CHADEMA yamtega tena JK


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete aweza kukitosa tena Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuhusu uundwaji wa katiba mpya, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya serikali zinasema Rais Kikwete anaweza kukitosa CHADEMA, iwapo atashindwa kuwa imara kupambana na wahafidhina ndani ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vyanzo vya taarifa kutoka serikalini vinasema, katika mkutano kati ya Rais Kikwete na ujumbe wa CHADEMA uliofanyika ikulu jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, rais alionekana kushawishika na hoja za CHADEMA za kutaka sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ifanyiwe marekebisho makubwa.

Katika mkutano huo, CHADEMA kiliongozwa na viongozi wake wakuu wa kitaifa, akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na katibu mkuu, Dk. Willibrod Slaa. Wajumbe wengine katika ujumbe wa CHADEMA, ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari, Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, John Mnyika, mbunge wa Ubungo, Said Arfi, makamu mwenyekiti na mbunge wa Mpanda Kati na John Mrema.

Hii ni mara ya pili kwa CHADEMA kukutana na Rais Kikwete na kujadiliana mambo kadhaa, ikiwamo kutosainiwa kwa sheria inayounda tume ya kukusanya maoni. Hata hivyo, Rais Kikwete alisaini sheria hiyo kwa madai kuwa alihofia kusakamwa na wabunge wa chama chake.

Tayari CHADEMA kimeonya kuwa ushiriki wake “katika mchakato mzima wa kupata katiba mpya uliowekwa na sheria ya mabadiliko ya katiba, utategemea utayari wa serikali ya Rais Kikwete…”

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa juzi Jumatatu mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa CC imesema, “…kufanyika kwa mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo, ndiyo njia pekee ya kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa gazeti hili, muundo mpya kwenye tume ya kukusanya maoni ambao rais Kikwete ameona kuna haja ya kufanyiwa marekebisho, unahusu upatikanaji wa wajumbe wa tume; ambapo sasa rais hatateua moja kwa moja wajumbe hao bila kwanza kupitishwa na taasisi wanazotoka.

“Sheria iliyopitishwa na Bunge na ambayo CHADEMA waliilalamikia, inampa mamlaka rais kuteua wajumbe wa tume kwa kushauriana na kubaliana na Rais wa Zanzibar tu. Hii ina maana kwamba rais anaweza kuteua mtu yeyote anayemuona anafaa, bila ya kulazimika kushauriana na taasisi anazotoka au matakwa ya wanaodaiwa kuwawakilishwa,” anasema mjumbe mmoja kutoka ndani ya mkutano huo.

Anasema, “Lakini katika mabadiliko mapya ambayo yanatarajiwa kufanywa na Bunge lijalo na ambayo Rais Kikwete ameona umuhimu wa kuingizwa kwenye sheria, ni kwamba rais kulazimika kushauriana na asasi za kijamii, vyama vya siasa na mashirika mengine ambayo yatatoa wawakilishi, kabla ya kufanya uteuzi.”

MwanaHALISI limeelezwa kuwa mabadiliko hayo ambayo yametajwa, yamo kwenye Ibara ya 6 (1) ya sehemu ya tatu inayohusu uundaji wa tume.

Ibara hiyo inasema, “Rais baada ya kushauriana na kukubaliana na rais wa Zanzibar atateua mwenyekiti wa tume, makamu mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo.

Lakini CHADEMA wamemweleza Rais Kikwete umuhimu wa kurekebisha ibara hiyo kwa kuweka sharti jipya linalotaka rais kuteua wajumbe kutoka kwenye orodha iliyowasilishwa kwake na asasi zilizotajwa kwenye sheria husika.

Inaelezwa ujumbe wa CHADEMA ulisisitiza umuhimu wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo kutofanywa moja kwa moja na rais kwa madai kuwa kuteuliwa kwa mfumo huo, kutawafanya wajumbe kuwajibika moja kwa moja kwake; na kutoa matokeo yatakayompendezesha rais au chama chake.

Aidha, hoja nyingine ya CHADEMA ni katika ibara ya 5 (a) inayoweka sifa za mtu anayetakiwa kuwa mjumbe wa tume ya kurekebisha katiba.

Inaelezwa na mtoa taarifa, CHADEMA kimemshauri Rais Kikwete kufanyiwa marekebisho yatakayoruhusu viongozi wa vyama vya siasa kuruhusiwa kuingia kwenye tume ya kukusanya maoni, isipokuwa wabunge na madiwani.

Mtoa taarifa anataja hoja nyingine iliyowasilishwa na CHADEMA, ni juu ya nafasi ya Zanzibar na Rais wa Zanzibar katika upatikanaji wa katiba mpya. Wakati sheria inasema, tume ya kukusanya maoni itaundwa na rais “kwa kushauriana na kukubaliana na rais wa Zanzibar,” CHADEMA walipendekeza rais wa Zanzibar kufanywa mshauri badala ya kutajwa kuwa “afikie makubaliano.”

Ni katika hoja hii, taarifa zinasema, Rais Kikwete aliwahakikishia viongozi wa CHADEMA kuwa wasiwe na hofu ya kuwapo kikwazo au misuguano kati yake na rais wa Zanzibar,” inaelezwa.

Rais Kikwete amenukuliwa akisema yeye na rais wa Zanzibar wamefanyakazi pamoja kwa muda mrefu; anamheshimu na wamekubaliana katika suala zima la upatikanaji wa katiba mpya itakayoshirikisha wananchi wote.

Hoja ya uhuru katika ukusanyaji wa maoni, inaelezwa ndiyo ilizua mvutano mkubwa baada ya CHADEMA kutaka kuwapo uwazi na uhuru mkubwa wa kutoa maoni.

“Hapa ndipo karibu viongozi wote wa CHADEMA waling’ang’ania hasa. Kwa mfano, Mbowe alisema, “Ni lazima kuwapo kwa uhuru mkubwa wakati wa kutoa maoni, vinginevyo sote sisi tutakamatwa, kushitakiwa na kufungwa,” alieleza Mbowe.

Alisema, “Sheria iliyopo haikidhi haja ya kuwapo uhuru huo, na kwamba inaonekana wazi itapendelea waliopo madarakani. Ninyi wenzetu hamjali kwa sababu, hamtakamatwa wala kushitakiwa.”

Akinyooshea kidole William Lukuvi, mjumbe kutoka kamati ya serikali, Mbowe alisema, “…mheshimiwa Lukuvi kwani ninyi hamfanyi makosa? Ninyi malaika, mbona hamkamatwi?”

Mtoa taarifa anasema, “Naye Profesa Baregu akichangia hoja hiyo huku akisema kwa msisitizo alitaka kuondolewa kwa wakuu wa wilaya katika usimamizi kwenye elimu ya uhamasishaji, jambo ambalo rais Kikwete aliona ni jema.”

Akimnukuu Profesa Baregu, mtoa taarifa anasema, “…Ni lazima wakuu wa wilaya waondolewe kutokana na kufanyakazi kama wale wa ukoloni.”

Kifungu kingine ambacho Rais Kikwete aliona kuna haja ya kufanyiwa marekebisho, ni kile kinachohusu adhabu kwa watu watakaopatikana na hatia ya kufanya mikutano kinyume na sheria inayounda tume. Hapa adhabu imetajwa kuwa ni kifungo cha miaka 5 hadi 7 gerezani au faini ya hadi Sh. 5 milioni.

Katika eneo hili, mtoa taarifa anaeleza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, aling’ang’ania adhabu hiyo kubaki kama ilivyo. Lakini Rais Kikwete baada ya kusikiliza kwa makini hoja za Lissu, na Profesa Safari, aliona mantiki ya hoja ya CHADEMA na hivyo kuonyesha kuikubali. Inaelezwa kuwa rais aliagiza Jaji Werema kuingiza marekebisho ya kuondoa au kupunguza adhabu kwenye kifungu hicho.

Mbali na muundo tume ya kukusanya maoni juu ya uundaji wa katiba mpya, CHADEMA wameshinikiza serikali kufanyika marekebisho kwenye kifungu kinachohusu uundwaji wa Bunge la Katiba.

Taarifa zinaeleza muswada wa kuifanyia marekebisho sheria ya kuundwa kwa Bunge la katiba itawasilishwa kwenye mkutano wa Bunge wa Aprili mwaka huu.

Nayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia zoezi la kura ya maoni Rais Kikwete ameona umuhimu wa kufanyiwa marekebisho makubwa ya kisheria, kabla ya zoezi hilo kufanyika.

Awali taarifa zinasema, Dk. Slaa alinukuliwa akimueleza rais Kikwete, “…nimekuja kukuona mheshimiwa rais, maana watu wanasema kuwa mimi nimekukimbia. Nikukimbie kwa nini,” alisema Dk. Slaa, huku wajumbe waliokuwapo wakiangua kicheko.

Naye rais Kikwete, akijibu hoja ya Dk. Slaa alisema, “…hawa akina michuzi (akimnyooshea mpiga picha wa ikulu, Muhidini Issa Michuzi)…wanapenda kutia chumvi.”

Mara baada ya kauli hiyo ya Dk. Slaa na majibu ya rais Kikwete, mkutano ulianza rasmi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: