Celtel lawamani


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Jaji Joseph Sinde Warioba

UONGOZI wa kampuni ya Celtel International jijini Dar es Salaam, umeshindwa kujibu tuhuma zinazoukabili kuhusu kutumia mali za TTCL kujiimarisha.

Wiki iliyopita gazeti hili lilinukuu baadhi ya vyanzo vilivyosema Celtel International inatumia mitambo ya TTCL iliyotapakaa nchini kuimarisha biashara yake ambayo haina mafao kwa TTCL.

Celtel International iliundwa kutokana na Celtel Tanzania ambayo nayo ilitokana na mtaji uliopatikana kwenye biashara ya makampuni ya MSI/Detecon yaliyokuwa na ubia na TTCL.

MSI/Detecon ambao walipaswa kuimarisha TTCL kwa kulipa dola 120 milioni kama malipo ya hisa 35 katika kampuni hiyo, wanadaiwa kulipa nusu ya malipo hayo hadi walipoondoka nchini mwaka 2005.

Ni MSI/Detecon waliounda Celtel Tanzania na baadaye Celtel International ambayo imekuwa ikitumia mitambo na mali nyingine za TTCL kwa kujiimarisha hadi kuwa katika nchi za Afrika Mashariki, Kati, Kusini na Maghgaribi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa Celtel International kwa mwandishi wa gazeti hili inaeleza matukio ya mwaka 2005 ambayo hayana uhusiano na hali halisi ya sasa inayolalamikiwa.

Katika mawasiliano yake Alhamisi, 10 Julai 2008, kwa njia ya baruapepe, ofisa huyo Georgia Mutagahywa amewasilisha andishi ' TTCL and Celtel Separated' (Makampuni yatenganishwa) ambalo halisemi lolote juu ya hali ya sasa.

Hata hivyo, taarifa ya Mutagahywa imethibitisha kuwa Celtel International inatokana na Celtel Tanzania ambayo ilikuwa kampuni tanzu ya TTCL.

Aidha, imefahamika kuwa hata Celtel International imeishanunuliwa na kampuni ya MTC ya nchini Kuwait inayoendesha makampuni matano makubwa ya simu za mkononi eneo la Mashariki ya Kati.

'Unaona sasa, mitambo ya TTCL ambayo ilianza kutumiwa na MSI/Detecon na kuzaa Celtel, ndiyo imezaa Celtel International na sasa in aendelea kuhimili mtandao mkubwa hadi nchi za Arabuni,' amelalamika mmoja wa wafanyakazi wa TTCL ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.

Waraka wa Mutagahywa haujibu hoja Celtel kuwa kampuni tanzu; kutumika kwa fedha za TTCL kuanzisha Celtel; matumizi ya mitambo ya TTCL kusambaza mtandao na kudhoofisha na hata kuua miradi ya TTCL iliyokuwa muhimu kwa nchi zote za Kusini mwa Afrika.

Aidha, imefahamika kuwa maofisa waandamizi nchini walioshiriki kubinafsisha TTCL kwa mwekezaji mgeni, ndio wanaounda Bodi ya Wakurugenzi inayosimamia menejimenti ya kampuni hiyo kwa sasa.

Imefahamika pia kuwa maofisa waliofanikisha utaratibu wa kuiingiza TTCL katika menejimenti ya wabia wa kigeni baada ya MSI/Detecon, ndio sasa sehemu ya menejimenti ya TTCL.

Mmoja wa maofisa hao ni George Mbowe, mfanyabiashara wa siku nyingi nchini ambaye sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL.

Wakati mchakato wa kubinafsisha TTCL unaanza na ulipokamilika, Mbowe alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kurekebisha na Kubinafsisha Mashirika ya Umma (PSRC).

Awali Mbowe alikuwa mjumbe wa Bodi ya lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC) ambalo baada ya kugawanywa, ndipo ilizaliwa TTCL na Shirika la Posta (TPC).

Wajumbe wengine wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kama walinzi wa hisa 65 za serikali, inayoongozwa na Profesa Mathew Luhanga, ni Agnes Bukuku na Iddi Suwedi.

Upande wa Celtel International, mkurugenzi wao katika bodi hiyo, ni Jaji Joseph Warioba wakati Gilder Kibola ni Katibu wa Kampuni ya TTCL.

Profesa Luhanga ambaye aliwahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 2006, kwa muda mrefu sasa amekuwa Afrika Kusini.

Kulingana na taarifa ya menejimenti ya TTCL ya mwaka 2006 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Celtel International inatambulishwa kama mbia wa TTCL.

Vyanzo vya habari vimesema kwamba Celtel ilianzishwa katika mazingira tata kwa kuwa wakati MSI/Detecon wanaingia TTCL, kulishasajiliwa kampuni ya Celnet iliyokusudiwa kutoa huduma ya simu za mkononi.

Mpaka sasa haijulikani mradi huo pamoja na mingine kadhaa iliyokuwa ndani ya mipango ya maendeleo ya TTCL, ilivyofutwa.

Uendeshaji TTCL ulioacha maswali mengi, ulisukuma baadhi ya wataalamu wa kampuni hiyo waliosomeshwa na TTCL hadi kufikia shahada ya falsafa (PhD) kuacha kazi kwa kukerwa na mazingira mabaya ya uendeshaji kampuni.

Matatizo yalioko TTCL hadi sasa yalisababisha chama cha wafanyakazi wa mawasiliano (TEWUTA) Mkoa wa Dar es Salaam kupeleka malalamiko kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006.

Moja ya mapendekezo ya msingi waliyotoa ni kuondolewa kwa uongozi wote uliopo TTCL ili kampuni irudi kwenye mstari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: