CCM wanachafua na kujichafua


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

YAPO mabango kadhaa katika makutano ya barabara za Nyerere na Kawawa, Dar es Salaam, lakini moja ni lile linalokinadi Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Bango hilo kubwa linasomeka, “Kwa amani na utulivu, chagua CCM, chagua Kikwete”.

Maneno hayo yako upande wa kulia wa bango kama unavyoliangalia na upande wa kushoto kuna picha ya mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete akikagua gwaride la Jeshi la Wananchi.

Ujumbe unaopatikana katika bango hilo ni kwamba kuwepo kwa amani na utulivu kumo mikononi mwa CCM au bila CCM hakuna amani wala utulivu.

CCM wanataka kueleza kupitia bango hilo kuwa jeshi haliwezi kusimamia amani na utulivu bila chama hicho tawala. Huu ni mwendelezo wa kampeni chafu na za vitisho zilizofanywa na chama hicho tangu mwaka 1995.

Miaka ya nyuma walikuwa wanasema moja kwa moja kwamba vyama vingi vitaleta uhasama na mapigano au vita. Leo wamebadili lugha, lakini ujumbe ni uleule wa vitisho.

Hadi leo CCM wanadai mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi za Rwanda, Burundi, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni kutokana na vyama vingi.

Hawa, kazi yao ni uzushi, uongo, ubaguzi, hila na kuchafua huku wakisahau kuwa wanajichafua wenyewe.

Wakitembelewa na wageni, hasa wazungu, wanadai wao ndio walioruhusu vyama vingi, lakini wakipanda katika majukwa ya siasa, hasa vijijini wanafundisha huku jasho likiwatoka kuwa vyama vingi vinasababisha vita. Hii ndiyo sura ya kigeugeu – CCM.

Hawana sera na hawana dira kama alivyosema hayati Horace Kolimba. Wanashika hili, wanaacha na sasa wanataka wananchi wachague CCM kwa sababu wao ndio wameshika jeshi na polisi.

Je, na wapinzani wawe na jeshi lao kama Lebanon? Maana katika nchi hiyo serikali ina jeshi lake na kundi la Hizbullah chini ya Hassan Nasrara anayeishi Syria, lina serikali ndani ya serikali. Wana shule, hospitali na zaidi jeshi linalopambana na Israel kila mara.

Kwa hiyo, wananchi wajue kuwa polisi wanapowapiga virungu wapinzani ni kwa vile wameagizwa na chama tawala. CCM inataka watu wajue kimatendo, jeshi na polisi ni miongoni mwa jumiya za CCM sawa na Umoja wa Vijana (UV-CCM), Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na umoja wa Wazazi.

Kwao, kuwa mpinzani ni kujiweka katika kundi ambalo litapigwa virungu na majeshi hayo kwa kisingizio cha kulinda amani na utulivu. Hizi ni kampeni za vitisho; ni chafu.

Mara baada ya kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini, majeshi ya ulinzi na usalama yalipaswa kujiweka kando na siasa. Jamii iliamini hivyo na upinzani ulijenga imani kinadharia kwamba wangetendewa haki, lakini taratibu wamekuja kugundua kuwa kivitendo polisi hutumiwa na CCM.

CCM inalazimika kusema uongo, kutoa vitisho vyote hivyo kwa sababu imebanwa mbavu. Tazama mabango yalivyojaa kila kona kana kwamba ni chama kipya.

Kama CCM ni kongwe na kama Kikwete ni maarufu na anauzika kama wanavyodai, kwa nini wameweka nguvu kubwa mpaka kutumia fedha za walipakodi katika kuchapisha picha za kutundika mitaani?

Kama kweli wanapendwa sana na wananchi, kwa nini wanatumia vyombo vya habari vya serikali kuwachafua wapinzani kwa mambo binafsi? Hivi ni chama gani duniani kinachosema kinaingia ulingoni kwa nia ya kuvuruga amani na utulivu?

Hivi si chini ya utawala wa Kikwete wananchi wameshuhudia mauaji makubwa ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara? Hiyo ndiyo amani na utulivu?

Nani amesahau wana-CCM wanavyorushiana makonde katika vikao vya kusaka wagombea uongozi wa ndani ya chama na wagombea ubunge?

Nani amesahau CCM ilivyokosesha amani na utulivu nchini kutokana na utawala huu kukumbatia mafisadi?

Wananchi wajue kwamba majeshi hayaleti amani. Majeshi hulinda amani iliyopatikana kwa njia ya siasa – sera na mipango ya kiuchumi na kijamii na inayotekelezeka.

Kwa ufupi, amani na utulivu siyo sera ya CCM; ni matakwa ya kila mwananchi na wajibu wa kila chama. Chama chochote kikishinda kinawajibika kusimamia hilo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: