CCM wasome, wajadili ripoti ya ufisadi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

RAIS Jakaya Kikwete ameruhusu ripoti ya tathmini ya hali ya rushwa nchini, ambayo ilikuwa inasuasua katika kumbi za wenye madaraka, itolewe kwa wananchi waione na kuijadili hata kama Baraza la Mawaziri bado halijapata nafasi ya kuipitia na kuijadili.

Taarifa hiyo ilitolewa katika mkutano wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wafadhili ambapo aliwahakikishia kuwa ripoti hiyo itatolewa kwa wananchi.

Taarifa kuwa ripoti hiyo ya “ufisadi” ambayo kwa uhakika ni kuhusu rushwa zaidi imepokewa na watu mbalimbali kwa furaha huku wengine wakiamini katika uthubutu wa Rais Kikwete kuonesha uongozi. Hivyo kwa watu wenye moyo, taarifa hizi zimewasisimua na nina uhakika wapo ambao wataanza kuimba nyimbo za kusifia uamuzi huu huku wengine wakisubiri kwa hamu kuisoma ripoti hiyo.

Baada ya kutafakari  nimepata pendekezo moja kubwa kwamba ripoti hii isomwe na wana CCM wote kuanzia mjumbe wa shina hadi kiongozi mkuu wa CCM. Hii si ripoti ambayo Watanzania wote wanahitaji kuisoma au hata kuijadili kuhusu hali ya rushwa nchini kwani kwa Watanzania wengi hali ya rushwa haihitaji ripoti nyingine kuelezea hali ilivyo.

Ripoti hii, kama tunavyojua, inahusu hali ya rushwa ilivyokuwa hadi mwaka 2009. Serikali iliridhia mwezi Juni 2007 (wakati wa kilele cha tuhuma za ufisadi) kufanya tathmini ya hali ya rushwa nchini. Lengo la kufanya tathmini hiyo ilitokana na uamuzi kuwa serikali  kuchukua msimamo wa “uvumilivu sifuri” (zero tolerance)  wa vitendo vya rushwa.

Msimamo huu  tunaambiwa na waraka wa Ofisi ya Rais Kitengo cha Utawala Bora kuwa ulianza mara baada ya ripoti ya Jaji Joseph Warioba ya 1996 ambayo kama wengi wanavyokumbuka iliweka wazi hali mbaya ya utawala bora nchini.

Ni katika mkakati wa kupambana na rushwa ndipo serikali ikaamua, kati ya mambo mengine, kufanya tathmini ikiamini kwamba matokeo ya utafiti huo “yatasaidia katika mkakati dhidi ya rushwa”.

Lengo la tathmini hiyo ni kufanya iwe kama chombo ambacho kinaweza kutumika mara kwa mara kuangalia hali ya rushwa nchini na kuchukua mapendekezo yake ya hali ya rushwa katika wizara, taasisi na idara mbalimbali za serikali, mikoani na wilayani, hivyo kuweza kuyatumia matokeo hayo katika kusaidia kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya rushwa nchini.

Hivyo, ripoti hii ambayo imepita miaka minne tangu iidhinishwe inatarajiwa kutupatia mwanga kuwa ni maeneo gani yana tatizo kubwa la rushwa, linatokea vipi hasa na mianya inayosababisha, na mapendekezo ya nini kifanyike.

Sasa, ripoti ya namna hii ni muhimu kwa watu ambao hawajui kina cha rushwa nchini au wale ambao kwa miaka hii mitano hivi, hawajawahi kutusoma au kufuatilia malalamiko yetu juu ya ufisadi.

Nimegundua kuwa watu pekee ambao hawajaamini maneno yetu na ambao hawajui kina cha tatizo la rushwa (ambayo ni sehemu moja tu ya ufisadi) ni wana CCM na wale ambao kwa asilimia 60 walienda na kuirudisha serikali ile ile madarakani kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Watanzania wengine hawahitaji kushawishiwa kujua kina cha tatizo.

Ni wana CCM ambao hawaamini kuwa Meremeta ni kampuni ambayo wamiliki wake na wahusika wake wote walitakiwa wawe jela, siku nyingi, wakitumikia vifungo vya maisha na si chini ya hapo. Watanzania wengine waliofuatilia suala hili hawahitaji kuambiwa Meremeta ni nini na iliingiaje nchini hadi kuweza kuhusishwa na ufisadi wa hali ya juu kabisa kutokea nchini. Hili wanahitaji kushawishiwa wana CCM.

Ni wana CCM ambao hawaamini kuwa kampuni ya Kagoda iliundwa kwa ajili ya kufanya ufisadi na kufanikisha kundi la watu wachache wanaohusiana na chama hicho tawala. Suala zima la EPA limetokea chini ya viongozi wa serikali ya CCM na ni wao pekee wanajua nini kilifanyika na ndio wao walishindwa kuwajibishana ilipotokea na wakawaacha wahusika wengine wakiendelea kupeta licha ya sera yao rasmi ya “uvumilivu sifuri”! Hili wanahitaji kushawishiwa wana CCM siyo sisi wengine.

Ni wana CCM wanaohitaji kushawishiwa kuamini kuwa tunapoteza karibu asilimia 30 ya fedha za bajeti yetu kila mwaka (maneno ya Rais Kikwete) kwa vitendo vya ufisadi. Kwamba katika kila shilingi 100 ambayo tunaitenga kwa ajili ya bajeti yetu ya mwaka, shilingi 30 zinachotwa na wajanja.

 Shilingi hizi thelathini ni sawa na shilingi 300 katika kila 1000, Sh. 3000 katika kila 10000, Sh. 30,000 katika kila 100,000, Sh. 300,000 katika kila 1,000,000. Kwenye bajeti ya shilingi trilioni 11, shilingi trilioni 3.3 inaishia mikononi mwa wajanja! Ni wana CCM tu wanaohitaji ripoti ya kuwashawishi ubaya wa hilo.

Sihitaji ripoti kujua ubaya na ukali wa ufisadi nchini ikiwemo vitendo vya rushwa. Kwa hakika inashangaza kabisa kuwa kuna watu wanahitaji ripoti “nyingine” ili wajue ubaya wa tatizo la ufisadi nchini.

Sihitaji kuaminishwa kuwa tatizo la rushwa ndilo pekee linalowakera wananchi – maana wapo wana CCM wanaofikiri kuwa tunapozungumzia “ufisadi” tunazungumzia “rushwa” tu na kwa hiyo tukikamata wala rushwa basi tumewakamata mafisadi wote!

Hivyo ripoti mpya juu ya rushwa nchini haitabadilisha mitazamo ya watu wengi kwani yote ambayo yatasemwa tayari yanajulikana na yameshatajwa kwenye ripoti mbalimbali.

Mashirika na taasisi mbalimbali nchini yameshafanya utafiti wa kutosha sana kuhusu hali ya vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya raslimali zetu. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inatosha kabisa kutuonesha tatizo la ufisadi nchini lilivyo lakini hadi leo imekuwa ni ripoti ya kukabidhiana kwa mbwembwe na kutuambia mambo ambayo tuliambiwa mwaka uliopita.

Ripoti za mashirika kama Transparency International na hata ripoti za ndani zinatujuza vya kutosha tu kina cha vitendo vya ufisadi nchini. Sasa tunataka ripoti nyingine tujue zaidi? Ili tukasirike zaidi?

Hivyo basi, wazo la ripoti hii kuwekwa wazi ni zuri lakini naamini wanaotakiwa kuisoma kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, kuanzia neno la kwanza hadi la mwisho na wairudie rudie na kuijadili kwenye vikao mbalimbali ni wana CCM na mashabiki wao na hasa waliojitokeza kwenda kuwarudisha madarakani viongozi wale wale, wenye sera zile zile na mtazamo ule ule ilhali walikuwa na nafasi ya kubadilisha uongozi uliopo ili tuanze upya kulijenga taifa letu.

Binafsi siihitaji, siitaki, siingojei na wala sina mpango wa kuisoma kwani hakuna chochote kilichomo ambacho hatukijui na hakuna mapendekezo ndani yake ambayo hatujayatoa huko nyuma. Habari kwa ufupi.

Niandikie: Mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: