CCM wanasubiri nguvu ya umma


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KATIBA ni nini, ni mali ya nani, inaandaliwaje hadi kuidhinishwa na ina mchango gani katika maisha ya kila siku ya mwananchi ni suala gumu kwa watu wengi. Hata baadhi ya wasomi hawajui.

Prince Bagenda, msomi aliyekuwa chachu ya mageuzi alipokuwa NCCR-Mageuzi, TLP, CUF kabla ya mwaka 2005, baada ya kurudi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) anaashiria kuamini katiba ni mali ya chama tawala.

Mtunzi huyu wa kitabu cha kumpigia debe Rais Jakaya Kikwete kiitwacho ‘JK: Tumaini lililorejea’ kilichochapishwa Machi 2006, anasema CCM haiwezi kuwapa wapinzani kila kitu, lazima wadai.

“Katiba ni mapambano. CCM inasema itawasikilizeni, lakini msitarajie kupewa kila kitu. Ni lazima mdai. Njooni na hoja zenu, tutazipima na kuzifanyia kazi,” anasema.

Anamaanisha kuwa wenye haki ya kufanyia marekebisho katiba iliyopo ni CCM tu; wengine watapaswa kudai na ni CCM tu wa kupima hoja za wadai kama zinafaa au hazifai.

Mtazamo wake huu ndio uliosababisha azomewe sana na kulazimika kukatisha hotuba yake kwenye kongamano la kujadili maudhui ya katiba mpya lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu hicho – UDASA – lilijadili maudhui ya muswada wa sheria uliotayarishwa na serikali kuhusu marekebisho ya katiba. Muswada ulioandaliwa chini ya hati ya dharura, unatarajiwa kuwasilishwa mkutano huu wa bunge.

Je, anaposema wapinzani lazima wadai ni kwa kiwango au kwa njia gani? Nguvu ya umma? Kama huu ndio ufahamu wa msomi huyu katika karne ya leo, ‘mbumbumbu mzungu wa reli’ vijijini watasema nini?

Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Cheyo alisema muswada ule si sheria, ni mapendekezo tu ya serikali. “Sisi wabunge tunaweza kuujadili hata kubadili kichwa kisiwe Marekebisho ya Katiba kama ilivyopendekezwa na serikali. Tumekuwa tukifanya hivyo.”

Cheyo, ambaye ni mbunge wa Bariadi Mashariki, naye hakuvumiliwa kwa kauli zake hizo. Alizomewa na kulazimika kushuka jukwaani kwenda kukaa. Kama Bagenda aliyeiwakilisha CCM, Cheyo naye hakukamilisha hotuba aliyoiandaa.

Alishushwa kwa kuonekana anadanganya watu wenye kumbukumbu mbili mbaya za serikali kukataa mapendekezo ya tume zilizowahi kuundwa kuhusu marekebisho ya katiba ya nchi.

Kwanza ilikataa baadhi ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1992 na pili Tume ya Jaji Kisanga iliyoshughulikia Waraka Na. 1 ulioletwa na serikali mwaka 1999.

Anayemlipa mpigazumari ndiye huchagua kibao cha kupigwa. Anayeandaa muswada ndiye anataja maudhui yake na hujenga nguvu kuhakikisha unapita.

Kwa hiyo, Cheyo ‘anayeshabikia CCM na rais’ hawezi kudanganya eti rais apange mambo yake halafu wabunge wayakatae. Hata uzoefu unamthibitisha Cheyo sivyo.

Pengine aliyetoa ujumbe wa moja kwa moja kwa njia ya jazba ni kijana mmoja aliyedai tatizo si CCM, bali ni wanasiasa wababaishaji.

“Wanasiasa ni wababaishaji, hapa mnazungumza mambo ya ubabaishaji, mnayoyazungumza hapa si lolote kwa shida za wananchi kule vijijini. Tatizo si katiba. Wala hawaijui. Mnazungumzia katiba wakati kule vijijini sukari inauzwa Sh. 1,800 na maharage bei juu,” alifoka.

Akasema, “Wala CCM si tatizo hapa, wanasiasa ndio wababaishaji… hawa wanasiasa wanazungumzia katiba, katiba gani? Inamsaidia nini mwananchi wa kijijini?”

Kama kijana ‘msomi’ hajui mchango wa katiba katika maisha ya kila siku ya mwananchi anafanya nini chuoni?

Hata anapozungumzia wanasiasa wababaishaji, anakusudia kulenga wanasiasa gani?

Angejua ni mwanasiasa yupi anayesababisha maisha magumu ya wananchi vijijini kati ya wale walio katika vyama vya upinzani na wanaounda serikali?

Mwanzoni mwa Machi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alifanya ziara ya wilaya za mkoa wa Kagera. Mbali na kufuta ‘sumu ya siasa’ iliyomwagwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huko alikemea na kuamuru bei ya sukari ishuke kutoka Sh. 2,200 hadi Sh. 1,700.

Nani alipandisha bei hiyo, viongozi wa upinzani au viongozi wa serikali ya CCM? Nani aliyepandisha kodi katika bidhaa hiyo – wapinzani au serikali ya CCM? Je, bei imeshuka?

Wakati Pinda akitaka wauzaji wa rejereja washushe bei hadi kufikia Sh. 1,700 kwa kilo, bei ya jumla kwa mfuko wa kilo 50 ilikuwa ni Sh. 85,000.

Muuzaji wa rejereja akiuza kwa Sh. 1,700 katika mfuko alionunua kwa Sh. 85,000 atakuwa amefanya kazi ya kurudisha mtaji wake wa Sh. 85,000. Sukari hiyo imefikaje kwenye duka lake?

Mwishoni mwa Desemba mwaka jana tulimshuhudia Rais akitoa hotuba iliyojaa machungu kwa watumiaji wa umeme na akishusha presha ya katiba mpya.

Aliwaomba wananchi wakubali maumivu ya ongezeko la gharama za umeme ambalo lilipendekezwa na TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania), lakini aliahidi pia kuanzisha mchakato wa katiba mpya.

Wiki mbili zilizopita alipotembelea Wizara ya Nishati na Madini, Rais aliitaka TANESCO ipunguze gharama za wateja kuunganishiwa umeme majumbani.

Rais amerudia kauli hiyo katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita alipogusia suala hilohilo. Pia alitangaza kuwa muswada kuhusu marekebisho ya katiba – siyo katiba mpya kama ilivyotarajiwa.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakidai kuwa rais alichukua hatua hiyo kupunguza joto kali la kisiasa lililopandishwa na CHADEMA katika maandamano makubwa yaliyofuatiwa na mikutano Kanda ya Ziwa.

CHADEMA wanashinikiza kuundwa kwa katiba mpya na waliishutumu serikali kushindwa kudhibiti mfumumo wa bei ambao ndio chimbuko la bidhaa mbalimbali za chakula kupanda holela.

Suala hilo pia limekuwa ajenda muhimu mahsusi katika mikutano ya CHADEMA ambayo itaendelea mwezi ujao kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Ajenda nyingine ni malipo ya Sh. 94 bilioni kwa kampuni ya Dowans kwa madai ilishinda kesi dhidi ya TANESCO.

Baadaye NCCR-Mageuzi na CUF walilalamikia pia gharama za maisha. Serikali ya CCM ilihamanika baada ya kelele za vyama vya upinzani.

Baada ya CCM kukwepa ajenda ya katiba mpya katika ilani yake kwa ajili ya uchaguzi uliopita, lakini sasa ikiwa ndiyo madai makuu ya wananchi wengi, serikali inataka wananchi wajimwage mitaani kupinga maudhui yaliyomo kwenye muswada uliopo?

Kwa hiyo serikali ya CCM haiwezi kujadili hoja mpaka wapinzani wadai kama anavyosema Bagenda? Kwa hiyo wananchi hawana haki ya kujadili katiba yao isipokuwa kwa hisani ya CCM?

Bila ya shaka CCM wanasubiri kupima nguvu ya umma kama Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alivyoonya pale alipotoa hotuba yake kwenye kongamano la UDASA Jumamosi.

Alisema, “Tusipopata katiba nzuri safari hii, hapana shaka miaka ijayo kuelekea 2015 kutakuwa na balaa… pakihitajika kuchimbika, pachimbike. Wananchi tushiriki kwa nguvu na wao wafungue magereza.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: