CCM wameacha akili quarter-guard


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KATIKA kambi yoyote ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuki hivi. Unapoingia kwenye lango kuu kuna Quarter-guard.

Hapo ndipo makuruta wote huambiwa waache shahada na digrii (akili) zao kwamba watachukua watakapokuwa wamemaliza mafunzo.

Kuruta akishapokewa, mwili wake ‘usio na akili’ ni mali ya maafande. Atahenyeshwa mchana kutwa, atapewa kazi na usiku disko (kuimba nyimbo) ili wasipate muda wa kufikiri.

Wakijaribu kukaa kufikiria hujikuta wakisinzia maana ‘akili’ wameacha quarter-guard. Maafande hufikiri kwa niaba ya makuruta; hawataki ushauri wala kukosolewa na kuruta.

Ndiyo maana utasikia, “Nikisema down nataka kuona unainuka haraka na nikisema up unakwenda chini kama umeme. Haya down….”

Ole wako usahihishe au utekeleze amri kufuata maana ya maneno hayo, unaweza kupelekwa quarter-guard waliko polisi wa jeshi (MPs) ambao kazi yao ni kutesa.

Hivi ndivyo ilivyo serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inalazimisha wapinzani waache akili zao quarter-guard.

Labda kwa vile mkuu wa nchi Jakaya Kikwete vijana wanasema ni “mjeshi”, katibu mkuu Yussuf Makamba ni mjeshi na aliyekuwa meneja wa kampeni za CCM, Abdulrahman Kinana naye mjeshi—Kanali mstaafu, mawazo yao ni ya kijeshi.

CCM kupitia kwa mjeshi Kinana wamelaani hatua ya wapinzani na hasa CHADEMA kukataa matokeo ya urais wanaodai yamepikwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Lakini mjeshi Makamba ameagiza wabunge na madiwani walioshindwa wafungue kesi kupinga ushindi wa wapinzani.

Kinana alidai CHADEMA wanashangaza kukataa matokeo ya urais, lakini wakayakubali ya ubunge wakati yote yamesimamiwa na NEC hiyo hiyo. Kinana hamshangai Makamba anayechochea vurugu.

Kwa nini Makamba analalamika matokeo ya ubunge wakati NEC wanayoiamini ndiyo imetoa matokeo ya urais? Kama wao wanatilia shaka, kwa nini ionekane wapinzani hawana haki kuhoji matokeo ya NEC?

Kinana aliwataka wabunge waliokataa kutia saini fomu, wakubali matokeo hata kama hawaridhishwi nayo na wafungue kesi halafu Makamba akasisitiza CCM itagharimia.

CCM wanapotaka CHADEMA wapeleke malalamiko yao mahakamani wakati katiba ya nchi hairuhusu matokeo ya urais kupingwa kortini ni kutaka wapeleke akili zao quarter guard.

CCM wajue haya ni mapambano ambayo mtu atatumia silaha yoyote iliyokaribu yake. Kwa vile katiba haijatoa njia mbadala, CHADEMA wameamua kumsusa mkuu wa nchi akabaki bungeni akijifariji, “…hata wanaoondoka, watakwenda watarudi mimi ndiye mkuu wa nchi”.

Baada ya tukio hilo, CCM wamepanga kuandamana ili kulaini. Sawa, polisi wako radhi kuruhusu maandamano ya CHADEMA kulaani wizi wa kura?

Hivi CHADEMA wakiandamana Mwanza au Mbeya au Musoma patatosha? CCM wanachekesha!

Hivi si CCM walioandamana miaka ya 1980 kupinga shilingi kushuka thamani lakini miezi miwili baadaye Nyerere akasalimu amri?

Hivi si wao waliosisitiza mfumo wa chama kimoja lakini wakashindwa?

Hivi si CCM walioandamana kuunga mkono hotuba ya Kikwete kupinga ulaji wa mapanki, lakini wanaendelea kula? CCM wanafanya hivyo kwa vile wamebaki na miili akili zao ziko quarter guard.

Wanachokipinga ndicho wanakifanya. Laiti sheria ya mtu kukutwa na kitu cha wizi ingekuwa inatumika hata katika uchaguzi, kazi ingekuwa imeisha; NEC ingetiwa ndani pamoja na mgombea zilikokutwa kura za urais.

Maana kama mtu amekutwa na mali kama gari, pikipiki au baiskeli ya wizi anashitakiwa kwa kosa la wizi, kwa nini aliyekutwa na kura za wizi aachwe huru? CHADEMA wanadai kura zao zimekutwa kwa Kikwete, kwa nini CCM wanachachawaa?

CCM wachukue akili zao quarter guard wamshauri mkuu wa nchi afanyie marekebisho Katiba, afumue NEC ili kutengeneza mazingira sawa ya ushindani katika chaguzi. Hiyo ni kwa faida ya CCM, wapinzani na utulivu wa nchi.

Ieleweke, kama mtu hatambui matokeo, hawezi kumpa ushirikiano mshindi. Ndivyo ilivyofanya CUF Zanzibar haikutambua ushindi wa CCM kuanzia mwaka 1995 hadi yalipofanyika maridhiano—Katiba ikarekebishwa na ZEC ikafumuliwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: