Chadema yamng'ang'ania Rostam Aziz


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), bado kimeng’ang’ania kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishiriki katika ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Akauti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika amesema hatua ya serikali ya kushindwa kumfikisha mahakamani mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyochota zaidi ya Sh. 40 za EPA kunaitia doa serikali.

“Hapa kuna ‘utatu usio mtakatifu’ kati ya CCM, Kagoda na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz. Hili ndilo linasababisha kampuni ya Kagoda kushindwa kufikishwa mahakamani,” anasema Mnyika.

Mnyika, mwanasiasa kijana na jasiri, anasema kwamba chama chake bado kinaamini kwamba CCM ilihusika na uchotaji fedha ndani ya BoT.

“Sisi bado tunasisitiza kwamba Kagoda ni mali ya Rostam,” anasema Mnyika katika mahojiano yake yaliyochapishwa na gazeti hili.

Akizungumzia tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wa Chadema wana mahusiano na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Mnyika anasema “huo ni sehemu ya mkakati wa CCM kukichafua Chadema.”

Anasema, “Tunaamini kwamba wanaotutuhumu wanatumiwa na wapinzani wetu wa kisiasa. Tunafahamu mahusiano ya karibu yaliyopo kati ya baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi na viongozi wa CCM.”

“Nani asiyejua kuwa Ismail Jusa Ladhu (Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyetuhumu viongozi wa Chadema, ana uhusiano wa karibu na Rostam Aziz?

Jusa aliwahi kusema hivi karibuni kwamba mbunge wa Viti Maalum, Grace Kiwelu, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Fedha Athony Komu, wana uhusiano na watuhumiwa wa ufisadi.

Anasema Chadema haijihangaishi kujibu kauli za Jusa. Inajua kuwa hizo ni kauli za Rostam Aziz ambaye ni mshirika wake na Rostam ni mmoja wa watuhumiwa wakuu.

“Chadema ingejibu kauli hizo kama zingekuwa zimetolewa na Kiongozi wa Upinzani bungeni Hamad Rashid, au Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba au Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad.

Anasema wanapata nguvu zaidi kutokana na mahojiano ya Jusa kuchapishwa katika gazeti la Rai wiki mbili zilizopita. Gazeti hilo linamilikiwa na Rostam.

Hata hivyo, Mnyika anakiri kwamba Kiwelu na Komu wana uhusiano wa kifamilia na Esther Komu ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa fedha BoT.

Anasema pia kwamba Zitto ana uhusiano wa karibu na kiongozi wa CCM, Rajabu Maranda, ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa katika kesi hiyohiyo.

Kuhusu matumizi ya fedha kutoka nchi za nje, Mnyika anasema siyo sahihi kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za kila siku kwa fedha kutoka nje.

“Chadema hakipokei fedha kutoka nje kwa ajili ya kujiendesha. Chama chetu kinaendeshwa kwa ruzuku ya serikali na michango ya wanachama,” amesisitiza.

Anasema, hata hivyo, kuwa wanachama na viongozi ndio wachangiaji wakuu wa chama na kwamba wabunge wa Chadema wamekuwa wanachanga fedha kila mwezi kutoka kwenye mishahara yao ili kuendesha chama.

“Fedha tunazopata kutoka nje, tunazitumia kwa mafunzo ya viongozi wa ngazi mbalimbali. Haziwezi kuendesha shughuli za kila siku za chama. Kwanza, ni kidogo, lakini pia siyo sera ya Chadema wala wale wanaozitoa,” anafafanua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: