CCM yahonga maaskofu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

KATIKA kampeni za uchaguzi mdogo jimboni Arumeru Mashariki, imebainika kuwa tabia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuuza na kununua uongozi, imevuka mipaka.  Safari hii imeingia mahali patakatifu pa watakatifu, yaani mahekaluni. 

Ofisa mmoja wa kampeni wa CCM ambaye amedaiwa kubeba mfuko wa fedha za kampeni akizunguka nao mitaani, alitinga katika ofisi kuu za dayosisi ya KKKT-Meru na kumwaga Sh. 2.5 milioni kwa kisingizio cha kukarimu mkutano wa wachungaji na watumishi uliokuwa unaendelea hapo.

Baada ya kujitambulisha kuwa yeye ni Mlutheri na kuwa ana zawadi za kalenda kutoka kwa Askofu, zikiwa na picha ya Askofu huyo pamoja na Rais Jakaya Kikwete, ofisa alimwaga mezani fedha na kutamka kuwa hicho ni chakula cha mchana kwa maaskofu.

Taarifa zinasema Askofu Paulo Akyoo wa KKKT Dayosisi ya Meru alionekana kukubaliana na “bahasha” hiyo, lakini baadhi ya wachungaji walipinga vikali kitendo hicho.

Ziara ya ofisa huyo mwenye “bulungutu” haikuishia hapo. Aliwaita wachungaji wa Kanisa la Pentekoste na kukutana nao katika hoteli ya Gateway, Usa-River na kuwabembeleza wakipigie kampeni chama chake.

CCM imemsimamisha Sioyi Sumari kugombea ubunge katika uchaguzi huo mdogo wa kujaza kiti kilichoachwa wazi baada ya mbunge wake, Jeremiah Sumari, kufariki dunia.

Alidai katika mkutano huo kuwa hali ya chama chake ni mbaya; tayari wametubu na kuahidi kujirekebisha.

Ofisa huyo anadaiwa kutoa Sh. 20,000 kwa kila mchungaji aliyekuwa kwenye mkutano huo.

Aidha, viongozi saba na wachungaji hao walilipwa kiasi cha Sh. 100,000 kila mmoja kama nauli katika mkutano ambao haukuandaliwa na CCM.

Wachungaji hao wa Pentekoste na viongozi wao, wamelaani kitendo hicho cha ofisa wa CCM kuhonga viongozi wa dini na kudai kwamba hiyo ni “tabia chafu iliyopitiliza.”

Mmoja wao amesema, “huku ni kunajisi mahali patakatifu kwa watakatifu.”

Askofu Akyoo alipopigiwa simu kuulizwa kuhusu tukio hilo, alisema atapiga kwa mwandishi baadaye. Akakata simu.

Hakupiga simu, na alipopigiwa tena baadaye, simu yake ilibaki kuita bila ya kupokelewa. Hata alipoandikiwa ujumbe wa simu, hakujibu.

Gazeti hili lilimtafuta meneja wa kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba ili ataje ni kiongozi gani alikuwa anagawa fedha katika kampeni ambazo anasimamia, lakini simu yake haikupokewa.

Alipoendelea kutafutwa mara kadhaa baadaye, simu yake ilionyesha kuzimwa.

Mwishoni mwa wiki, Nchemba alipobanwa kuwa anahonga fedha, alikaririwa akijibu kuwa yeye hana fedha za kugawa ili kutafuta kura, na kwamba kama angekuwa nazo angezipeleka jimboni kwake Iramba Magharibi, mkoani Singida.

Jitihada hizo za CCM kuhonga viongozi wa dini zimekwenda sambamba na jitihada nyingine za chini kwa chini zinazofanywa na Edward Lowassa, Mbunge wa Monduli.

Lowassa ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa waziri mkuu kutokana na tuhuma za upendeleo kwenye mkataba tata wa Richmond, Februari 2008, yuko Arumeru kumpigia kampeni mkwewe, Sioyi Sumari.

Taarifa zinasema kwa wiki nzima sasa, Lowassa amekuwa akituma ujumbe kwa viongozi wa dini na kuwatembelea wengine ofisini kwao ili kuwasihi wamuunge mkono Sioyi.

Mara kadhaa Lowassa ameonekana maeneo ya Mererani, Mbuguni na Usa River katika ofisi za dayosisi ya KKKT.

Wakati hayo yakitokea, taarifa zinasema CCM kimepanga kupora ushindi endapo itadhihirika kuwa wananchi wamelalia upande wa CHADEMA.

Chama ambacho kimeonyesha ushindani mkubwa katika uchaguzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinachompigia kampeni Joshua Nasari.

Njama zinaratibiwa kwa karibu na kikosi maalum kinachohusisha baadhi ya polisi, maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na maofisa wa idara ya usalama wa taifa.

Mkakati wa awali wa wizi tayari umevuja baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kudai hadharani kuwa kuna vituo 55 vya bandia vilivyoundwa maalum kwa ajili ya kuingizia kura hewa.

Kuvuja kwa mpango huo, mtoa taarifa anasema, ndiko kulikosababisha NEC kutaka kujisafisha kwa kudai kuwa imegundua baadhi ya kasoro hizo na kwamba itazifanyia kazi.

Aidha, NEC imegoma kubandika majina ya wapigakura siku saba kabla ya uchaguzi kama sheria inavyoelekeza; badala yake viongozi wa tume wamesema zoezi hilo litafanyika siku ya uchaguzi.

Hata hivyo, Dk. Slaa na chama chake wamepinga mpango huo wa NEC na kuituhumu kupanga kuvuruga uchaguzi kwa ajili ya kuipendelea CCM.

Kuwapo kwa vituo hewa kuligunduliwa na wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) wa CHADEMA baada ya kupitia daftari la wapigakura.

Hivi sasa taarifa za mpango huo uliodokezwa na watoa habari ndani ya tume, polisi na usalama, zinadai kuwa “kura zitaibwa kwa nguvu” kupitia vituo vya kupiga kura na ikishindikana hapo, zitaibwa wakati wa majumuisho kwa kuingiza masanduku kutoka vituo hewa.

Hili laweza kuleta kelele zitakazosababisha vurugu na matumizi ya polisi. Mkakati huu umewekeza katika kile kinachoitwa “Tangaza mshindi, asiyeridhika aende mahakamani.”

Jitihada hizi zinatokana na ukweli kwamba CCM imegundua kuwa haikubaliki katika kata nyingi za mjini na vijijini katika jimbo hili.

Kwa mfano, maeneo ya barabara kuu kuanzia Kingori, Kikatiti, Maji ya Chai, Usa River, Kilala, Tengeru na Patandi yamedhibitiwa kikamilifu na CHADEMA.

Wakati huohuo, maeneo ya vijijini kama Pori, Mlala, Ngare Nanyuki, Nkoaranga na mengineyo, CCM inatarajiwa kugawana kura na CHADEMA.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)