CCM wanahatarisha amani, mshikamano


editor's picture

Na editor - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MARA baada ya kuapishwa kushika kipindi cha pili cha uongozi wake, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai kwa Watanzania wote na hasa wanasiasa wa vyama vya upinzani kusaidia juhudi za kutibu majeraha ya udini yaliyosababishwa na kampeni.

Rais Kikwete alikiri kwamba, hata wao Chama Cha Mapinduzi (CCM) walifikia mahali wakapitiliza katika kampeni hizo hivyo ametaka washirikiane kurejesha mshikamano na umoja ili tubaki wamoja, wenye amani na utulivu.

Tunamuunga mkono Rais kwa kutambua hilo mapema maana madhara ya migogoro ya kidini ni makubwa na hakuna anayeweza kupona. Si wanasiasa, viongozi wala wapambe au wafuasi wa vyama, wote wataangamia ikiwa hakutakuwa na uvumilivu wala amani.

Hata hivyo, tunamtaka Rais Kikwete na chama chake waonyeshe dhamira ya kuponya majeraha ya udini na ukabila ambayo kwa kiasi kikubwa yalisababishwa na CCM.

Hii imekuwa kawaida ya CCM kukimbilia kwenye udini na ukabila kila kinapobanwa kwenye kampeni tangu uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Tulishuhudia mwaka 1995 CCM ikisingizia Chama cha Wananchi (CUF) kuwa kinafanya kampeni misikitini, na NCCR-Mageuzi ni ya Wachagga.

CCM na wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani na jeshi zima la wenyeviti, makatibu wa mikoa na wilaya hueneza sumu mbaya ya chuki za udini halafu uchaguzi ukimalizika—kwa vile wao huibuka washindi—huomba wasaidiwe kutibu majeraha ya udini.

Mwaka huu, tumeshuhudia pia viongozi wa ngazi za juu wa CCM akiwemo Kikwete wakilazimisha ionekane kuna udini katika vyama vya CHADEMA na CUF. Hii ni hatari kwa chama kilichopewa dhamana ya kuongoza nchi kuzua mambo ili kipate ushindi.

CCM katika kampeni zao walionekana kujipanga vizuri, wakatengeneza picha, wakateua ‘askari’ wa kampeni, wakadhibiti vyombo vya habari, hata opena kwenye baa zilikuwa zinaimba umaarufu wao.

Kwa nini waliingiza udini wakati wanajua migogoro ya kidini imesababisha madhara makubwa katika nchi nyingi barani Afrika na duniani?

Tujuavyo, vyama vyote vya siasa ni vya kitaifa, vina wanachama bara na visiwani na vinaungwa mkono na wakristo na waislamu. Kama kuna chama cha waislamu tu au wakristo pekee, kwa nini kisifutwe?

Kwa sasa, mbinu hizo chafua zimesaidia CCM kushika madaraka, lakini tunaomba watu wenye busara kama wapo katika chama hicho, wakae watafakari upya kwani mwelekeo wa chama chao unahatarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: