CHADEMA yatambia umati wa wafuasi wake


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Umati kampeni za CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetamba kuwa kitashinda katika uchaguzi huu kwa kuwa wananchi wengi wanataka mabadiliko.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu amesema, “Tuna uhakika wa kushinda nafasi ya urais na tuna uhakika kupata zaidi ya nusu ya wabunge.”

Katika mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake jana, Prof. Profesa Baregu amesema chama chakekitashinda kwa kuwa kimesimama na kizazi kipya kinachosema “Hatudanganyiki.”

“Hawa wamelelewa katika mabadiliko; ni jasiri na wang’amuzi. Wako tayari kulinda na kutetea kile wanachokiamini,” amesema.

Prof.Baregu amesema tofauti na chaguzi zilizopita, Watanzania wa sasa wameonyesha shauku ya kutaka mabadliko na kwamba hilo ndilo linawapa imani.

Amesema katika nchi yoyote, kitu kinacholeta mabadiliko ni wananchi wenyewe kuyataka; na kazi ya vyama vya siasa ni kuwapa mbadala wa chama kilichopo madarakani.

“Wananchi kote tulikopita, wameonyesha kutaka mabadiliko. Wanavaa sare za chama na kubeba bendera hadharani. Haya mambo hayakuwapo katika siku za nyuma. Tanzania iko tayari kwa mabadiliko,” amesema.

Alisema kama kuna ushindi mkubwa ambao upinzani umepata mwaka huu, ni ule wa kuwafanya wananchi waondoe hofu waliyonayo kwa CCM na dola kwa jumla.

“Vizazi vinabadilika. Kile kilicholelewa na kukulia katika mazingira ya chama kimoja, taratibu kinabadilishwa na kizazi kipya cha vijana ambao wengine wanapiga kura kwa mara ya kwanza mwaka huu,” ameeleza Baregu.

Amesema nguvu ya umma ndiyo tegemeo letu na ni nguvu hiyohiyo itakayotubeba kwenye uchaguzi huu,” amesema.

Prof. Baregu amesema CHADEMA ina matumaini ya kufanya vizuri kwa vile mgombea wao wa urais, Dk. Willibrod Slaa amefika katika maeneo mengi na kufanya mikutano ya hadhara zaidi ya 500 nchini kote.

Kuhusu suala la CHADEMA kupunguza bei za saruji na mabati kwa kiwango kikubwa ambalo limezua mjadala nchini, Prof. Baregu amesema ahadi hiyo ya Dk. Slaa inatekelezeka.

Amesema kitu kikubwa ni kipaumbele. Kama serikali itaamua kuwajali raia wake na kuhakikisha wanaishi na kulala kibinadamu, hilo linawezekana.

“CHADEMA itaondoa kodi katika bidhaa hizi na hili litasaidia kushusha bei. Kinachofanya saruji na mabati yauzwe kwa bei kubwa ni kodi. Lakini serikali inaweza pia kuamua kutoa ruzuku kwa makampuni yanayotengeneza bidhaa hizi,” amefafanua.

Prof. Baregu amesema wananchi wakipata mahalipazuri pa kuishi, “tutakuwa tumeua ndege wawili kwa jiwe moja; yaani kwa watu kuishi pazuri, serikali itapunguza magonjwa na kukuza elimu. CHADEMA inaweza. CCM hawana ubunifu; watupishe.”

Kuhusu elimu, Baregu amesema CHADEMA ina uwezo wa kutoa elimu bora kwa wananchi wote ba bila kuwatoza kodi..

“CCM ndio waliosema haiwezekani kutoa elimu bure. Baada ya sisi kusema inawezekana, umewasikia sasa wanasema eti elimu bure ni sera yao. Kazi yao hawa ni kuiga. Hawana ubunifu na ni vema wakawaachia wenye ubunifu waongoze nchi hii,” amesema.

Kuhusu siasa za ushindani nchini, Prof. Baregu amesema uchaguzi wa mwaka huu umedhihirisha kwamba bado hakuna ulinganifu katika siasa za ushindani nchini baina ya CCM na upinzani.

Akitoa mfano, amesema katika uchaguzi huu, zipo taarifa za mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete pamoja na wagombea wengine wa nafasi za ubunge kutumia raslimali za serikali katika kampeni.

Amesema upinzani unashindana na CCM ambayo imewazidi mno kiraslimali na kwa ushawishi serikalini na katika vyombo vya dola, jambo linaloondoa ushindani wa kweli katika siasa.

Katika mazingira ya namna hii, uwanja wa ushindani hauko sawia baina ya CCM na upinzani. Hili ni miongoni mwa matatizo makubwa katika kampeni za mwaka huu.

Amesema uzoefu mkubwa walioupata katika kampeni za mwaka huu ni kuwa CCM haikuwa imejiandaa na aina ya ushindani uliojitokeza baada ya Dk. Slaa kujitokeza kuwania urais.

“Wamepata kiwewe. Ndiyo maana kuna kipindi waliamua kuanza kufanya siasa za majitaka, kama kushambulia mgombea kuhusu mambo ya binafsi kama utashi wa uchumba na ndoa. Ile ilikuwa dalili ya kuingiwa kiwewe,” ameeleza.

Kuhusu tishio la uchakachuaji matokeo katika uchaguzi wa mwaka huu, Baregu amesema tishio hilo liko wazi na tayari wameanza kuchukua hatua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: