CHADEMA: Chuki na visasi vya mawifi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 02 December 2009

Printer-friendly version

JUHUDI za ndani kwa ndani za kuzamisha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huenda zikagonga mwamba. Lakini zinaendelea.

Taarifa za uchunguzi ndani ya CHADEMA zinaonyesha kuwa mradi mkubwa wa wanachama na viongozi kuhama chama hicho umeiva. Hiyo ni kwenye makao makuu Dar es Salaam na mikoani.

Viongozi ambao wako mbioni kuondoka, bila kujua iwapo wanakwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) au vyama vingine vya upinzani, ni wawili kutoka uongozi wa kitaifa; sita kutoka idara ya wanawake; wanne kutoka miongoni mwa wazee na 14 kutoka idara ya vijana.

Wengine 37 kutoka ngazi mbalimbali za mikoa wanatarajia kutangaza kujiondoa katika chama, kwa mtindo wa mmoja baada ya mwingine, ili kuweka sura ya mkondo wa wanachama kukimbia.

Orodha ya viongozi watakaokuwa wamehama CHADEMA ifikapo Februari mwakani inatembea kwa siri mikononi mwa baadhi ya viongozi wa idara za vijana na wanawake.

Hata hivyo, imebainika kuwa maandalizi ya kudoofisha CHADEMA yamekuwa hafifu kwa maana kwamba hoja hazijawa thabiti na wengi wanaotumika na, au kutumiwa wana sifa za uanasiasa wa magazetini, redioni na kwenye televisheni tu; siyo wana-mikakati.

Ukabila wa Wachaga, ukosefu wa demokrasi na matumizi mabaya ya “fedha za ruzuku,” ndiyo mabango makuu ya wanaopinga uongozi wa sasa ndani ya CHADEMA.

Mabango haya yametumiwa zaidi na CCM hasa wakati wa uchaguzi ili kuchafua CHADEMA.

Wakati mwingine CCM ilipoopoa mwanachama wa upinzani, viongozi wake walitaka “anyee kambi” hadharani; atoe lawama, shutuma na tuhuma kwa viongozi na chama chake cha zamani huku akiwa amevalishwa shati la rangi ya kijani.

Rudisha nyuma kanda za televisheni na soma magazeti yaliyopita. Ushahidi mtupu. Ndivyo walivyofanya akina Thomas (Ngowi) Ngawaiya, Abbas Mtemvu, Masumbuko Lamwai, Danhi Makanga, Tambwe Hiza, Mbaruku Msabaha, John Guninita. Orodha ni ndefu.

Mabigwa wa kunyea kambi waliambulia nafasi za uongozi katika CCM na hata serikalini. Hadi leo, na kuna dalili kuwa hili litaendelea, kila anayekana wenzake katika chama na kuwapaka matope, aweza kuzawadiwa, ikiwa ni pamoja na kupewa jimbo la kugombea ubunge.

Hali hii inayoweza kuitwa “kiungulia cha kisiasa,” inaelekeza kuwa sharti “utukane ndipo utukuke;” na mwenye uwezo wa kupima uzito na kiwango cha kunyea kambi ni mpinzani wa chama chako.

Yanayotendeka ndani ya CHADEMA leo hii, ni mwendelezo wa yaliyokwishatendeka katika vyama vingine kwa nyakati tofauti.

Katikati ya mwezi uliopita, David Kafulila aliyekuwa ofisa wa habari wa chama hicho alijiondoa uanachama baada ya kunyang’anywa nafasi hiyo ya uongozi. Amejiunga na NCCR-Mageuzi. Ameacha amenyea kambi.

Wiki iliyopita, Juju Danda aliyekuwa ofisa wa masuala ya bunge wa CHADEMA alijivua uanachama huku akidai kuna matumizi mabaya ya fedha. Hii ni baada ya kuondolewa kwenye uongozi wa idara ya bunge.

Hata hivyo Danda ameibua madai mapya; kwamba yeye na Kafulila walifukuzwa uongozi wa idara zao kutokana na kutofautiana mawazo na viongozi wakuu, hasa pale walipomuunga mkono Zitto Kabwe aliyetaka kugombea nafasi ya mwenyekiti wa taifa.

Madai haya yanaonyesha kuwa hadi wakati wa uchaguzi mkuu ndani ya chama, kulikuwa na mikutano mingi ya siri; ahadi nyingi za siri; maapizo ya kila aina; joto la mapinduzi kwa njia ya sanduku la kura na labda safu mpya ya uongozi.

Kwa hiyo wafuasi wa Zitto, ambao kwa muda mrefu walikuwa wamejiandaa kufanya mabadiliko, bado wapo na wengine hawajakubali kwamba Zitto aliishasema “yaishe.”

Aidha, kwa Zitto kusema yaishe ni kupoteza wafuasi na mashabiki wake katika chama ambao tayari alikuwa amewaahidi na walikuwa wakipigania mabadiliko au mapinduzi. Siyo rahisi kuwakana na siyo rahisi kuendelea nao wote hadi uchaguzi mwingine.

Kuendelea kuwa na wafuasi wake, wasio katika uongozi wakati yeye anaendelea katika uongozi aliokuwa anataka kuubomoa, ndiko kunafanya wapenzi wake kusema huko alipo “yupoyupo tu.”

Vilevile kuendelea kuwa kwenye uongozi nje ya uongozi wa wale aliowaandaa, ama ni kujiandaa kufanya mapinduzi au kujiandaa kuondoka katika chama.

Kafulila analiweka vizuri hilo kama anayeongea moyo wa Zitto. Anasema Zitto hajasema kuwa anaondoka CHADEMA lakini ana uhakika kuwa atafanya (Zitto) “maamuzi makini.”

Je, kauli hii haiwezi kuwa na maana kwamba Kafulila ametangulia na wengine, akiwemo Zitto watafuata? Swali ni kufuata wapi; NCCR-Mageuzi, CCM, CUF au nje ya vyama?
 
CHADEMA ilianza kuvuma zaidi baada ya Freeman Mbowe kuwa mwenyekiti mwaka 2003. Mwaka huo pia Zitto alimaliza masomo chuo kikuu na kuanza moja kwa moja siasa za wazi. 

Uongozi chini ya Mbowe uliokuja kwa staili mpya na mpango mahususi wa “Kuanzisha CHADEMA Upya.” 

Wakati huo viongozi wake walianza kufanya ziara nchi nzima, wakihutubia kwa sauti, hoja, mifano na ahadi – mithili ya nyakati za kuasisi mageuzi – kati ya 1985 na 1992.

Hotoba za nyakati hizo zilikuwa za kuwapa wananchi ujasiri wa kudai haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya kushiriki siasa za nchi yao; na kuwapa taarifa na maarifa ambavyo ni nyenzo muhimu katika kufikiri na kutenda.

Maarifa hayo yaliwasaidia kujiuliza kwa nini wasibadilike; kwa nini waache kuchagua chama kilekile cha miaka yote na kwa nini wachague hata asiyekubaliana na serikali.

Ni hotuba hizi ambazo ziliitwa za “uamsho,” zilizotoa wengi usingizini; kusambaza elimu na kusisimua vijana wengi nchini; kuleta mvuto kwa upinzani na sasa zilikuwa zinavuna ufuasi mkubwa kwa CHADEMA mpya.

Enzi za “siasa poa” za waanzilishi – Edwin Mtei na Bob Makani – walezi wa chama hadi vijana wakakamavu wakajitokeza, zikatoa fursa kwa mlipuko uliowavuta vijana wengi.

Ni katika “CHADEMA Mpya” ambamo Zitto Kabwe na vijana wengine wamekuwa wakishiriki uongozi.

Kilichoitwa “chama cha Wachaga” kikavuna wanachama kutoka sehemu nyingi nchini hadi kufikia kuongoza halmashauri mbili  za wilaya (Karatu na Tarime) na kugawana uongozi na CCM katika halmashauri moja (Kigoma-Ujiji).

Leo kuna mradi wa wanachama kuhama CHADEMA. Kwa nini leo? Kuna wanaosema uchaguzi mkuu umekaribia; CCM inavuruga uongozi kwa makusudi. Hilo linawezekana lakini itakuwa inavuruga wanaovurugika.

Wanaojiondoa au wanaojiandaa kujiondoa CHADEMA wanafanya kazi moja nzuri – ile ya kujisafisha kwa njia ya kusafisha chama.

Hata hivyo wasinyee kambi kwani hizo ni siasa za visasi vya mawifi; kwani siku moja waweza kujikuta wakirejea “nyumbani.” Wamuulize Guninita.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: