CHADEMA: 'Hatutetereki hadi kieleweke'


John Mnyika's picture

Na John Mnyika - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
John Mnyika

MAKALA ya Ndimara Tegambwage yenye kichwa cha habari, CHADEMA: Chuki na visasi vya mawifi inastahili kujadiliwa.

Kwa wale tuliosoma kitabu chake cha “Duka la Kaya” tulipokuwa sekondari, tumejifunza jinsi Ndimara alivyo mjuzi wa kutumia lugha ya picha kufikisha ujumbe anaokusudia kwa hadhira yake.

Makala hiyo iliyochambua kile alichokiita taarifa za kiuchunguzi wa mambo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imedokeza mkakati wa baadhi ya wanachama kukimbia CHADEMA.

Amewaasa wasifanye kile alichokiita “kunyea kambi.” Ametumia busara kuwaasa kwamba sio lazima “utukane ili utukuke.” Utukufu haulingani na utukutu; mwanadamu anaweza kupata umaarufu kwa wema au ubaya; lakini umaarufu wa ubaya hauna maana katika jamii ya wastaarabu.

Katika siku za karibuni pamekuwa na taarifa katika vyombo kadhaa vya habari zenye kupotosha hali ya mambo ndani ya chama baada ya uamuzi wa Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa kutengua uteuzi wa maafisa wawili wa chama tarehe 10 Novemba 2009.

Lakini kauli za maofisa ambao uteuzi wao umetenguliwa, David Kafulila na Danda Juju, hakika ni za “kunyea kambi” na zinalenga kuchonganisha viongozi.

Kafulila na Juju walizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa CHADEMA kuna uongozi mbaya, ukabila na matumizi mabaya ya fedha. Wamedai pia kuwa wamefukuzwa kwenye nafasi zao kutokana na wao kutaka mabaya hayo yarekebishwe.

Napenda wasomaji wa MwanaHALISI wajue kwamba kutenguliwa kwa uteuzi wao hakutokani na sababu wanazotaja, bali kwa wao kukiuka kanuni, maadili na itifaki ya chama katika utendaji wao.

Uamuzi wa kutengua uteuzi wa maafisa hao ulitokana na kikao cha Sekretariati ya Kamati Kuu ya chama cha tarehe 10 Novemba 2009 ambamo nilishiriki kikamilifu.

Ulitokana na vitendo vyao vya utovu wa nidhamu kwa mujibu wa vifungu 10.1(i), (viii), (ix), (xi), (xii) na 10(2)(iv), (ix), (ix) vya kanuni za chama.

Utovu unaotajwa ni pamoja na kutuhumu viongozi wenzao nje ya vikao vya chama; kuendekeza makundi ya majungu; kutuhumu viongozi na chama kwa tuhuma za uongo hata ikiwa ni ndani ya vikao vya chama; kwa jumla kutozingatia maadili ya uongozi.

Vijana hao kwanza, hawajawahi kutoa madai wanayoyatoa sasa katika kikao chochote cha chama. Pili, hawakufukuzwa chama. Hata barua walizopewa zinaeleza wazi kuwa uteuzi wao ndio umetenguliwa na kwamba wajitahidi kuwa wanachama waadilifu.

Kwa hiyo kauli zao kuwa “CHADEMA wanafukuzana,” au ni “visasi na chuki za mawifi” ni propaganda za kufanya Watanzania waache kuamini chama chetu. Ukweli kauli hizo ni za kunyea kambi halafu wakimbie na kutangaza “kambi inanuka.”

Kafulila amedai kuyeyuka kwa Sh. 35 milioni za chama na kuhoji hatua ya mwenyekiti Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa Fedha, Anthony Komu kuwa watia saini hundi za chama.

Hili limewekwa wazi na Dk. Slaa. Maamuzi ya nani afanye nini katika chama huamuliwa na vikao na kama kuna upotevu wowote, basi vikao hivyo vingefahamu.

Chama kiko tayari kukaguliwa na mkaguzi mkuu wa serikali na matumizi yake katika uchaguzi yamekuwa yakiwekwa wazi tangu 2006.

Katika hali ya juu ya kunyea kambi, Kafulila na Juju wamedai kuwa CHADEMA ni mali ya Mbowe na Dk. Slaa na kwamba wanaiendesha kidikiteta. Ashakumu si matusi: Huku ni kwenda haja kubwa hadharani.

Kauli hizi ni matusi kwa wajumbe wa vikao vya juu vya chama; kuanzia Kamati Kuu ya chama inayokutana kila baada ya miezi mitatu, Baraza Kuu la Chama ambalo limekuwa likikutana kila mwaka na Mkutano Mkuu wa chama ambao ndani ya kipindi cha miaka mitano pekee umefanyika mara tatu; mwaka 2005, 2006 na 2009.

Ni vikao hivi vya kikatiba ambavyo vimekuwa vikifanya maamuzi kuhusu mwelekeo wa chama; maamuzi ambayo leo vijana wawili waliojivua uanachama wanajaribu kuyabeza. Kauli hizi zinalenga kuwachafua viongozi wakuu wa chama mbele ya wananchi wanaounga mkono chama chetu.

Natoa rai kwa Watanzania kusoma alama za nyakati tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2010. Upo mkakati ambao ulianza toka miaka kadhaa ya nyuma wa kuwachafua viongozi wakuu wa upinzani kwa lengo la kupunguza imani ya wananchi kwao.

CHADEMA imepita vikwazo vingi. Baada ya uchaguzi wa ndani ya chama mwaka 2004, Mweka Hazina Taifa, Paul Kyara alijivua uanachama na kuanzisha chama cha SAU. CHADEMA ilisonga mbele na kuongeza idadi ya wabunge na madiwani katika uchaguzi wa 2005.

Mwaka 2006 baada ya kuandikwa kwa katiba mpya ya chama na kuzinduliwa upya kwa chama, Makamu Mwenyekiti Aman Kaborou alijivua uanachama na kjiunga na CCM. Pamoja na kauli za uchafuzi, chama kikasonga mbele salama.

Mwaka 2007, mwezi mmoja tu kabla hatujatoa Orodha ya Mafisadi (list of shame) 15 Septemba, Naibu Katibu Mkuu Shaibu Akwilombe alijivua uanachama na kuingia CCM. Hata hivyo, chama chetu kilisonga mbele na kumchagua Zitto Kabwe kuziba nafasi yake.

Mwaka 2008 aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Chacha Wangwe (Apumzike kwa Amani) alisimamishwa uongozi. Uchafu ukaenezwa juu ya CHADEMA.

Hata baada ya kifo chake, viongozi wa CCM na watuhumiwa wa ufisadi wakajaribu kutumia msiba wake kuchafua chama chetu. Kwa mara nyingine chama kikapita salama na kushinda pia uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Tarime.

Machi mwaka huu, chama kilimwndoa mjumbe wa Kamati Kuu, Mecky Mziray. Propaganda chafu zikafanywa na wakati wa uchaguzi wa chama Septemba propaganda zikafanywa kuwa chama kitavunjika wakati huo. Chama kimepita salama na kuchagua viongozi wake.

Sasa ikiwa imebaki miezi 10 tu kufanya uchaguzi mkuu – 2010, CCM ambayo imeghubikwa na tuhuma za ufisadi, imeanza kupenyeza mkono wake mchafu katika CHADEMA ambacho kilikuwa cha kwanza kuanika ufisadi mchafu wa serikali ya CCM na viongozi wake.

Hivyo, kama ambavyo kwa miaka yote CHADEMA, chini ya uongozi wa Mbowe, Dk. Slaa na viongozi wenzao, kimeweza kuvuka na kushinda majaribu makubwa zaidi, ndivyo kitakavyoendelea kuwa salama “mpaka kieleweke.”

Nakubaliana na Ndimara kuwa waliojiondoa na wanaojiandaa kujiondoa CHADEMA, wanafanya kazi moja nzuri- wanaisafisha CHADEMA. Wananchi watawatambua kwa harufu zao za kifisadi.

John Mnyika ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA. Anapatikana: 0754694553 na imeili: mnyika@chadema.or.tz
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: