CCM yazidi kutota: Huku moto, huku baridi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version

KWA upande mmoja Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinajipiga kifua kimeshinda uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010. Iwe halali au haramu, lakini kipo madarakani.

Kwa upande mwingine, chama hiki hakikushinda uchaguzi kama kilivyotaka na hivyo mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu, ufanye kazi ya kutafuta mchawi na kujivua gamba.

Katika hili, wanachama wamegawanyika katika maeneo mawili. Wapo wanaoamini kuwa CCM imeshindwa uchaguzi kwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete hakupata muda wa kukijenga chama chake na kwamba alibinafisha kampeni kwenye familia yake.

Kampeni za Kikwete zilisimamiwa na ikulu, mkewe wake, Mama Salma Kikwete na wanawe wawili – Ridhiwan Kikwete aliyekuwa anatembea na koba la fedha na msululu wa viongozi wa vijana wa makao makuu (UV-CCM), ambako kila mmoja alikuwa na magari matano na wabunge watarajiwa wa viti maalum kupitia vijana.

Kila alikofika, Ridhiwani na kundi lake walipokelewa na wakuu wa wilaya na mikoa. Wakati hayo yakifanyika, vikundi vya CCM vya Green Guard katika wilaya na mikoa havikuwa hata na fedha ya kununua maji.

Naye Miraji Kikwete alikabidhiwa vikundi vya wanamuziki wa kizazi kipya na “matapeli wa mjini.” Alikuwa na ofisi Kawe na Upanga jijini Dar es Salaam.

Katika kampeni hizo, Kikwete alikuwa anatumia helkopta tatu na magari 20 yaliyokuwa katika misafara mitatu tofauti iliyokuwa inakimbizwa na helkopta.

Mjadala mwingine ambao utaibuka, ni kuhusu kamati ya kampeni iliyokuwa chini ya Abdulrahman Kinana ikiachwa bila fedha wala maamuzi. Kazi kubwa ya Kamati ya Kinana, ilikuwa kujibizana na mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

Wanasema katika kipindi chote cha miaka mitano, Kikwete amefanya kazi ya kuzungusha mawaziri kutoka wizara hii, kwenda wizara ile.

Mfano hai wanaoutoa, ni uteuzi na uhamisho wa Shukuru Kawambwa na Steven Wasira. Wawili hawa wameshazunguka katika wizara zaidi ya tano katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Wanasema kama wahusika walikuwa hawafai, basi wasingeteuliwa kuliko kuwapigisha mchakamchaka.

Wanasema Kikwete ametumia miaka mitano kuteuwa na kuhamisha, naibu mawaziri, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya; maofisa tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti wa bodi na makamishina katika wizara mbalimbali. Ameshindwa kuangalia watendaji wenye sifa ndani ya chama chake.

Kwa hiyo wanataka chama kianzishe mchakato wa kutenganisha kofia mbili – uenyekiti wa chama na urais – ili rais afanye kazi za serikali na mwenyekiti wa chama afanye kazi za chama. Hapa wanadai kuwa mwenyekiti wa chama atapata fursa ya kutosha ya kujenga chama. Atapata pia nafasi ya kutembelea wanachama, kufungua matawi na kujibu hoja za kisiasa za viongozi wa vyama vya upinzani.

Wanazungumzia hata safari za rais nje ya nchi kuwa zimechangia kwa kiwango kikubwa kudhoofisha chama chao. Kwamba ukilinganisha na watangulizi wake wawili – Benjamin Mkapa na Ali Hassani Mwinyi, Kikwete ndiye rais aliyefanya safari nyingi nje ya nchi katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wake.

Mwenyekiti ambaye si rais, atakuwa anapata fursa ya kukutana na viongozi wenzake wa chama bila kuwapo hofu ya kukamatwa na vyombo vya dola. Maana huyu aliyepo sasa, hayuko huru. Analindwa na jeshi na usalama wa taifa.

Ni kupitia mradi huu, wanaopigia upatu mradi wa kutenganishwa kwa kofia mbili, wanataka Kikwete abaki na serikali na wengine wabaki na chama.

Lakini hawa lazima wakae tayari kupambana na kundi la pili la wanaodai kushindwa kwa CCM kumetokana na kupakwa matope na watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.

Kwamba hatua ya baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi kuendelea kushikilia nafasi za juu za uongozi katika chama, ndiyo sababisho kuu la chama kufanya vibaya. Chama kimepoteza sura. Kilidhoofika wakati ule na kinaendelea kudhoofika sasa. Hakikuuzika na hata sasa hakiuziki.

Hoja ni hii. Kuna watu wanaotuhumiwa kufanya ufisadi. Wamo ndani ya CCM. Wako ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC). Ni kwamba wale wanaotuhumiwa, wakiendelea kuwa wanachama, wanakipa chama sura ya watuhumiwa – kuanzia mwanachama wa kawaida hadi kiongozi wa juu kabisa wa chama hicho.

Wanaotajwa kudhoofisha chama, ni pamoja na waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashifa ya Richmond, Edward Lowassa. Mwingine, ni mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Wakati Rostam na Chenge ni wajumbe wa CC na NEC, Lowassa amebaki mjumbe wa NEC tangu alipoondolewa katika wadhifa wake wa uwaziri mkuu, Februari 2008.

Lakini Chenge ana nafasi nyingine nyeti ndani ya chama hicho. Ni mjumbe wa Kamati ya Maadili. Ameteuliwa na Kikwete.

Hakika wanachama hawa watatu ambao ni viongozi wa ngazi ya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu wako jikoni katika chama ambacho kimepanga ikulu. Ni kamati hii inayosimamia utekelezaji wa maamuzi mengi ya chama na kuandaa ajenda za vikao vya juu.

Wajumbe wa vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya chama kilichoko ikulu, ndiyo wanaotunga na kusimamia sera za chama, kuandaa ilani ya uchaguzi na kutoa mwelekeo wa utawala. Wanaweza, kwa vyovyote vile, kuathiri uongozi wa chama chao na taifa.

Ndiyo maana wanaofahamu nguvu ya vikao hivi, wanataka wanachama hawa waondolewe. Wanasema kuendelea kwa watuhumiwa kuwa ndani ya chombo hiki, bila shaka kutakiathiri chama kwa njia mbalimbali: Kitatuhumiwa. Kitatiliwa shaka. Kitadharauliwa. Kitapuuzwa na hatimaye kinaweza kuyeyuka machoni na nyoyoni mwa wengi.

Hivyo agenda yoyote itakayowasilishwa NEC, iwe ile ya kutathmini uchaguzi au kutenganisha kofia mbili, itazalisha mpambano wa pande mbili.

Hii ni kwa sababu, wanaosema Kikwete hana muda wa kujenga chama, ndio haohao wanaotaka kujenga daraja na kumuondoa Kikwete katika kiti chake – siku mia moja baada ya kukikalia.

Huu ni mpango unaoandaliwa na wanaotaka kuingia ikulu mwaka 2015 kwa kuwa rais mtarajiwa atakuwa tayari amekishika chama. Anakitumia chama kupanga safu yake kwa kuweka amtakaye na kumuondoa asiyemtaka.

Hoja hii inaweza kukigawa vipande viwili chama hiki, kwa kuwa wakati katibu mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba anasema wanaotaka kutenganishwa kwa kofia mbili ni wahaini, kiongozi mwingine anayeheshimika ndani ya chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru anaripotiwa kuunga mkono hoja hiyo.

Katika mazingira haya, Kikwete hawezi kupuuza hoja hizi kwa kuwa aweza kufukuzwa katika chama kwa madai “hakisaidii chama chake.” Kipengele hiki kinaweza kuingiza hata nchi katika machafuko.

Aliyekuwa rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi alifukuzwa urais na chama chake kwa kile walichoita, “Amejiuzulu kwa hiari nafasi yake ya urais.” Hata kama katiba haitamki hivyo, ving’ang’aninzi ndani ya CCM wanaweza kusukuma hoja na hata kufanya wabunge kuchocheka kupitisha marekebisho ya katiba.

Si rahisi kutabiri kitakachotokea pale chama kitakampomtaka rais wake ajiuzulu kama ilivyotokea kwa Jumbe, huku aliyetakiwa kujiuzulu akigoma kutii agizo hilo. Hili siyo kwamba haliwezi kufanyika, bali kwa mtindo na mazoea ya CCM, ni geni na labda hatarishi.

Ili Kikwete asiweze kufukuzwa mithiri ya mpangaji aliyeshindwa kulipa pango, atakuwa amebakiza njia moja tu ya kupita: Kuungana na wanaodai kuwa mafisadi wamekichafua chama na hivyo waondoke.

Hapo atakuwa amejihakikishia kubaki katika nafasi yake, vinginevyo anaweza kuondoka katika chama na pengine katika urais, kabla ya kumaliza ngwe yake ya pili ya uongozi.

Kikwete anajua kuwa hatua yake ya kutafuna maneno kwa kuita ufisadi uliofanywa na Lowassa, “ajali ya kisiasa” ndiyo chanzo kikuu cha chama chake kupotezea mvuto kwa wananchi. Haitarajiwi kosa lilelile lijirudie tena katika kikao hiki cha sasa.

Lakini kwa jinsi Kikwete alivyogandamana na Lowassa na Rostam, wapo wanaotilia shaka uwezo wake wa kuondoa marafiki zake hao wawili ndani ya chama chake.

Wanaotilia shaka uthabiti wa Kikwete, wanatolea mfano uamuzi wake wa kubariki kumuondoa katika kinyang’anyiro cha uspika Samwel Sitta kwa hoja kwamba mgombea anayetakiwa ni mwanamke na Sitta, kwa vyovyote vile, hata kwa kurejea vyuoni kutafuta digrii nyingine, asingepata sifa hiyo.

Mbali na hilo, Kikwete ameshindwa kumuondoa katika nafasi yake, Yusuf Makamba anayetuhumiwa kukivuruga chama chake. Alikuwa ni Makamba aliyeshiriki katika kikao cha Baraza Kuu la Vijana (UV-CCM taifa) lililopitisha maamuzi ya kutaka Kikwete avunje Kamati Kuu kwa hoja kwamba imeshindwa kumsaidia kusimamia serikali na chama.

Makamba ni mjumbe wa Kamati Kuu ambayo vijana wametaka ivunjwe. Kikwete ndiye mwenyekiti wa kikao hicho muhimu cha chama, ambacho vijana wametuhumu kushindwa kazi.

Katika hali ya kawaida, Makamba asingeweza kuendelea kuwa mtendaji mkuu wa chama wakati mwenyewe ameshiriki katika kupitisha maamuzi ya kutaka Kamati Kuu ivunjwe.

Wala Makamba asingeweza kubaki katika nafasi yake, wakati tayari ameshiriki katika “kutengeneza uasi” wa kukivuruga chama chake na mwenyekiti wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: