CCM wanamkomoa nani: wapinzani au wananchi?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Meneja kampeni wa CCM, Abdulrahman Kinana

KATIKA baadhi ya hotuba zinazorudiwa katika vituo vya televisheni alizotoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika miaka ya 1990, inaonekana alikuwa anatumia lugha kali.

Alikuwa anaonekana kukerwa na maelezo au majibu rejareja yaliyokuwa yanatolewa na viongozi kwa masuala mazito.

Mathalani, katika hotuba moja anasema, “Kama mtu atakwambia jambo la kijinga na wewe ukajua kwamba jambo hilo ni la kijinga, lakini ukakubali atakudharau.”

Mwalimu Nyerere leo hayupo, angekuwepo angetumia lugha hiyo kukemea kauli za viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliofikia mahali pa kudharau uwezo wa kuchambua, kuchanganua na kupambanua mambo. Tazama majibu yao;

  1. Ndani ya CCM hakuna mafisadi ila kuna ufisadi!
  2. Fedha zilizochotwa kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) zilikuwa kwa kazi maalum baadaye Waziri Zakia Meghji anajiumauma, “Aaah nanihii alinipotosha!”
  3. Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na wafuasi wake wanasema, “Elimu bure haiwezekani”.
  4. Halafu meneja kampeni, Abdulrahman Kinana anashadidia, eti hata Mwalimu Nyerere hakusomesha watoto bure ila alikopa fedha nje kwa ajili ya kusomesha bure; fedha alizokopa zilianza kulipwa awamu ya tatu.

Hayo ndiyo majibu ya viongozi wa CCM. Kinana hajui serikali inaposema itasomesha bure ina maana inabeba dhamana ya kutafuta fedha kutoka vyanzo vyote—kodi, mikopo na misaada—ili kugharamia elimu.

Kinana anasahau kwamba hata serikali hii, imebeba dhamana hiyo ikishirikiana na mashirika ya kimataifa; Umoja wa Mataifa (UN), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF) na Benki ya Dunia (WB).

Viongozi wa CCM walidai na misuli iliwatoka mwaka 2000, kwamba elimu bure haiwezekani, lakini mwaka 2001 wakasalimu amri wakaanza kutoa elimu bure kama Prof. Ibrahim Lipumba alivyonadi sera ya elimu ya Chama cha Wananchi (CUF).

Mashirika ya UN, WB, UNICEF, ambayo yanafadhili mradi wa elimu bure katika nchi zinazoendelea yanasema inawezekana kutoa elimu bure. CCM hawana hoja.

Masikitiko

Kinachosikitisha ni kwamba Kinana, Mbunge na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi amevaa miwani ya mbao asione wala kukumbuka Malengo ya Milenia yaliyopitishwa na UN mwaka 1990 (siyo mwaka 2000 kama nilivyosema awali).

Kikwete alikuwemo katika serikali ya awamu ya pili na akawa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa. Anajua siyo tu malengo, bali pia programu ya utekelezaji wake.

Spika Sitta ambaye amewahi kushika nyadhifa nyingi ikiwemo ya Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), anajua mambo mengi ya kimataifa. Lakini linapofika suala la chama, anafumba macho na kuungana na wale wanaosema “elimu bure haiwezekani”. Inasikitisha!

Ukweli ni kwamba juhudi za kuhakikisha elimu bure inatolewa zinafanywa na UN, UNICEF na WB.

Septemba 2000, mashirika hayo yalifanya mkutano ili kuona namna ya kupata fedha za kugharamia huduma bure ya elimu kusaidia juhudi za serikali zenyewe.

Mwezi uliofuata yaani Oktoba 2000 ulifanyika mkutano mkubwa wa kimataifa Dakar, Senegal kuangalia namna ya kufikia mamilioni ya watoto duniani waliokosa elimu na kuhakikisha kila aliyefikia umri wa kwenda shule anapata nafasi.

Rais Kikwete anajua ila anaghilibu watu ili wapinzani wake Prof. Lipumba na Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaosema elimu bure inawezekana, waonekane waongo mbele ya macho ya CCM. Anamkomoa nani, Prof. Lipumba, Dk. Slaa au maelfu ya wananchi maskini wanaoshindwa kupeleka watoto wao sekondari na kusomesha elimu ya juu?

Rwanda imeweza

Kwa kuwa Malengo ya Milenia yaliwekwa mwaka 1990 baadhi ya nchi zilianza kutoa elimu bure miaka michache baadaye.

Nchi zote jirani; Malawi, Burundi, Kenya, Uganda, Zambia zinatoa elimu bure hadi ngazi ya sekondari na Rwanda hadi kidato cha sita. Rwanda isiyo na madini wala bandari imeweza Tanzania inashindwaje?

Hata baadhi ya nchi zilizoendelea hutoa elimu bure katika baadhi ya shule na vyuo nchini Ujerumani, Sweden, Denmark na Finland.

Bajeti ya Kikwete

Ingawa Kikwete anadai kuwa elimu bure haiwezekani, katika bajeti yake ya 2010/ 2011 ametafuta na kutenga Sh 1.7trilioni kwa ajili ya kulipa kampuni za kibepari zinazodaiwa kupata hasara katika biashara ya pamba. Kama ameweza kupata fedha za kufidia kampuni za kufikirika, kwa nini ashindwe kupata fedha kwa ajili ya elimu bure?

Hapa moja kwa moja serikali imethibitisha kwamba inawajali, inaendeshwa na kuwatumikia mabepari, ndiyo maana inatetea na kuwalinda mafisadi ndani ya CCM.

Dawa mujarabu

Mwalimu Nyerere alijaribu kutafuta dawa ya kunywesha wahujumu uchumi lakini akafanikiwa kiasi; baadaye wakaja kuhujumu nia safi ya Rais Mwinyi kulegeza masharti ya kiuchumi, wakamnasa Mkapa na sasa Kikwete hawezi kufurukuta.

Kwa kuwa imejulikana mafisadi wamo ndani ya CCM na ndio wanaendesha serikali, dawa ni kung’oa mizizi ya ufisadi—kuiondoa CCM ili kiingie chama kingine ambacho hakitakomoa wananchi wala kuhujumu afya zao na elimu ya watoto wao.

Sababu nyingine ya kuing’oa CCM ni kutokana na Mtendaji Mkuu, Yussuf Makamba kukiri wazi kwamba wagombea wote wa CCM wametoa rushwa kwa kuzidiana dau. Jamii inataka ushahidi upi zaidi ya huo?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: