CHADEMA wanahukumiwa kabla ya kusikilizwa


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

LEO tutafanya mtihani wa kupima uwezo wetu wa uelewa wa mambo rahisi ya kila siku nchini. Wale watakaofaulu hawatapata tuzo lakini wale watakaonekana kufeli au kupata maksi chache watapelekwa Ngurudoto  kuhudhuria semina elekezi na watalipwa posho ya kutosha.

Katika mtihani wa leo, wananchi watatakiwa kusoma habari fupi ifuatayo na kisha kujibu maswali yatokanayo na habari hiyo. Kila msomaji/mwananchi atakayesoma na kujibu maswali anatakiwa kuchagua jibu moja tu analodhani ndilo sahihi zaidi. Sasa soma habari hii:

… Awali kabisa tulitangaziwa kwamba siku ya Alhamisi 15 Septemba, 2011 kulizuka vurugu kubwa katika kata ya Isakamaliwa wilayani Igunga zilizowahusisha viongozi wa CHADEMA na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Igunga, Bibi Fatma Kimario.

Tuliarifiwa kwamba katika vurugu hizo wanachama na viongozi wa CHADEMA walimkamata ‘redihendedi’ DC Kimario akiendesha mkutano wa ndani na watendaji wa serikali za vijiji wakati akijua kuwa kulikuwa na mkutano wa kampeni za CHADEMA karibu na eneo hilo.

Kulingana na habari hizo, Meneja wa kampeni wa CHADEMA ambaye pia ni mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbai, akifuatana na mbunge wa viti maalum wa CHADEMA, Susan Kiwanga na baadhi ya wananchi na vijana wao ndio waliohusika katika sakata hilo.

Msafara wa Kasulumbai na Kiwanga ulimfuma DC Kimario akiendesha kikao hicho cha ndani katika ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Isakamaliwa na kumtoa nje huku mikufu, bangili, mapambo mengine na simu vyote vya Mheshimiwa DC vikipotea, kudondoka au kuibiwa.

Tuliarifiwa pia kuwa DC alichukuliwa mzobemzobe, akatolewa nje na kuketishwa kwenye kiti na kutakiwa kueleza kuhusu mkutano wake na wale watendaji wa vijiji na kata ambapo aliwajibu kwamba hakuwa na taarifa za mkutano wa kampeni za CHADEMA katika eneo hilo.

Wakati tukitafakari yaliyowakuta CHADEMA mbele ya DC aliyeonekana dhahiri shahiri kufanya mambo kinyume na wakuu wa wilaya wengine, tukapata habari kuwa wabunge wa CHADEMA walikuwa wamefikishwa polisi kutoa maelezo kuhusu vurugu za kumkamata DC huyo.

“Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji wa tathmini kutoka Makao Makuu ya upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issaya Mungulu, alieleza kuwa polisi inawashikilia watu sita na kufungua majalada mawili polisi kuhusu shambulio la aibu na kuingiliwa kwa ratiba ya mkutano wa kampeni,” Mwananchi liliandika juzi.

Tunafahamu sasa kuwa Mungulu alifafanua kwamba jalada moja linahusu mkuu wa wilaya kunyanyaswa na kufanyiwa shambulio la aibu na jalada la pili linahusu CHADEMA wanaodai kuwa ratiba yao ya kampeni iliingiliwa na mkuu wa wilaya kwa lengo la kuvuruga mkutano wao wa kampeni.

Siku ya Jumapili wakajitokeza waandishi na wachambuzi wakieleza tukio la Igunga kila mmoja kwa namna yake lakini aliyetia fora ni mwandishi mmoja aliyedai “CHADEMA hawana haki hata kidogo kisheria kumkamata DC kiupole au kinguvu bila kutumia vyombo vya sheria.”

Kwa maelezo yale, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Rajabu Kiravu, amesema kitendo cha CHADEMA kumkamata mkuu wa wilaya ya Igunga na kumweka chini ya ulinzi wao ni uhuni!

Akizungumza katika kikao kilichoandaliwa Tume hiyo na viongozi wa vyama vya siasa nchini, Kiravu alisema, “Ule ni uhuni tu, kama kosa limetendeka kuna taratibu zake. Ifike mahali watu tuheshimiane, huu utaratibu wa kukamata (wakuu wa wilaya) umetoka wapi?” alihoji Kiravu… 
Sasa maswali: 

  1. Kichwa kizuri cha habari hii kinapaswa kuwa; (a) DC avuliwa hijabu; (b) DC akatikiwa mikufu, shanga, bangili, saa katika purukushani na CHADEMA; (c) DC afumwa akikiuka maadili; (d) CHADEMA wawafundisha polisi namna ya kufanya kazi.
  2. Katika purukushani za kumkamata mhalifu wa kike na ikatokea shanga zikakatika, hijabu ikadondoka na saa ikapotea, kitendo hicho ni; (a) shambulio la aibu; (b) utovu wa adabu wa mkamataji; (c) halali kwa sababu bila hivyo vielelezo havitapatikana; (d) si halali kwa sababu mhalifu mwanamke inabidi akamatwe na mwanamke na hayupo basi aachiwe ‘asepe’ tu.
  3.  Mwandishi wa habari hii ni; (a) mkereketwa wa CCM;  (b) shabiki wa CHADEMA; (c) mpenda haki, amani na utulivu; (d) mtu anayechukia chama cha CUF.
  4. Polisi wa Tanzania ni wabovu kwa sababu; (a) hawatumii akili bali hutii amri yoyote kutoka juu; (b) wanapendelea chama tawala waziwazi; (c) hawawapendi wapinzani; (d) majibu yote a, b na c ni sahihi.
  5. Kwa kuwahukumu CHADEMA kuwa ni wahuni kabla ya kuwasikiliza Rajabu Kiravu ni; (a) Mkurugenzi mzuri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi; (b) Mkurugenzi mzuri wa Tume ya Taifa ya CCM ya Uchaguzi; (c) msimamizi mzuri wa maslahi ya chama tawala; (d) majibu yote ya a, b na c ni sahihi.
  6. DC asiyejua ratiba ya kampeni zinazofanyika wilayani kwake ni; (a) mvivu anayepokea mshahara asioufanyia kazi; (b) mbumbumbu tu wa kazi ya ukuu wa wilaya; (c) mbabaishaji ambaye ni kielelezo cha ubaya wa kuteua watu kwa sababu tu ya ukererekwa wao; (d) mtu safi anayefanikisha matakwa ya chama tawala.
  7. Waandishi na wachambuzi wanaoilaumu CHADEMA kwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu; (a) wanafanya kazi yao vizuri; (b) wanajipendekeza kwa CCM na watawala ili wapate safari na posho; (c) hawajui walifanyalo kwa sababu hawajasoma katiba; (d) mamluki wanaotumiwa na CCM na kuvivurugia vyama vingine.
  8. Jukumu la kumkamata mhalifu ni la; (a) polisi pekee; (b) kila mwananchi; (c) askari yeyote mwenye magwanda na silaha; (d) vyama vya siasa.
  9. Kama anayepaswa kukamata yaani polisi hataki kukamata mhalifu wajibu wa mwananchi wa kawaida ni; (a) kumwachia mhalifu aendelee kuvunja sheria; (b) kumwachia mhalifu aondoke aende zake; (c) kulalamika kwa polisi wale wale wasiotaka kukamata; (d) yote a, b na c si sahihi
  10. Wanaosababisha amani kuvurugika katika kampeni za uchaguzi hapa Tanzania ni; (a) polisi wasiotaka kutenda haki; (b) wasimamizi wa uchaguzi na wakuu wa wilaya wanaofanya kazi kwa upendeleo; (c) viongozi wa ngazi za juu wanaowaamuru polisi kufanya wanavyotaka na siyo polisi walivyoona inafaa; (d) waroho wa madaraka wanaopendelea ccm makusudi kwa matarajio ya kupandishwa vyeo.

Tunaendelea kusahihisha na pindi matokeo yakiwa tayari mtaarifiwa, lakini yaelekea polisi, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa wilaya kama hawakuelewa somo maana wanaelekea kupata maksi chache sana.

0
No votes yet