CCM watoana roho kwa urais


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 June 2011

Printer-friendly version
Benard Membe, Waziri wa Mambo  ya nje na Ushirikiano wa kimataifa

RAIS Jakaya Kikwete ameendelea kukaa kimya huku viongozi wake wakianza “kutoana roho” kwa urais wa 2015, MwanaHALISI limeelezwa.

Benard Membe, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, anaparurana na waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa wakati January Makamba, mwenyekiti wa kamati ya nishati ya bunge, anamparura Membe.

Huyu anamtuhumu yule “kumchafua” na yule anamtuhumu huyu “kumchimba” na kumzushia tuhuma; huku Rais Kikwete akiendelea kukaa kimya kama asiyesikia au aliyebariki minyukano hiyo.

Kwa miezi mitatu sasa, kumekuwa na tuhuma kwa njia ya piga nikupige zikihusisha wanaojitaja na hata kutajwa kuwa wanataka kugombea urais mwaka 2015.

Jumatatu iliyopita, Membe alinukuliwa na gazeti la kila siku la Mtanzania akimtuhumu Lowassa kuwa ndiye anamchafua kwa kutumia baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja.

Hatua ya Membe kutuhumu Lowassa ilikuja siku moja baada ya gazeti kuripoti kuwa anahusika katika njama za “kuchota mabilioni ya shilingi” kutoka serikali ya Libya uliopangwa kufanywa na kampuni ya MEIS Industries ya jijini Dar es Salaam.

Lakini kutuhumiwa kwa Makamba kunatokana na taarifa za mtandao, moja kwa moja kutoka Canada, kwamba amepokea mlungula wa dola 2 milioni (sana na Sh.  3 bilioni) ili kukingia kifua kampuni ya kuchimba madini ya African Barrick inayotuhumiwa kusababisha vifo vya watu saba kwenye mgodi wa Nyamongo, mkoani Mara.

Makamba amenukuliwa katika vyomvo vya habari Jumatatu akisema anayemchafua ni mwanasiasa mmoja aliyeondolewa kwenye sekretarieti ya CCM na ambaye nafasi yake ameishika yeye. Hakumtaja jina; lakini kama ni aliyemrithi, basi ni Membe.

Kuibuka kwa minyukano ya sasa kumekuja baada ya kipindi kirefu cha kubwatukiana baina ya Samwel Sitta, waziri wa Afrika Mashariki na kambi ya akina Rostam Aziz, Edward Lowassa na Andrew Chenge.

Pamoja na kuadhiriwa kwa kuitwa na chama chao kuwa ni mafisadi, Lowassa, Rostam na Chenge wameendelea kushikilia kuwa wana “hadhi na sifa” za kugombea urais, hasa kwa kutaka kumweka mbele Lowassa kama mgombea wao.

Dhamira ya Lowassa ya kutaka kugombea urais ilidhihirika upya pale makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa aliporipotiwa akimwambia kuwa “aachane na urais;” na Lowassa akamjibu, “kwani ni makosa kugombea urais?”

MwanaHALISI liliripoti mahojiano hayo katika toleo lake la Juni 1 hadi 7, likinukuu vyanzo vya habari vilivyoshuhudia majibizano kati ya Msekwa na watuhumiwa hao watatu ambao CCM imeita mafisadi na kujiapiza kuwatosa.

Wakati hao wakinyukana kwa ama kupakaziana, kutuhumiana au kukashifiana, washindani wa tangu mwaka 2005 bado wananyemelea kiti cha urais. Hao ni pamoja na Profesa Mark Mwandosya, Frederick Sumaye na Dk. Abdallah Kigoda.

Haijafahamika iwapo Dk, Salim Ahmed Salim bado ana nia ya kugombea urais, hasa baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kupakaziwa na mtandao wa Kikwete mwaka 2005 kuwa alishiriki mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume.

Kutajwa kwa minyukano kati ya Membe na Lowassa kunafuatia tuhuma za kuhusika kwa Membe katika njama za kugombea kitita cha dola za Marekani 34 milioni (karibu Sh. 55 bilioni) za serikali ya Libya.

Gazeti hili liliripoti wiki iliyopita kuwa kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) na mtu mmoja, Massoud Mohamed Nasir aliyejiita raia wa Libya, wamekubaliana kugawana sehemu ya dola 121.9 milioni (Sh. 180 bilioni) ambazo zinatajwa kuwa deni sugu la Tanzania kwa serikali ya Libya.

Sasa kuna tuhuma kwamba naye Membe yumo katika mpango huo kwani anataka kutumia fedha hizo kuwapa kampuni ya MEIS Industries ili kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha saruji mkoani Lindi.

Kutokana na mkorogano huu, wakili wa MeTL, Dk. Masumbuko Lamwai, amemwandikia balozi wa Libya ajiandae kuwajibika iwapo fedha hizo zitalipwa kwa kampuni ya MEIS.

Lowassa na Membe ni miongoni mwa wanachama wa mtandao waliofanya kazi kubwa ya kumuingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005, lakini kwa sasa hawapikiki tena chungu kimoja.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa MwanaHALISI uhusiano kati ya Lowassa na Membe ulianza kuwa mbaya mara baada ya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005.

Lowassa anadaiwa kushinikiza Kikwete kumfanya Membe naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi katika baraza lake la kwanza la mawaziri aliloliunda baada ya kutangazwa mshindi wa urais, Desemba 2005.

Hata hivyo, Lowassa alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za kumchafua Membe, haraka alijibu, “Sifahamu lolote juu ya kinachoelezwa kwa kuwa sijasoma gazeti hilo. Mimi niko kijijini kwangu Monduli…”

Membe hakupatikana kueleza kwa undani kinachodaiwa na gazeti hilo kuwa ni njama za Lowassa. Bali kiongozi mmoja wa juu serikalini ambaye yuko karibu naye ameeleza kuwa mwanasiasa huyo amepanga kukutana na waandishi wa habari mara atakaporejea nchini ili kufafanua kinachoitwa, ‘Tuhuma dhidi yake.”

Gazeti hili limeelezwa na kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM, kuwa kiini cha migogoro, minyukano na mifarakano isiyoisha ndani ya chama hicho, ni Rais  Kikwete na mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.

Kikwete anatuhumiwa na baadhi ya wanachama wenzake ndani ya chama, kwa  kunyamazia minyukano inayoendelea kwa kuwa inamuimarisha kisiasa kutokana na staili yake ya “wagawe uwatawale.”

“Hata haya ya sasa ya kuwafukuza Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge yana baraka za Kikwete. Yeye ndiye aliyewasuka Membe na wenzake katika kujenga hoja ya kuwafukuza wenzake ndani ya Kamati Kuu (CC) na NEC. Lakini dili lilipoiva la kuwaondoa Rostam na Chenge kwenye CC, Kikwete akamtosa Membe kwenye CC,” anaeleza mbunge mmoja wa chama hicho. 

Anasema, “Ngoja nikuambie, hii mifarakano ndani ya CCM haitaisha kwa kuwa yote haya yanasababishwa na Kikwete mwenyewe. Hawa wote, Membe, Samwel Sitta, Rostam na Lowassa, ni watu wa JK (Jakaya Kikwete). Hapa ndipo lilipo tatizo la msingi.”

Naye rais mstaafu Mkapa anatuhumiwa kwa hatua yake ya kupindisha kanuni za uchaguzi ndani ya chama chake mwaka 2005 wakati wa kutafuta mgombea urais.

Alipindisha utaratibu na kuamuru kila mjumbe kupiga kura moja badala ya tatu kwa wagombea watano waliopitishwa na chama, hatua iliyolenga kumbeba Kikwete.

“Waliomshauri Mkapa amuunge mkono Kikwete, walikuwa ni Membe, Rostam na Apson Mwang’onda ambaye alikuwa mkurugenzi wa usalama wa taifa. Hili lilifanyika baada ya kuwapo kwa tishio la kutokea mpasuko ndani ya chama, iwapo Kikwete angekataliwa,” vinaeleza vyanzo vya taarifa.

Uswahiba kati ya vigogo hao – Lowassa, Rostam, Membe, Abdurahman Kinana na Sitta – ambao sasa wameanza kutoa macho ulianza mara baada ya Mkapa kushinda kiti cha urais.

Mkutano wa kwanza wa kupanga mkakati wa kuelekea ikulu mwaka 2005 ulifanyika nyumbani kwa Sitta, Kinondoni Dar es Salaam.

Ni ndani ya mkutano huo, ndiko mkakati wa kushughulikia wote wanaotajwa katika mbio za urais za mwaka 2005 ulipangwa na kutekelezwa. Mbali na Kikwete, wengine waliohudhuria kikao hicho, walikuwa ni Sitta, Lowassa, Rostam na Anne Makinda.

“Pale ndipo safari ya Kikwete ilipoanzia. Wale wote walionekana kutafuta urais wakaanza kushughulikiwa. Watu kama Dk. Hassy Kitine, Salim Ahmed Salim, Fredrick Sumaye, Profesa Mark Mwandosya, Iddi Simba na wengineo, ambao ama walitajwa au walisikika wakisema watagombea urais baada ya Mkapa, walianza kusakamwa kwa tuhuma, mmoja baada ya mwingine,” ameeleza mtoa taarifa wetu.

0
Your rating: None Average: 4.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: