CCM wanamhitaji Dk. Slaa


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

UTEUZI wa Dk. Willibrod Peter Slaa kugombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) una mambo mengi yanayohitaji tafakuri kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kabla ya uteuzi wake, Dk. Slaa amekuwa akihangaika, kama katibu mkuu wa chama, kumtafuta mgombea urais anayekubalika.

Hata pale baadhi ya watu walipompendekeza yeye, alikataa na kuongeza kasi usiku na mchana kutafuta mgombea mwingine.

Ilifika mahali hata maofisa wenzake wa chama walianza kumwogopa na kutodiriki tena kumwambia habari ya yeye kuwa mgombea.

Fursa ilijitokeza tu pale alipopata safari ya ghafla kwenda Karatu kwa siku tatu. Hapo ndipo mikakati ilifanyika kwa uhuru na kwa haraka, ili akirudi akute imeiva ya kumtaka akubali kuwa mgombea urais.

Hata baada ya kurudi ofisini, aliponusa harufu ya mpango huo alikuwa mkali kwenye sekretariati ya chama, lakini mgomo wake haukufua dafu kesho yake ndani ya Kamati Kuu.

Hii inaonyesha kuwa hapa tuna mtu anayeheshimu ikulu; aliye tayari kuwatanguliza wengine anaodhani ni wazuri kuliko yeye. Ukipima hali hii na kulinganisha na mbio za kutafuta urais katika vyama vingine, ikiwemo CCM, utaona tofauti kubwa ya kimtazamo.

Ndiyo maana baadhi ya wana-CCM wanaoweza kuthubutu kufikiri kwa uhuru, wamenieleza kuwa kama CHADEMA wangemtangaza Dk. Slaa kabla ya mkutano wao mkuu kule Dodoma, Julai mwaka huu, si ajabu hali ya mkutano ule ingebadilika sana.

Mmoja alienda mbali zaidi na kusema, “si ajabu utamaduni wetu wa kuachiana miaka 10 ungetikiswa.”

Ni Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyesema mwaka 1995 kuwa upinzani unaweza kuisaidia CCM kuwa makini zaidi katika kuteua mgombea wake.

Sioni aibu kusema mpaka hapa kuwa, kukosekana kwa umakini katika uteuzi wa wagombea ndani ya CCM, kunasababishwa na ama unyonge wa vyama vya upinzani au udhalilishaji na uonevu wa vyombo vya dola kwa vyama hivyo.

Jukumu la kurejesha umakini huo ndani ya CCM na serikali yake, sasa liko mabegani mwa Dk. Slaa kwa sababu kadhaa.

Dk. Slaa ni mnyenyekevu na msikivu. Haleweshwi na sifa anazomwagiwa na watu, bali huzisikia kisha huendelea mbele na jitihada za kuutafuta ukweli na kuutumikia. Anapingana na dhana ya watu binafsi kuwa mtaji na maarufu kuliko vyama vyao.

Umakini wake umemwezesha kujijengea sifa katika utetezi wake au upinzani wake kwa mambo yasiyo na faida, kwani kabla ya kutetea na kujenga msimamo, hutafiti na kuuliza sana.

Kutokana na tabia hii, Dk. Slaa amevuna marafiki wengi ndani ya serikali, vyama vya siasa, madhehebu mbalimbali na hata watu wa kada ya kawaida.

Hili ndilo linamfanya aonekane jasiri wa kuweza kuvisaidia vyama vingine katika kupambana na udhalimu ndani ya vyama hivyo na hatimaye kukuza uzalendo kuanzia ndani ya vyama mbalimbali.

Kwa mfano, CCM imewatisha na kuwasambaratisha wanachama wake wenye maoni tofauti. Hivi sasa wanachama hao wanaishi kwa hofu ya kufukuzwa uanachama au hata kuhofia maisha yao endapo watadiriki kujiunga na vyama vingine na kuipinga CCM.

Kimsingi, chama tawala hivi sasa ni chama-dola kisicho na uhalali wa kuongoza nyoyo za wanachama wake. Kinaishi kwa ubabe wa fikra na hujuma kwa maoni tofauti kupitia vyombo vyake vya dola.

Dr. Slaa ameleta nuru ya tumaini mioyoni mwa baadhi ya watu hao. Hivi sasa wanaweza kufikiria kuhama vyama vyao iwapo na kujiunga na Dk. Slaa iwapo hawatasikilizwa.

Hili likifanyika, Dk. Slaa atakuwa amevisaidia vyama hivyo kuanzisha utamaduni mzuri wa kukubali kukosoana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: