CCM wanawachukia mafisadi, si ufisadi


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

MIKUTANO ya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinatarajiwa kufanyika wakati wowote wiki hii mjini Dodoma. Kubwa linaloonekana ni mgawanyiko wa mtizamo katika kushughulikia matatizo yanayokikabili chama hicho.

Siyo siri tena, taifa hili linakabiliwa na matatizo mengi yanayotishia kuliingiza katika mitafaruku ya kijamii. Kukosekana kwa nishati ya umeme, kuporomoka kwa thamani ya shilingi, kuongezeka kwa deni la ndani lisiloweza kulipika, na kupanuka kwa nyufa katika serikali na chama chenyewe ni baadhi ya matatizo hatarishi ya amani yetu.

Mtindo wa sasa wa serikali “kufukia shimo moja kwa kuchimba jingine” hauna tija na ni sawa na kuhamishia matatizo chumbani kutoka sebuleni wakati nyumba ni ile ile.

Pamoja na makundi kadhaa yaliyomo ndani ya CCM, liko kundi linalodai ufisadi ndilo tatizo kuu na kwa hiyo dhana ya kujivua gamba ndiyo dawa pekee ya kukinusuru chama hiki.

Kwamba, mafisadi wafukuzwe ndani ya chama na hilo litaleta umeme, litapandisha thamani ya shilingi, litalipa madeni ya walimu na wafanyakazi wengine, na tendo hilo litamaliza nyufa za muungano na makundi ndani ya chama.

Kundi hili linaloaminika kuwa chini ya uongozi wa Samwel Sitta halisemi kwa uwazi ikiwa kuwafukuza mafisadi bila kuondoa ufisadi ndani ya CCM, kama kutaweza kusaidia jambo la maana.

Hii ni kwa sababu haiwezekani kuwa ndani ya chama hiki kuna mafisadi watatu tu, Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge; Sitta alikuwa miongoni mwa wanamtandao uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani. Tuliokuwapo tunadhani Sitta anaweza kuwa anawachukia mafisadi bila kuuchukia ufisadi.

Kundi la pili linaona hali tete ya nchi imesababishwa na baadhi ya watendaji wa chama na ndani ya serikali ambao wamekisaliti chama na kuidhoofisha serikali mbele ya umma. Watu hawa wamediriki hata kujaribu kusajiri chama kipya – Chama cha Jamii (CCJ). Kwa njia hiyo, hawa wameitelekeza dhamana ya CCM iliyowaweka madarakani.

Kwa ujumla wao, viongozi hawa wanalalamikiwa na mahasimu wao kuwa hatua walizozichukua kwa kisingizio cha kutetea maslahi ya nchi, zimekidhalilisha chama na serikali mbele ya umma.

Hata sasa, wanaendelea kutuhumiwa kukigawa chama. Hawataki ule msingi wa uwajibikaji wa pamoja na wala hawakusudii tena kuurejea katika maisha yao ya utumishi.

Kwa msingi huo, kundi hili la pili linadai watendaji hawa wafukuzwe ndani ya chama na kuwa hatua hii itarejesha umeme, itapandisha thamani ya shilingi, italipa madeni ya ndani na kuziba nyufa za ndani ya chama na serikali na kumaliza makundi hatarishi.

Nimeongea na vinara wa makundi yote mawili. Kundi la Lowassa linaeleza wazi jitihada za kupatana na kundi la Sitta zimeshindikana. Kwa maoni ya kundi la Lowassa, Sitta hayuko tayari kwa suluhu pungufu ya yeye kuwa waziri mkuu au rais wa nchi.

Maoni haya ya kukata tamaa kutoka kundi la Lowassa yanaashiria jambo moja la msingi, Sitta na kundi lake siyo tatizo tena kwa kundi la Lowassa, bali ni tatizo kwa taifa. Kwa maneno mengine, unahitajika ujasiri wa kiuongozi kumaliza madhara yanayosababishwa na kundi la Sitta kwa kuzidi kukigawa chama na serikali.

Nalo kundi la Sitta ambalo kimsingi na kwa dhati linasema kuwa tatizo la nchi ni mafisadi; linakiri wazi kuwa kuna tatizo la uongozi katika taifa, vinginevyo hawa mafisadi wasingeweza kuyumbisha nchi kiasi hiki. Ili kutatua tatizo la uongozi, waliona ni vema kusajiri chama kingine ambacho kingechukua nafasi ya CCM katika kuwashughulikia mafisadi.

Sitta na wenzake wanakiri wazi kuwa kasi ya kuwashughulikia mafisadi ni ndogo sana na wakati mwingine inakatisha tamaa na kuhatarisha hatima yao kisiasa. Hata baada ya kutoa ushauri kwa chama tawala na viongozi wakuu, akina Sitta wanadai kilio chao hakijasikilizwa.

Ukisikiliza pande hizi mbili unashawishika na pengine kuamini kuwa tatizo linalokikabili CCM ni uongozi na wala si ufisadi ama usaliti wa kuanzisha chama. Hii ni kwa sababu waliofanya ufisadi ni makada waandamizi; walifanya hivyo mchana kweupe na wakati mwingine kwa ridhaa ya viongozi wakuu wa chama.

Sehemu kubwa ya ufisadi wao, ndiyo uliyokiwezesha chama kupata ushindi wa kishindo na hata kuwaweka madarakani baadhi ya viongozi hao. Wakati wote huo, ufisadi haukuwa tatizo kwa taifa wala CCM!

Mabadiliko ya sasa yanayosikika midomoni mwa viongozi hao kuhusu ufisadi, hayatokani na mabadiliko ya mioyo yao, bali ni kukosa msimamo na ujasiri wa kiuongozi. Tatizo si ufisadi wala mafisadi, bali ni ombwe la kiuongozi.

Hali kadhalika, usaliti uliofanywa na makada na watendaji wa serikali dhidi ya CCM, ulifanyika huku viongozi wakuu wakiuangalia. Vyombo vya dola ikiwamo idara ya usalama wa taifa vilitoa taarifa kwa viongozi wakuu wa CCM na serikali yake na hata kukabidhi rasimu ya katiba na nyaraka nyingine nyeti za CCJ. Hakuna hatua iliyochukuliwa.

Kushindwa huko kuchukulia hatua waasisi wa CCJ, kumesababisha wana CCM wengi walioaminishwa kuwa nyuma yake kulikuwa na vigogo wa chama hicho waliochoshwa na ombwe la uongozi lililopo ndani ya chama na serikali, kukosa imani na chama chao.

Kwa njia hii, CCJ ikapata umaarufu bila kusajiliwa huku CCM ikiporomoka kila uchao. Kwa maoni yangu, ushindi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hautokani na uzuri wa chama hicho, bali udhaifu wa CCM uliosababishwa kwa sehemu kubwa na ombwe la uongozi lililohubiriwa kwa muda mrefu na viongozi wa CCJ.

Mpaka hapa ni sahihi kusema, usaliti wa watendaji na makada wa CCM waliohamia CCJ kimya kimya huku wakishikilia nyadhifa zao ndani ya CCM, si jambo kubwa kuliko udhaifu wa kiuongozi ulioshindwa kuwashughulikia wakati huo na na hadi sasa. Hii inamaanisha si usaliti unaokimaliza CCM, bali udhaifu wa uongozi ndio chanzo cha makundi, usaliti na ufisadi.

Vikao vya CCM vitafanya makosa makubwa vikikimbilia kuona ufisadi na usaliti ndiyo agenda kuu ya kushughulikia. Kwangu mimi, ufisadi na usaliti ni dalili za ombwe la uongozi, yaani kukosa ujasiri na kusingizia kutumia hekima.

Uongozi huu umejaa woga na kusingizia utawala wa sheria. Ni uongozi unaowaheshimu sana mafisadi na kuwaogopa wasaliti wa chama. Ni uongozi unaotetemeka mbele ya uovu badala ya kuufanya uovu utetemeke mbele ya uongozi.

Tumeona wenyewe wiki iliyopita, kiongozi mkuu wa shughuli za serikali ndani ya serikali akilia mbele wa wabunge na kudai hana mamlaka yoyote ya kumwajibisha katibu mkuu wa wizara anayetuhumiwa kwa rushwa.

Kana kwamba hiyo haitoshi, hata mkuu wa nchi aliyedaiwa ana mamlaka juu ya mtendaji huyo, akaishia kumgwaya na kumpa nafasi ya kupumzika kwa muda baada ya kazi nzuri na ngumu aliyoifanya.

Inasikitisha sana kuona rais anasita kumfukuza katibu mkuu anayetuhumiwa kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara yake. Kweli chama legelege, huzaa serikali legelege.

tutikondo@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: