CHADEMA kufuta kinga ya Mkapa


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebainisha maeneo matano ya kipaumbele katika “kipindi kifupi kijacho,” ili kujiimarisha miongoni mwa umma.

Vipaumbele hivyo vimeelezwa, kwa nyakati tofauti, na viongozi wa juu wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu mkuu, Dk. Willibrod Slaa.

Katika hotuba za viongozi hao, imefafanuliwa kuwa watasimamia mambo hayo matano likiwemo la kujenga hoja ya kuwafutia kinga ya kushtakiwa viongozi wastaafu.

Maeneo yenyewe ni:

  • Kuwaondolea mafao viongozi wa kitaifa wastaafu ambao watajiingiza katika siasa za ubaguzi wakati wakilipwa mafao kwa fedha za walipa kodi wote.
  • Kuwaondolea viongozi wa kitaifa waliostaafu, kinga inayofanya wasishitakiwe kwa makosa waliyofanya wakiwa madarakani.
  • Kuendesha elimu ya uraia nchi nzima ili umma uamke kama inavyoanza kujionyesha katika majimbo ambako Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinabwagwa kwenye chaguzi.
  • Kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa katiba mpya huku kikipigania kurekebishwa kwa vifungu katika sheria ya mabadiliko ya Katiba.
  • Kuhakikisha kinasimamia kesi zote zinazokikabili, nyingi zikiwa za kubambikiwa, ili kiweze kufanya kazi za kisiasa bila bughudha.

Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Arusha, Mbowe alisema CHADEMA kitaanzisha harakati za mabadiliko ya sheria kupitia katiba mpya.

Kwa njia hii alisema, kitahimiza fikra bora za kuondoa kinga kwa viongozi wastaafu ambao, kwa jeuri na ubabe, walitawala kwa udhalimu na hata kusaidia kukua kwa ubadhilifu na ufisadi.

Alisema viongozi wa serikali, ambao watabainika kutenda makosa wakiwa madarakani, kwa makusudi ya kuumiza umma, sharti washitakiwe.

Katiba ya sasa, inatoa kinga kwa  rais aliyeko madarakani au aliyestaafu, kutoshitakiwa kwa makosa ya jinai, aliyotenda akiwa madarakani na baada ya kustaafu.

Alisema wataendesha harakati hizo, kutokana na viongozi waliopo madarakani kujiwekea sheria zinazowapa kinga ya kutoshtakiwa kwa makosa wanayotenda kwa makusudi wakiwa madarakani.

Alitolea mfano tukio la mauji ya Arusha ya Januari 5 mwaka jana, ambapo licha ya polisi kuwaua wananchi kwa kuwapiga risasi, hakuna aliyefikishwa mahakamani hadi sasa.

Mbowe alikuwa akiongea baada ya Mahakama Kuu kutengua ubunge wa Godbless Lema, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini.

Kwa upande wake, Dk. Slaa, aliwaeleza waandishi wa habari 5 Aprili 2012 jijini Dar es Salaam, kuwa chama hicho kitaanzisha mchakato ili kiongozi mstaafu anayekiuka maadili asiendelee kulipwa fedha za wananchi.

Dk. Slaa alisema hayo baada ya kupokea msaada wa Sh. 100 milioni, zikiwa pongezi kwa chama chake kushinda kiti cha ubunge cha Arumeru Mashariki.

Fedha hizo zilitolewa na mfanyabiashara maarufu nchini na kada wa CCM, Mustapha Sabodo.

Dk. Slaa alimlenga rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa anayejihusisha katika kampeni za uchaguzi mdogo akitumia fedha za walipakodi.

“Ingawa haki inaweza kucheleweshwa, lakini tutahakikisha tunalisimamia hili ili itungwe sheria inayobana kiongozi mstaafu anayekiuka maadili asiweze kulipwa fedha za walipa kodi,” alisema.

Katika utawala wake, Mkapa alituhumiwa kukiuka misingi ya utawala bora ambayo ni pamoja na kuanzisha kampuni ya biashara huku akiwa ikulu.

Naye Mbowe amerudia kutangaza kwenye mikutano yake kuwa chama hicho kimedhamiria kusimamia kesi mbalimbali anazodai zina lengo la kukidhoofisha hadi haki ipatikane.

“Tunawaheshimu mahakimu na majaji wote, lakini wanapokosea hatutaacha kuwaambia, kwani wao sio miungu; ni binadamu kama sisi,” amesema Mbowe.

Vilevile, chama hicho kimekusudia kuendesha elimu ya uraia kwa umma kwa ngazi zote ili umma uamke kama inavyoanza kujionyesha katika baadhi ya maeneo kama vile mkoani Arusha.

Katika kutoa elimu hiyo, chama hicho kitahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa katiba mpya, ili wajitokeze kutoa mawazo yao.

Wakati mikakati hiyo ikiendelea, Mbowe ameibua madai kuwa chama chake kimebaini mpango wa CCM kutaka kukidhoofisha bungeni na kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Hata wakitupiga risasi, mimi na Dk. Willibrod Slaa, bado nguvu ya mageuzi nchini haitafutika kwani kuna makamanda wengi ambao wanataka mabadiliko ya kweli katika nchi hii,” amesema Mbowe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: