CCM wanamhadaa nani?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KATIKA mdahalo wa hivi karibuni uliowakutanisha wawakilishi wa vyama vitatu – CCM, CHADEMA na CUF – mshiriki kutoka CCM alitonesha vidonda aliposema kwamba ana imani itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea inaweza kuwavusha Watanzania kwa miaka 50 mingine .

Mshiriki huyo, ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM bado inaamini sera ya ujamaa na kujitegemea na kwamba misingi yake bado inasimamiwa kama ilivyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.

Nape, katika mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Stars TV, alisema kwamba CCM inataka kujenga Tanzania katika misingi ya ujamaa, kuishi kama ndugu na kuheshimiana.

Mshiriki huyu, ambaye amekuwa akitoa, katika siku za hivi karibuni, kauli tata, hii ni moja ya kauli, ambazo tunashindwa kuelewa viongozi wa CCM wana lengo la kumhadaa nani.

Mwaka 1967 Watanzania walitembea kwa miguu nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha lililoanzishwa kusimamia sera ya ujamaa na kujitegemea. TANU ndiyo iliasisi na CCM ilirithi sera hiyo.

Lakini katika hali ya kushangaza, mwaka 1990, viongozi wa CCM waliketi Zanzibar kufuta Azimio la Arusha na miiko ya uongozi na sera za ujamaa na kujitegemea.

Tangu wakati huo serikali ya CCM ikaanza kuhubiri ubinafshaji, utandawazi na soko huria. Chini ya sera za ubinafsishaji wananchi wakaanza kushuhudia serikali ikijitoa katika umiliki na uendeshaji mashirika ya umma badala yake ikayauza kwa wageni.

Chini ya sera ya utandawazi na soko huria, Watanzania wakashuhudia serikali ikijitoa kusimamia bei ya bidhaa kwa maelezo nguvu ya soko ndiyo itaamua.

Japokuwa ni kweli Katiba bado inataja sera ya Ujamaa na Kujitegemea, utendaji ni wa kibepari. Tangu mwaka 1990 CCM ilikoma kunadi ujumaa na kujitegemea kwa vile ilikumbatia ubepari.

Kwa hiyo CCM wanaposema wana imani na ujamaa na kujitegemea wakati maeneo yenye rutuba, yenye madini, usafiri na viwanda wamewapa wageni, wanamdanganya nani?

Wanamhadaa nani wanapodai wanapinga ufisadi wakati viongozi na makada wa CCM ndio washirika wakuu wa ufisadi? Unafiki huu unawasaidia vipi CCM?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: