CCM yateua 'mafisadi' kufadhili Kikwete 2010


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 November 2009

Printer-friendly version
Rostam Abdulrasul Aziz

WATUHUMIWA wa ufisadi wameteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuunda kamati ya kukusanya fedha za uchaguzi mkuu ujao, MwanaHALISI limeelezwa.

Uteuzi huo ulifanyika Dar es Salaam, wiki iliyopita, katika kikao cha sekretarieti kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba. Kamati hiyo inaundwa na wajumbe watano.

Miongoni mwao, wamo watatu ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa ufisadi mara kwa mara, na wako katika kundi ambalo lilipachikwa majina ya “watafuna nchi,” na “mafisadi papa.”

Majina yaliyochomoza sana ni ya mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Abdulrasul Aziz, Tanil Somaiya na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi.

Wamo pia mfanyabiashara wa Morogoro, Abood Aziz Abood na Mohammed Dewji, mfanyabiashara na mbunge wa Singida Mjini.

Makamba alipoulizwa kuhusu uteuzi wa wajumbe hao, alisema, “Vikao vya sekretarieti ni mambo ya siri. Mimi ndiye mwenyekiti…”

Alipobanwa zaidi akang’aka, “Ni nani kawaambia mambo ya ndani ya sekretarieti? Huyo kawapa umbea…”

Alipoelezwa kuwa ni yeye aliyevujisha siri kwa kumweleza mmoja wajumbe waliopendekezwa, Makamba alisema, “Nani huyo? Kama kuna mtu kawapigia simu kuwaeleza kuwa tulijadili ajenda hiyo katika vikao, ambavyo mimi ni mwenyekiti, basi kaeneza umbeya. Mpigieni tena.”

Wajumbe hao waliopendekezwa na sekretarieti, wanasubiri kuidhinishwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.

Taarifa za ndani ya kikao zinasema uteuzi huo ulizusha zogo na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wajumbe wa sekretarieti.

Waliokuwa wanapinga uteuzi huo, ambao ulisimamiwa na Makamba, walidai kuwa hatua hiyo ingeendelea kukichafua chama chao, ambacho kimekuwa kinahusishwa na ufisadi mkubwa wa vigogo na maswahiba wao.

Baadhi ya wajumbe walimkumbusha Makamba kuwa yeye ndiye amekuwa akikanusha ufisadi wa CCM kwa nguvu zote, lakini uteuzi huu unaoingiza baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika orodha ya wafadhili wa chama, unaweza kusimika dhana kwamba “CCM ni chama cha mafisadi.”

Mbunge mmoja wa CCM alinumkuu mjumbe wa kikao cha sekretarieti hiyo akisema, “wakati wote ambapo ajenda hiyo ilipokuwa inajadiliwa, Makamba alikuwa akitolea macho kila aliyekuwa anaonekana kupinga mapendekezo yake.”

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, wamedokeza kwamba iwapo vikao vya juu vya CCM vitaridhia uteuzi wa wajumbe wanaotuhumiwa kwa ufisadi, upinzani utakuwa umepata mtaji mkubwa kisiasa.

Inaeleweka kuwa baadhi yao ndio waliokifadhili chama hicho kwa fedha na raslimali nyingi katika uchaguzi uliopita, uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani na ambaye tayari anapigiwa debe kugombea tena 2010.

Mingoni mwa wafadhili wakubwa wa kampeni za Kikwete ni Rostam, anayehusishwa na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi ya fedha za umma kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ni Rostam huyo huyo anayedaiwa kuwa “mwasisi wa kampuni ya Kagoda Agricultural Ltd,” iliyosajiliwa 29 Septemba 2005, na ndani ya siku tano baada ya kusajiliwa ilichotewa Sh. 30.8 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT.

Vile vile amekuwa anahusishwa na kashfa ya kampuni ya kitapeli ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development (LLC).

Somaiya anahusishwa na ufisadi kwenye ununuzi wa rada na ndege ya rais, huku Karamagi akihusishwa na mikataba kadhaa ya madini, kashfa ya Richmond na mkataba tata wa kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam (TICTS).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: