CHADEMA yang’ara


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Joseph  Kashindye mgombea wa CHADEMA

UCHAGUZI mdogo katika jimbo la Igunga ukifanyika leo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitaibuka mshindi, uchunguzi uliofanywa na MwanaHALISI umeeleza.

Kwa wiki mbili sasa, gazeti hili limekuwa likifuatilia mipango ya vyama, taratibu, kampeni zilizoanza wiki mbili zilizopita, mwitikio wa wananchi; pamoja na kufanya mahojiano na wapigakura, viongozi wa vyama husika na asasi za kijamii jimboni.

Gazeti limefanya mahojiano katika kata zote 26 za jimbo la Igunga na kugundua wapi chama kipi kina nguvu na uwezekano wa kushinda kwa kura nyingi na wapi pa kupoteza katika uchaguzi wa tarehe 2 Oktoba.

Vyama vinane vya siasa vinashiriki uchaguzi Igunga kutafuta mbunge wa kuziba nafasi iliyoachwa na Rostam Aziz ambaye wakati anatangaza kujiuzulu, alikejeli chama chake akisema kimezidi kwa “siasa uchwara.”

Lakini ni Rostam aliyebebana na rais mstaafu Benjamin Mkapa kufungua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Igunga.

Taarifa zinaonyesha CHADEMA kukubakika zaidi katika kata saba zilizopo katika maeneo ya mijini na ambazo zinabeba karibu nusu ya wapigakura wote.

Kata ambazo CHADEMA inakubalika, ni Mwisi, Nkinga, Ziba, Igurubi, Choma, Igunga na Nsimbo.

Katika eneo hilo la kata saba, hojaji zimeonyesha CHADEMA inaweza kupata kati ya asilimia 60 na 65 ya kura zote zitakazopigwa, CCM asilimia 25 hadi 32 na Chama cha Wananchi (CUF) kati ya asilimia nane hadi 10.

Haya ni maeneo ambako wananchi wengi wana ufahamu mkubwa juu ya utawala; wanafahamu matatizo ambayo taifa hili linakabiliwa nayo; na miongoni mwao kuna wanaodiriki kusema kwa sauti ya juu kwamba “matatizo yetu yamesababishwa na CCM.”

Katika eneo hili, kwa karibu kila wananchi 10 waliokuwa wakiulizwa watapigia kura mgombea wa chama gani, sita walitaja CHADEMA.

Hivyo basi, katika eneo hili, haitarajiwi CCM kikapata kura nyingi ukilinganisha na upinzani na hususani CHADEMA,” ameeleza “Hata CCM wanaonekana kutaka mabadiliko,” anasema Christopher Iboro, mmoja wa wapigaakura watarajiwa.

Anasema, “Wananchi wengi wanaifahamu CCM tokea wakati wa Rostam Aziz. Ndiyo maana pamoja na yeye na chama chake kutumia mamilioni ya shilingi katika uchaguzi mkuu uliopita, lakini wananchi walimpa mgombea wa upinzani zaidi ya kura 11,000. Hii ni ishara tosha kwamba hali ya CCM hapa Igunga, si ya kujivunia sana.”

Wagombea katika uchaguzi huo, ni Leopold Mahona (CUF), Joseph Kashindye (CHADEMA), Dk. Peter Kafumu (CCM) na Magid Maguma (SAU). Vyama vingine vilivyosimimisha wagombea jimboni Igunga, ni United Democraty Party (UDP), Chausta, UPDP na Democratic Party (DP).

CCM ina mvuto wa wastani katika meneo ya vijijini hasa Kaskazini mwa Igunga ambako wananchi wake wengi ni kutoka jamii ya wafugaji.

Maeneo ambako hojaji zimeonyesha ndiko kimbilio la CCM ni tarafa ya Igurugi yenye kata za Itunduru, Mamashimba, Kingingirina, Itumba, Mbembezi na Mbutu.

Ni huko ambako hojaji zimeonyesha CCM inaweza kupata kati ya asilimia 60 na 65 ya kura zote. Hojaji zinaonyesha CHADEMA yaweza kupata asilimia 30 hadi 32 na CUF kati ya asilimia tatu hadi tano.

Katika eneo hili, upinzani ungali mchanga na baadhi ya waliohojiwa wamekiri kutofahamu hata baadhi ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi.

Aidha, haya ni maeneo yenye umasikini mkubwa wa kipato, jambo ambalo linaweza kuwa msingi wa hoja za upinzani unaotafuta kura kwa udi na uvumba.

Nyumba za wananchi, jinsi wanavyovaa na mwonekano wa afya zao, vinaashiria kutokuwepo ufahamu mpana wa shughuli za kisiasa – ama kwa woga au kwa umasikini na elimu ya wapigakura haijaweza kupenya.

Ni katika maeneo haya ambako kati ya watu 10 waliohojiwa, sita walisema wataipigia CCM kwa kuwa “tumekuwa na chama hiki.”

Hii inaonyesha kuwa wamekuwa wakipata ujumbe wa chama kimoja; bali wakipata fursa ya kusikiliza wengine, wana uwezekano wa kufanya maamuzi tofauti.

Wahojaji wa MwanaHALISI wameelezwa kuwa katika kata nane nyingine, baadhi ya wapigakura wanaipa nafasi kubwa ya ushindi CHADEMA.

Huko ni katika eneo lenye kata za Nyandekwa, Mwamashiku, Mwamashimba na Manga, ambako maoni ya wananchi yamempa mgombea wa CHADEMA asilimia 46, CCM asilimia 40 na CUF asilimia 12.

Kwa maoni haya, iwapo hali itaendelea kuwa kama ilivyo sasa (Jumamosi iliyopita), CHADEMA yaweza kupata ushindi wa jumla wa kati ya asilimia 52 na 55, huku CCM ikivuna asilimia 42 hadi 46 na CUF ikipata kati ya asilimia 5 na 10. Vyama vingine vilivyosalia haviwezi kupata zaidi ya asilimia 1 ya kura. 

Hata hivyo, mazingira ya uchaguzi yaweza kubadilika kwa kadri siku zinavyosogea mwisho kwa vyama kueleza vema sera zao na jinsi wagombea watakavyofanikiwa kuwafikia wananchi na wengine kujitetea kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Kwa mfano, Dk. Kafumu atalazimika kujikita zaidi kujibu madai ya kwamba yeye ni miongoni mwa watu waliolifikisha taifa hili hapa lilipo, kutokana na hatua yake ya kushiriki moja kwa moja au kwa kunyamazia mikakataba tata ya madini nchini.

Wakati wa mkutano wa Bunge la bajeti, mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alilitaja jina la Kafumu mara sita akisema amewathamini zaidi wawekezaji kuliko wananchi wake.

“Kwa jumla pamoja na rabsha za hapa na pale, mpaka sasa kampeni zinakwenda vema. Wananchi wengi wamehamasika kujitokeza siku ya uchaguzi ili kuchagua mabadiliko. Kile ambacho wengi hawakifahamu, ni iwapo uchaguzi huu utafanyika katika mazingira huru na haki,” ameeleza Juma Ismaili, mkazi wa Igunga.

Katika uchaguzi huo wa Oktoba, CCM inakabiliwa na tatizo kubwa la kuwapo makundi ndani yake, jambo ambalo limesababisha kutokuwapo hadi sasa, kwa baadhi ya viongozi mashuhuri wa chama hicho.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa wameshindwa kushiriki kampeni za Igunga kutokana na kushamiri kwa makundi, ni Katibu Mwenezi, Nape Nnauye, Samwel Sitta na John Chiligati.

Nape na Chiligati wameshindwa hata kuhudhuria kikao cha sekretariati ya CCM kilichofanyika Ingunga mwishoni mwa wiki ili kutekeleza kile kinachodaiwa kuwa ni “kutimiza mashari yaliyowekwa na Rostam.”

“Hata umoja wa wabunge wa mkoa wa Tabora umeparaganyika. Wabunge wamejengeana chuki kubwa kiasi ambacho wengine wamefikia kutoamkiana. Kilichobaki kwa sasa ni kila mmoja vyake,” anaeleza mmoja wa wabunge wa CCM mkoani Tabora.

Anasema, “Kikubwa kilichowafikisha hapo, ni tambo za pande mbili zinazotokana na makundi mawili yanayovutana toka uchaguzi mkuu uliopita, pamoja na dhana ya kujivua gamba.”

Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinadai kampeni hizi zitakapomalizika, CCM itakuwa imetumia mabilioni ya shilingi, kutokana na kampeni zake kuendeshwa na viongozi waastafu wanaolipwa kiasi kikubwa cha posho, jambo ambalo limewasababishia baadhi ya wananchi kuona chama hicho kiko mbali nao.

Aidha, kuwepo kwa viongozi hao kumeshindwa kukisaidia chama hicho kutokana na wengi kutokuwa na mvuto kwa vijana ambao ndio wapigura wengi.

“Hata kuwapo kwa Mkapa hakukukisaidia sana chama chetu. Yeye alikuwa anahubiri mambo ya mwaka 47, wakati wananchi wanataka mambo ya sasa. Wananchi wanajua fedha za EPA ziliibwa wakati wake, sasa kuwaambia kwamba nchi ina maendeleo, walikuwa wanamuona kama anawatania,” ameeleza kiongozi mmoja wa CCM kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Swali: Kwa kauli yako hiyo, unaonekana utachagua upinzani.

Jibu: Hiyo ni siri yangu.

Swali: Lakini wananchi wanakufahamu kuwa ni mpinzani moyoni na mwanachama wa CCM kijuujuu?

Jibu: Hayo nitajua mwenyewe.

Swali: Kwa hiyo utapigia CHADEMA?

Jibu: Sitaki kupoteza kura yangu. Iwe CCM au CHADEMA, nataka kupigia washindi. Nitaangalia.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, hatua ya CCM kuwatumia wastaafu badala ya vijana wake mahiri, imeidhoofisha kwa kiasi kikubwa.

Habari zinasema kwa kutambua udhaifu huo wa CCM, CHADEMA imeamua kupeleka kuanzia leo, Jumatano kile kinachoitwa “majeshi ya ardhini” yatayoongozwa na naibu katibu mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, Zitto Kabwe, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, mbunge wa Ubungo, John Mnyika na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Aidha, viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, wanatarajiwa kutua Igunga wiki moja kabla ya kufungwa kwa kampeni.

0
No votes yet