama bila mafanikio. Matarajio yetu ya kuona chama hiki kikongwe kinakuwa safi, kinang’aa kama theluji, kinapata mvuto upya kwa watu wote hasa vijana, yameanza kufutika.

Mara nyingi, huwa nawaambia marafiki zangu kuwa ukitaka kumchinja kobe lazima umvizie, maana ukichelewa akakuwahi yeye, atarudisha kichwa ndani ya gamba na hutaambulia chochote.

Kosa kubwa walilofanya CCM, kuanzia mwasisi wa falsafa na makuwadi wa zoezi hilo ni kutoa muda mrefu wa “magamba kujivua yenyewe” badala ya kuyavua kwa nguvu na kwa haraka.

Suala hili lilisumbua akili za watu wengi wenye akili. Eti unamwambia mtuhumiwa wa ufisadi, mwenye uwezo mkubwa wa kifedha, ajiondoe kwenye chama ambacho ni kinga yake.

Yaani, eti mtu huyu ajiondoe kwenye kivuli na mwavuli wa kulinda madhambi yake, abaki juani ambako anaweza kushambuliwa na kuchukuliwa hatua kirahisi.

Eti, mtu huyu ajiondoe kwenye chama kinachoongozwa na rafiki yake ambaye hawajakutana barabarani, ambaye wameshirikiana “usiku na mchana” kuutafuta uongozi wa juu!

Eti, atoke kwenye chama pekee anachokifahamu tangu anaanza kazi baada ya kutoka masomoni! Aondoke sehemu alikowekeza kwa fedha nyingi na kwa urafiki! Thubutu!

Hivi nani ana uhakika, kati ya wananchi na makuwadi wa magamba, kama urafiki kati ya hawa “jamaa wenye magamba” umekoma au unaendelea?

Maana, mmoja wao anasema wazi kuwa urafiki wao bado ungalipo, wengine wananyamaza. Hata hao wanaonyamaza, hasa wenye mamlaka, hawachukui hatua za kuwavua wenzao magamba, bali wanatumia mtindo wa kutishia tu badala ya “kulamba kichwa.”

Na wakati mwingine tuliwahi kusikia kuwa marafiki hawa wanawasiliana kwa kila hatua, na mmoja wao aliwahi kuhudhuria hata “bethidei pati” nyumbani kwa gamba mwenzake.

Lakini cha ajabu kuna watu, hasa makuwadi wa magamba, hawajaona wala kutafakari mazingira haya. Hawajangundua kuwa wanachezewa mchezo kama watoto wadogo.

Nawashangaa. Yaani makuwadi wa kuvua gamba wanataka mtu aache maziwa na asali aliyotengeneza na kuyalinda kwa miaka mingi, aende kuangukia mchangani ambako atapigwa na mawimbi na kusutwa na kila mtu!

Yaani wanataka mtu aache maslahi mapana ya biashara na miradi yake inayolindwa na serikali kwenye kivuli cha chama, aanze kuhangaika na zimwi lisilomjua linaloweza kummaliza wakati wowote! Hata ningekuwa mimi, nisingekubali.

Wakati mwingine mimi nashindwa kushangaa ni kwa nini wale makuwadi wa kuvuana magamba, wanashindwa kubaini ugumu wa suala hili.

Wanashindwa kuona kuwa wanapambana na kipenzi cha mchukuaji wa hatua. Wanashindwa kuona kuwa wameachwa uchi, kama wachekeshaji au wapiga filimbi wa Hamelin.

Sina shaka kwamba uwezo wao ni mdogo, au wanalinda maslahi yao, au wamelewa sifa za kuzunguka mitaani wakiimba kila siku, “siku za magamba zinahesabika,” mara wanabadili wimbo, ohoo, “siku za magamba zimekwisha.” Lengo la safari zao ni posho za safari tu.

Hata pale CCM ilipokiri kuwa muda wa kuvuana gamba kwa nguvu umefika, kwa sharti la kusubiri hadi Februari au Machi 2012, bado haikutekelezeka.

Chama hicho kilieleza sababu za kuuvutia pumzi mchakato huo, kuwa ni kukamilisha uundaji wa Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili ngazi ya Taifa, lakini hadi hii leo, Mei 23, 2012, hatujaona kitu.

Aliyeeleza hayo Novemba 2011 ni Katibu Mkuu, Wilson Mukama. Aliweka bayana kuwa mipango ya namna tume hiyo itakavyoendesha shughuli zake ilikuwa imekamilika. Kilichokuwa kimebaki ni upatikanaji wa wajumbe wake 14.

Mukama alisema wajumbe hao hawapaswi kuwa na nyadhifa nyingine zozote zinazoweza kuingiliana na kazi yao, akimaanisha kuwa walikuwa na kazi maalumu ya kuyavua magamba badala ya kusubiri yaote sugu kama ilivyo sasa.

Akirejea maagizo ya NEC ya Aprili 2011, Mukama alisema, “Viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama. Wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha mara moja.”

Hadi sasa hatujaona lolote labda bado wanajipanga. Na magamba kwa upande wake yanazidi kukomaa kama ya kobe. Sidhani kama atatokea mchinjaji kwa kufanikisha lengo la CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: