CHADEMA, CUF ondoeni "shetani"


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Gumzo

MFARAKANO unafukuta ndani ya kambi ya upinzani. Vyama viwili vikuu – Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), vimeanza kushutumiana.

Vyama hivi pamoja na UDP au United Democratic Party, ndivyo vinavyounda kambi ya upinzani ndani ya bunge.

Vimefanya kazi kubwa ndani na nje ya bunge kufikia sasa. Mafanikio ya wazi yaliyopatikana kutokana na nguvu yao, ni kujenga umma katika namna ya kuwa na mwamko wa kutambua haki zao.

Hili limepatikana kutokana na upinzani kutoboa siri zinazohusiana na ufisadi ndani ya sekta ya umma ikiwemo kutaja orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi kwenye mkutano wa hadhara wa 15 Septemba 2007 pale viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam.

Wengi walitarajia vyama vya upinzani vingeendelea kushikamana na kukabiliana na mpinzani mkuu – CCM, hasa baada ya kuthibitika kuwa chama tawala kimeanza kutikisika kutokana na shutuma zisizokwisha za viongozi wake, wakiwemo wale waliomo serikalini, kuhusishwa na ufisadi.

Ni vigumu kuamini CCM, kwa namna mbalimbali, haihusiki na mfarakano unaokabili wapinzani wake. Mfarakano wenyewe unaonufaisha sana CCM.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba mfarakano huo umezuka wakati Muswada wa Sheria unaolenga kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992 (Political Parties Act of 1992) unatayarishwa na huenda ukafikishwa bungeni baadaye mwaka huu.

Kama marekebisho hayo yatapitishwa, utaviwezesha vyama vya siasa kuungana, bila ya chama kulazimika kupoteza uwakilishi wake bungeni.

Aidha, marekebisho hayo yataviwezesha vyama kuunda umoja (alliance) utakaotambulika kisheria, na hivyo kutambulika katika uchaguzi. Hivyo basi, mfarakano kati ya CHADEMA na CUF ni msiba mkubwa kwa taifa.

Dalili za mfarakano huu zilianza wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Tarime, mkoani Mara, uliofanyika kujaza nafasi iliyoachwa baada ya kifo cha Chacha Zakayo Wangwe (CHADEMA). Wangwe alikuwa pia makamu mwenyekiti wa CHADEMA.

Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na ushirikiano ulioundwa na vyama vine: CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi.

Ulikuwa ni ushirikiano ulioashiria mema katika upinzani. Baadhi yetu tulipata matumaini kwamba hatimaye upinzani nchini utakuwa na nguvu kubwa.

Hata hivyo mara tu baada ya kifo cha Wangwe ambacho rasmi kilielezwa kuwa ni ajali ya gari, kulisukwa mikakati ya kutaka kuonyesha kuwa haikuwa ajali, bali ni mauaji ya makusudi yaliyohusisha viongozi wa CHADEMA.

Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya msiba wa Wangwe, uliofanyika kijijini kwao Kemokerere, wilayani Tarime.

Kinyume na matarajio ya wengi, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani vilivyojenga ushirika, walisikika wakitoa kauli za kuhusisha viongozi wa CHADEMA na kifo cha Wangwe.

Ama kwa hasira au kwa kujiamini au kutokana na uhakika utokanao na uchunguzi thabiti, CHADEMA iliamua kwenda kivyake kwa kuweka wagombea – udiwani na ubunge katika jimbo la Tarime.

Chama cha NCCR-Mageuzi kiliweka mgombea ubunge na kuungwa mkono na CUF na TLP.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alinukuliwa akisema chama chake hakiungi mkono mgombea yeyote wa upinzani jimboni Tarime.

Hata hivyo, uongozi wa CUF wilayani Tarime ilimuunga mkono mgombea wa CHADEMA. Bila ya shaka walifanya hivyo bila baraka za viongozi wao wa kitaifa.

CHADEMA iliibuka mshindi kwa ubunge na udiwani, ushindi uliotokana na imani ambayo wananchi wa Tarime waliwapa. Hapo ndipo ikaanzishwa inayoitwa “Operesheni Sangara” inayoeneza ujumbe wa chama na sera zake nchi nzima sasa na kuitikisa CCM.

Malumbano yanayoendelea sasa kati ya CUF na CHADEMA yamekolezwa na kauli zilizotokana na kampeni za uchaguzi Mbeya Vijiji ambako mgombea wa CHADEMA alienguliwa kwa “kushindwa kujaza fomu za mgombea inavyostahili kisheria.”

Na hakuna kitu kingine ambacho baadhi ya viongozi wa CCM na serikali yake wangependa kuona kinashamiri kama kusambaratika kwa CHADEMA, ama kuvunjika kabisa kwa kambi ya upinzani ndani na nje ya bunge.

Hii ni kwa kuwa ajenda kuhusu ufisadi imeumbua vema baadhi ya viongozi na washirika wao ndani ya CCM.

Ni ajenda ya kupambana na ufisadi iliyochanganyika na umahiri wa kujenga hoja na ushupavu wa viongozi wa CHADEMA, iliyokiinua na kukiimarisha chama hicho.

Bali kuimarika kwa CHADEMA kunaweza kuiangamiza CUF. Dalili zimeanza kuonekana. Profesa Lipumba amepata mpinzani katika uchaguzi ndani ya chama chake.

Aliyejitokeza kupambana naye ni Profesa Abdallah Safari. Inawezekana asitoe upinzani mkubwa, lakini kauli zake kwamba “CUF iko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU),” inakuza ufa na kukiumiza chama hicho.

Wengi wanaona kuwa suala la kutomalizika kwa mgogoro wa kisiasa ulioko Zanzibar, nalo limechangia kukitafuna chama cha CUF.

Ni miaka 12 sasa tangu mgogoro huo ulipoanza kushughulikiwa. Ilikuwa ni Jumuiya ya Madola iliyoingia na kufanikisha kusainiwa kwa muafaka wa kwanza kati ya CCM na CUF Juni 1999. Siyo tu utekelezaji wa muafaka huo haukufika mbali, bali yaliyoufuata yalizidisha chuki na hatimaye kuzuka kwa mauaji ya 26-27 Januari 2001, miezi miwili tu baada ya uchaguzi wa 2000 uliolalamikiwa na CUF na ambao waangalizi wa kimataifa waliuita “aibu tupu.”

Hadi sasa, mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi licha ya ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa 30 Desemba 2005 alipozindua bunge. Chama chake mwenyewe kimeupiga kumbo kwa kutoa hoja mpya ya kura ya maoni wakati makubaliano yalishafikiwa na kusubiri kusainiwa.

CUF haionekani kwa kakamavu katika kupinga ufisadi, ingawa Profesa Lipumba amekuwa akisikika sana akilalamikia mipango na mienendo mibaya ya utawala wa serikali ya CCM.

Yote haya na mengine yanapanua ufa kwa upande wa CUF hata kama hayaongezi mafao ya moja kwa moja kwa CHADEMA.

Aidha, tayari ni kiini cha mjadala mitaani ambapo vijana wa CHADEMA wanajivuna kuwa angalau harakati za chama chao zimefanikisha kutinga mahakamani kwa zaidi ya watuhumiwa 20 wa ufisadi wakiwemo mawaziri wawili wa zamani.

Ufa kati ya CHADEMA na CUF ulipanuka zaidi Mbeya Vijijini wakati baadhi ya viongozi wa CUF waliposema “kampeni zisiwe za kuchafuliana majina kwa tuhuma za ufisadi zisizokuwa na ukweli,” kauli iliyotarajiwa kutoka CCM peke yake.

Hakuna anayefurahia mgawanyiko wa upinzani unaoleta mauti kwa wanaoikosoa serikali na kuinyima usingizi. Wala hakuna anayetaka kibaki chama kimoja cha upinzani baada ya TLP na NCCR kutota.

Inahitajika akili mpya ya kuweka pamoja wapiganaji wa CUF na CHADEMA, hata kama si kwa lengo la kuungana; lakini angalau kusikilizana na kubadilishana mawazo na mbinu za kupambana dhidi ya CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: