CCM wamekanyaga sheshere


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Mtazamo

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaelekea imekanyaga mdudu mchafuzi. Mdudu huyo Zanzibar anaitwa sheshere, Wabena humwita hilufi, Wasangu wanamwita shilufyana Wahaya humwita …

Mtu akikanyaga sheshere, hawezi kufika anakokwenda; atazunguka sana, atapitiliza hata eneo analokwenda hadi ashikwe au asimamishwe na mtu anayemfahamu.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa Serikali ya CCM. Imekanyaga sheshere. Inasema ovyo, inayumba njia nzima tangu ilipoanza safari mwaka 2005. Haieleweki. Mara inasema maisha bora yanawezekana, mara wabunge wake wanalia Ilani ya CCM haitekelezeki.

Tazama mkanganyiko huu. Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta anasema Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe amelishwa sumu. Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha anaibuka na kumtaka Sitta awasilishe ushahidi.

Sitta anasisitiza hatawasilisha anachotakiwa kwa sababu hata “polisi wanajua.” Anamshangaa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukaa kimya kuhusu suala hili. Shamsi Vuai ananywea anasema polisi wameanza kuchunguza.

Wanahabari wamewahi kuwafuata watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, watoe maelezo kuhusu afya ya Dk. Mwakyembe. Wamesema ni siri.

Sitta anapoibuka na kusema bayana Dk. Mwakyembe amelishwa sumu, kuna kila sababu ya kuamini serikali ya CCM inajua ila inaficha. Je, analindwa nani?

Tazama suala la posho za wabunge. Taarifa ya ikulu kwa vyombo vya habari imesema Rais Jakaya Kikwete hajaidhinisha posho mpya za wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 wakati wa vikao. Taarifa ile iliishia kuwataka wabunge watumie busara.

Kama Rais ndiye mwenye mamlaka kisheria ya kuidhinisha posho hizo, nani aliyeidhinisha? Je, ni Spika Anne Makinda au Waziri Mkuu, Mizengo Pinda? Je, wana mamlaka kisheria?

Katikati ya matatizo makubwa ya kiuchumi; wahisani wakitoa chini ya asilimia 40 ya ahadi walizotoa na hivyo kusababisha nakisi ya Sh. 214 bilioni katika bajeti, serikali imewasilisha marekebisho ya kiwango cha ushuru wa maji ya kunywa na kupunguza matumizi ya fedha katika baadhi ya maeneo.

Katika kipindi hiki kigumu cha uchumi na nakisi katika bajeti, serikali imeona busara kuwachotea wabunge Sh. 200,000 zaidi badala ya Sh. 70,000 na Sh. 80,000 za kujikimu kila siku.

Wabunge wa CCM wakitetea ulaji huo usio jasho, wanamuita mnafiki yule anayepinga posho za wabunge, lakini wabunge haohao wanasema anayepinga posho za madaktari ni mzalendo. Ni kukanyazga sheshere.

CCM wamekanyaga sheshere kiasi cha kuona madaktari, ambao hakuna ubishi wanafanya kazi katika mazingira magumu, hawastahili malipo mazuri. Kwa sasa, daktari akiitwa kazini, analipwa posho ya Sh. 10,000 tu.

Nini kimesababisha wabunge wa CCM wajitazame wao tu, mafisadi na wafanyabiashara na kuacha wakulima na wafanyakazi?

Serikali hii ipo kisheria, lakini kiutendaji imesambaratika ndiyo maana makada wake wanasema wazi itakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amewataka wabunge wa CCM kusikiliza kilio cha wananchi na ushauri wa wasomi, lakini wakiongozwa na Spika Makinda, wanatembea kama wamekanyaga sheshere.

Inasikitisha kuona Spika aliamuru kuchunguzwa uhalali wa fedha alizochangisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo ili zichukuliwe hatua za kisheria.

Makinda mwenyewe amedai ikulu iliidhinisha posho za wabunge lakini ikulu imekana. Makinda anasimamia wapi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: