CCM watabana demokrasia hadi lini?


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version

DEMOKRASIA ya vyama vingi hapa Tanzania bado inachechemea, ikilinganishwa na nchi nyingine katika eneo hili la Afrika.

Nchi zinazozungumziwa hapa ni zile zilizokuwa chini ya utawaliwa wa Uingereza, yaani Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Zimbabwe. Karibu miongo miwili sasa tangu nchi hizi, ikiwemo Tanzania, zikumbatie mfumo wa siasa za vyama vingi, bado kuna mapungufu kadhaa.

Kwa mfano, uwiano wa uwakilishi wa vyama ndani ya mabunge, baina ya vyama vya upinzani na vyama tawala utaona kwamba karibu nchi zote zilizotajwa uwiano umekuwa karibu nusu kwa nusu (50:50).

Ni Tanzania pekee ndiyo siku zote ilikuwa, na bado inayo tofauti kubwa ya uwiano baina ya pande mbili za uwakilishi katika Bunge lake.

Angalau, baada ya uchaguzi wa mwaka huu wabunge wa upinzani wanakaribia theluthi moja ya wabunge wote. Katika chaguzi za nyuma wapinzani walikuwa hawazidi robo ya wabunge wote.

Hata hivyo, kuwa na theluthi moja tu ya wabunge wa upinzani bado haitoshi katika kuchochea demokrasia halisi nchini hasa ikizingatiwa uwezekano wa upinzani wenyewe kugawanyika au kugawanywa.

Swali hapa na ambalo ndiyo mada kuu ya leo, ni kwa nini demokrasia ya Tanzania iko katika hali hii – yaani iko nyuma, siyo changamfu ikilinganishwa na nchi zilizotajwa hapo juu?

Jibu rahisi ni kwamba chama tawala – CCM – hakitaki, wala kuonyesha dalili zozote za kuwa tayari kuleta mabadiliko yoyote ya kisiasa nchini.

Kwa bahati mbaya, maneno ‘mabadiliko ya kisiasa’ yamekuwa yanatafsiriwa vibaya na watu wengi kwamba ni kukibadilisha chama kinachotawala na kuweka kingine.

Mabadiliko ya kisiasa ni kubadili mfumo mzima wa kisiasa ambao umepitwa na wakati kutokana na hali halisi inayokuwapo nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kweli katika fani mbali mbali.

Inaweza kuletwa na chama kilichopo madarakani kwa hiari na makusudi mazima iwapo kina nia njema na mustakabali wa nchi.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge jipya wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete anayeingia muhula wake wa pili hakugusia kabisa suala la kuwepo mchakato wa kuleta katiba mpya licha ya kelele nyingi za wapinzani na wanaharakati wengi.

Kikwete anafumbia macho huku akijua amechaguliwa na asilimia 61 ya waliokwenda vituoni kupiga kura, ambao idadi yao ilikuwa asilimia 42 ya wapiga kura wote walioandikishwa. Na hii asilimia 42 ni kama nusu tu ya Watanzania wote.

Kikwete na wapambe wake hawataki kusikia vilio vya kuwepo katiba mpya, kwa sababu kwa mtazamo wao katiba ya sasa inatosheleza kuendelea kwao kuwapo madarakani milele na milele.

Lakini hali halisi inayojitokeza ni kwamba hata hii katiba wanayoing’ang’ania polepole inaanza kuwaathiri wao wenyewe.

Hawataki kuamini kwamba kwa manufaa yao, pia, ni bora waanze mchakato wa kuleta mabadiliko ya katiba kuliko yaje kwa kupitia michakato au njia nyingine. Gharama ya njia nyingine ni kubwa kama waliyopata Kenya kutokana na ucheleweshaji wa kuleta katiba mpya.

Viongozi wa CCM hawataki kukubali kuwa mabadiliko ni lazima yatakuja, watake wasitake, na kinachofanyika ni kujaribu kuyachelewesha tu, kitu ambacho ni hatari zaidi.

Imefikia mahala ambapo nchi zinashindwa kujikwamua kutoka kwenye umaskini kutokana na viongozi au vyama vyao vilivyopo kuendeleza uhafidhina, kuhodhi madaraka na kutumia kila mbinu kubakia madarakani katika mifumo ya kisiasa ambayo haitoi fursa kwa watu na makundi mengine yenye mawazo tofauti kuibuka.

Katika mdahalo kupitia TV uliofanyika siku chache kabla ya uchaguzi mwezi uliopita, Kikwete aliulizwa swali kwamba baada ya kumaliza muda wake, angependa Watanzania wamkumbuke kwa lipi. Alishindwa kujibu kwa kujiamini na kwa ufasaha kwa sababu anatambua hana cha maana cha kukumbukwa. Angekuwa na nia njema na nchi hii ili akumbukwe, angeweza kujibu hivi: “Nataka nikumbukwe kwa kuleta katiba mpya.” Au haidhuru, “nataka nikumbukwe kwa kuanzisha mchakato wa kuleta katiba mpya.”

Bahati mbaya Kikwete hana ujasiri wala uthubutu wa kushinikiza chama chake kutoa maamuzi mazuri kama haya kwa sababu tu yanaweza kuathiri masilahi ya kiuchumi ya kikundi cha watu wachache sana wenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kifedha ndani ya chama hicho.

Hali hii inajitokeza pamoja na kwamba CCM, yenyewe kama chama au serikali yake, inatumia kila njia, mbinu, gharama zozote za kifedha, kila aina ya ubabe na vitisho katika kuvifinya vyama vya upinzani, na ikiwezekana kuona vinatokomea mbali ili kubaki chenyewe peke yake.

Vyama vya upinzani na wanaharakati wanaopigania demokrasia wamejikuta wanakosa hata pa kukimbilia kwani hata mahakamani mbinu hutumika kuvinyima haki.

Mathalani katika kesi ya mgombea binafsi serikali ilipiga danadana katika rufaa yake katika Mahakama ya Rufaa na hukumu yenyewe ilivyopatikana imekosolewa na wasomi mbali mbali.

Aidha kuna watu ndani ya uongozi wa chama hicho wanaoongozwa zaidi na ushabiki wa kisiasa kuliko hoja, ubabe na kukomoana kuliko busara. Mmojawapo ni Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Chiligati.

Nitatoa mfano. Baada ya kutambua wingi wa wabunge wa chama chake Chiligati aliamua kujenga hoja kwamba watumie wingi huo kupitisha azimio la kuwafukuza wabunge wa CHADEMA kwa kitendo chao cha kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge mara tu Rais Kikwete alipoanza kutoa hotuba yake ya ufunguzi.

Aliviambia vyombo vya habari kwamba chama chake kinatafuta namna ya kuiadabisha CHADEMA kwa kitendo hicho ikiwemo kutoa azimio Bungeni kuwafukuza wabunge wa CHADEMA.

Kada huyo wa CCM hakufafanua azimio kama hilo litapitishwa chini ya kifungu gani cha Katiba au kanuni ipi ya Bunge. Inawezekana yeye na wenzake wanaangalia kupitia darubini kali zenye uwezo wa kutafuta vipengele vya sheria au kanuni ili kuifuta CHADEMA.

Mara nyingi CCM wamekuwa wanautumia ukubwa wa uwakilishi wao bungeni kwa mambo ya hovyo hovyo tu, mambo yasiyokuwa na masilahi kwa taifa kwa sababu ya ushabiki mkubwa. Ni kama vile wamekuwa wanashindwa kutumia amani iliyopo nchini kama fursa nzuri ya kuendeleza nchi.

Mbunge wa CCM akisimama na kutoa hoja ya kusema “hakuna ufisadi kabisa ndani ya CCM na serikali yake, hayo ni mambo ya magazetini tu” itaungwa mkono na wabunge wengi kwa kelele na makofi. Lakini mbunge akilaani ufisadi uliomo ndani ya CCM atashughulikiwa.

Laiti wingi wa uwakilishi wa CCM bungeni ungekuwa unatumiwa katika jitihada za kuwabaini wezi wa kampuni ya Kagoda, Deep Green na nyinginezo na kushinikiza kufikishwa kwao mahakamani, serikali ingejirudishia imani yake kwa wananchi katika masuala la maadili na uwajibikaji.

Badala yake wanatafuta kila uwezekano wa kuwafukuza wabunge wa CHADEMA kuliko kuwachukulia hatua za kisheria wezi wa fedha za umma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: