CCM wamekosea ‘kumshika matiti’ binti yao


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

KUMKOSEA adabu mtoto wako wa kike, tena mtoto mwenyewe mkubwa aliyekwishavunja ungo, ni kosa kubwa lisilosameheka katika mila za makabila mengi duniani yawe ya Kiafrika, Ulaya, Uchina, Uhindini na hata Marekani.

Kwa sababu hiyo nawaasa wazazi wenzangu, chondechonde, msithubutu hata siku moja, hata kwa bahati mbaya kuwashika matiti mabinti zenu yasije yakawakuta yale yanayomkuta leo mzazi aitwaye Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwani mnafikiri mambo yanayoisumbua CCM na serikali yake yanatokana na nini? CCM na serikali yao wanasema lakini hawasikiki, wanashauri lakini umma haushauriki hata wanaposhawishi hakuna anayeshawishika; Kwa nini?

Makosa wameyafanya wenyewe CCM na serikali yao kwa kumshika mtoto wao wa kike matiti mchana kweupe mbele ya walimwengu wote. Kwa kudharau sheria, kwa kukiuka sheria, kwa kutosikia kilio cha wananchi, CCM walijitakia yanayowakuta leo.

Ipo sheria inayoelekeza makosa dhidi ya serikali, mashauri kama jinai. Sheria hiyo inaitwa Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya sheria za nchi. Kanuni ya Adhabu imeyataja makosa mengi pamoja na adhabu ya kila kosa kwa yule atakayethibitika, bila shaka yoyote, kuwa katenda kosa dhidi ya Jamhuri.

Pamoja na hiyo, ipo sheria nyingine ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sheria Na. 9 ya mwaka 1985, Sura ya 20 ya sheria za nchi. Sheria hii ndiyo inayoonesha jinsi mtuhumiwa wa kosa lolote lililoainishwa kwenye Kanuni ya Adhabu atakavyokamatwa.

Sheria pia inaelekeza mtuhumiwa atakavyopekuliwa, atakavyotoa maelezo polisi, atakavyofunguliwa mashitaka na namna ushahidi dhidi yake utakavyotolewa. Pia inaelekeza haki yake ya kujitetea kabla ya mahakama kutoa uamuzi.

Sheria hizi mbili zilikiukwa na utawala wa awamu ya tatu na zinaendelea kukiukwa na awamu ya nne. Zimepuuzwa waziwazi kiasi cha wakosaji, wahalifu, wezi wa mali ya umma, matapeli na mafisadi wakubwa, papa na nyangumi, kuachiwa huru.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inataka mtu yeyote atakayetuhumiwa kutenda kosa lolote lilioainishwa kwenye Kanuni ya Adhabu kama vile wizi, utapeli, ubadhirifu wa mali ya umma au kughushi kwa aina yoyote ile akamatwe.

Zaidi ya kukamatwa, sheria inaelekeza mtuhumiwa huyo apelekwe polisi, aandikishe maelezo na aswekwe korokoroni wakati upelelezi ukiendelea, lakini lipo sharti kwamba mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ndani ya saa 24 na dhamana itafaa kutolewa akitimiza masharti ya dhamana yenyewe.

Serikali iliyo madarakani ni ya CCM. Serikali ya CCM inapaswa kuheshimu, kusimamia na kutekeleza matakwa ya sheria zilizopo. Na viongozi wa CCM waliopewa madaraka serikalini waliapishwa na wakaahidi katika kiapo hicho kutekeleza matakwa ya sheria na si vinginevyo.

Kwa bahati mbaya sana, hali haikuwa hivyo pale ulipotokea ukwapuaji pesa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Eti, safari hii wahalifu waliokiri kuhusika na wizi huo waliachiwa kuranda mitaani na kuombwa kwenda hotelini au ofisini kukutana na wakubwa kupanga namna ya kulipa pesa walizoiba! Na wengine hadi leo ninapoandika haya, hawajalipa walichoiba. Kitu kibaya zaidi ni kuwa hawatajwa waziwazi ingawa wanajulikana.

Hivi ndivyo watawala wa CCM walivyobaka sheria na kunajisi mwenendo wa kesi za jinai. Yamesemwa mengi ikiwamo taarifa kuwa pesa zilizoibwa zilitumika kuhonga na kununua mawakala wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM na wakati wa uchaguzi mkuu wenyewe.

Mwizi wa mali ya umma unakaa naye mezani, mnakunywa chai, kahawa au valuu, mnaulizana namna atakavyorudisha pesa alizoiba! Huku ndiko kumshika binti yako matiti. Wakubwa wenzako hawatakuamini tena kusafiri gari moja au kukaa nyumba moja peke yenu wewe na binti yako huyo.

Halafu anatokea mtu anasema eti Rais ni Mkuu wa nchi hivyo aaminiwe na kupelekewa maoni ya wananchi baada ya kukusanywa na Tume ya kukusanya maoni ya marekebisho ya katiba. Ni nani mwenye imani kuwa maoni hayo yatapelekwa na kufika salama bila ya kuchakachuliwa?

CCM wamemshika binti yao matiti hadharani sote tunaona! Leo, waaminike kukabidhiwa mtoto wa kike wa jirani yao ambaye ni mchakato wa katiba, na ktuarajia wakae naye salama. Hata wakisema rais ni mkuu wa nchi, sawa; ni mkuu wa vyombo vya dola, sawa; ni kamanda wa majeshi ya ulinzi na usalama, sawa. Kwa hiyo?

Swali ni, je, wakati wa EPA hatukuwa na mkuu wa nchi? Hatukuwa na kamanda wa majeshi ya ulinzi na usalama? Hatukuwa na Jeshi, Polisi, Takukuru, Usalama wa Taifa, JKT na utitiri mwingine wa walinzi? Ilishindikanaje kukamata na kushitaki badala yake watu wakakutana faraghani kupatana zitarudishwaje fedha za wananchi?

Hapa ndipo wananchi walipopoteza imani kwa CCM na viongozi wao. Walimshika binti yao matiti. Rais yupo tunamwona, alipigiwa kura na kutangazwa na tume na baadaye kuapishwa. Yeye ni mkuu wa nchi kikatiba na kisheria, lakini je, umma unamwamini kama rais au kama mkuu wa nchi?

Mwenyekiti wa CCM ni mkuu wa nchi, lakini anaaminiwa na raia wake kuwa atatenda haki na siyo kufanya upendeleo kama waliofanyiwa wezi wa fedha za EPA? Hii ndiyo hoja kuu. Wanaomuua mwizi wa kuku lakini wakamwachia mwizi wa EPA wataaminika kuendesha kwa haki mchakato wa katiba? Mie siamini.

Pia wananchi walishuhudia baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, mkuu wa nchi akiteua rafiki zake, maswahiba zake na washikaji zake kuwa mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu wakuu na wakurugenzi katika wizara. Nani ataamini leo kuwa rafiki, maswahiba na washikaji wa mkuu wa nchi hawatateuliwa kwenye Tume ya kuratibu maoni au kwenye Bunge la Katiba?

Polisi wanaoweza kutabiri kitakachotokea kesho mjini Arusha kwenye maandamano ya CHADEMA lakini wanashindwa kumwona mbele yao Ismael Aden Rage na bunduki kiunoni jukwaani wataacha upendeleo kwenye mchakato wa katiba?

Kama kweli CCM na wakuu wao wana nia njema kwa nini tutishane? Kama kweli lengo ni katiba nzuri kwa sote na siyo CCM pekee kama alivyoongeza kusema Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, kwa nini mikutano ya wazee wa CCM waisho Dar? Kwa nini hotuba za wana-CCM, zikiwamo za mkuu wa nchi zijae vijembe, kebehi na vitisho?

Tambo, vitisho vya kutumia majeshi na vyombo vingine vya dola havitawafanya wananchi na hasa wapinzani kuamini kuwa mchakato wa marekebisho ya katiba utaendeshwa kwa haki na watu wanaobaka sheria. CCM wameumbuka na hawataaminika tena. Tatizo si CHADEMA tatizo ni kukosekana IMANI kwa watawala.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: