CCM wana ugonjwa wa kusahau


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

KATIKA maisha yake yote, Bogi Benda alikuwa msumbufu. Mtu wa vituko, dharau, kejeli. Bali alivumiliwa kwa vile alikuwa ‘bosi’.

Kuna wakati alipotaka kuzima hoja fulani ili kusumbua tu watu, aliamua kulala na kukoroma kwenye vikao.

Kuna siku alikwenda hospitali akitaka atibiwe ugonjwa wa kusahau aliodai unamsumbua sana. Akabahatika. Alimkuta daktari nje na hapohapo akamweleza kinachomsumbua.

Daktari akamtaka waende ndani ambako kuna vifaa. Daktari anasema, “Haya mzee tulia, nieleze tatizo limeanza lini na unajisikiaje ili nichukue maelezo na kubaini tatizo.”

“Tatizo? Tatizo gani?” eti kasahau. Lahaula walakuwata! Si hivyo tu, siku nyingine alikwenda akiwa ‘ameutwika’ akilalamika mwili unauma mno. Daktari akafanya kazi yake akampima kila mahali, lakini alibaini Bogi Benda alikuwa anasumbuliwa na uchovu wa mwili kutokana na ulevi.

“Samahani bosi, sijagundua tatizo lolote isipokuwa nadhani ni mchoko wa mwili kwa sababu ya mtungi mwingi,” alisema daktari. Bogi Benda akijua ameumbuka akachukua shati lake akafoka huku anageuza maneno; “Kwa hiyo nirudi ulevi wako utakapokuwa umeisha siyo?”

Kwa hiyo, haikuwa rahisi watu kujua ni wakati gani bosi wao ana busara na wakati gani ana akili chakavu. Mabosi wa aina ya Bogi Benda, yule mhusika mkuu katika katuni maarufu za gazeti la Daily News miaka ya 1980 iliyokuwa inachorwa na James Tumusiime, Mganda aliyekuwa anaishi Nairobi, wamejaa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tazama, viongozi wa CCM wachovu kisiasa wanaokoroma bungeni, wamebebana, safari hadi Arumeru Mashariki kwa kampeni za uchaguzi mdogo – kama Bogi Benda – bila kujua wanakwenda kufanya nini.

Tazama, miaka yote CCM waliwaaminisha watu kuwa CHADEMA wanafanya ufisadi kutumia helikopta katika kampeni. Lakini, katika chaguzi ndogo za Kiteto na Igunga nao walitumia. CCM wakatumia helikopta tatu kwa ajili ya mgombea wao wa urais katika uchaguzi mkuu 2010.

Leo, eti wanaibana CHADEMA inafanya ufisadi kutumia helikopta Arumeru!

Bahati mbaya CCM wamepumbaza, wamewatia ujinga na kuwaloga watu kwa hirizi ya amani.

Tatizo la Arumeru, kabla na baada ya uhuru ni ardhi. Wameru walifikia mahali wakachanga fedha wakamtuma Japhet Kirilo kwenda Umoja wa Mataifa kudai ardhi yao.

Badala ya kuzungumzia hayo, mgombea wao anasema atapeleka maji ya bomba ili Wameru wasiwe na meno yenye rangi. CCM inaona hili ndio tatizo.

Halafu waziri usingizi akakusanya wazee kwa vijana akidai kapata bomu la kulipua. “Niseme, nisiseme,” aliuliza waziri usingizi na akajibiwa, “Semaaaaaaa.”

“Si mnawaona jamaa hawa (akionyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA) wanaendesha harambee?” alihoji na umati ukajibu, “Ndiyoooo.” Akasema, “Wamekimbiwa na wafadhili Conservatives wa Uingereza kwa sababu Serikali ya Tanzania imekataa ushoga.”

Kwa waziri usingizi, CHADEMA kukimbiwa na wafadhili ndiyo tatizo la wakazi wa Arumeru. Pamoja na usomi wake na uzoefu wa miaka mingi serikalini, waziri usingizi huyu hajui kuwa chama kikiingia madarakani, hata marafiki hubadilika!

Mwingine, badala ya kueleza suala la ardhi akaenda Arumeru akaorodhesha ukoo wa Mwalimu, halafu akamtoa mmoja akisema “katika maisha yangu yote sijawahi kuambiwa huyu ni mtoto wa mwalimu wangu!”

Amezodolewa, amerudi Dar akilalamika ameaibishwa! Hivi alitaka upuuzi huo uaminiwe? Uchovu huu wa kisiasa ndio unachangia viongozi wakuu na hata wabunge kuzomewa. Ole wao!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: