CHADEMA yatambia ushindi: Yasuta CCM kutumia silaha kupiga kura


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa anasema chama chake hakikushindwa   uchaguzi. Anasema kimeshinda, tena kimepata ushindi mkubwa.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Dk. Slaa anasema, “Kuanzia Sumbawaga, mkoani Rukwa, Kinondoni, Dar es Salaam, Ilemela, mkoani Mwanza hadi Karatu, mkoani Arusha, kote huko matokeo yametangazwa siku mbili baada ya matokeo ya awali kutangazwa tena chini ya usimamizi wa askari wa jeshi la polisi.”

Anasema katika mazingira hayo ya kushindana na dola, badala ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama chake “hakikushindwa uchaguzi. Bali kimeshinda.”

Akiongea kwa kujiamini Dk. Slaa anasema,  “Tuko hai. Umma unatuunga mkono. Na hili limeonekana wazi katika uchaguzi huu, kwamba pamoja na CCM kutumia dola kubaki madarakani, upinzani kwa ujumla umefanya vizuri ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2004.”

Katika mazingira ya CCM kutumia polisi kujitangazia ushindi, kwa kupora ushindi mchana kweupe, na katika mazingira ya kumtumia Waziri wa TAMISEMI kujitangazia ushindi, “CCM hakiwezi kujitapa kwamba kimeshinda upinzani,” amesema.

Anasema CCM kilitumia polisi, watendaji wa serikali na hata Waziri wa Serikali za Mitaa, Celina Kombani “kuamrisha wakurugenzi wa halmashauri kutangaza ushindi kwa wagombea wake.”

“Tunasema haya tukiwa na ushahidi wa kutosha na uwezo wa kuyathibitisha mahali popote pale,” anasisitiza.

Dk. Slaa alikuwa akijibu pamoja na mambo mengine hoja iliyoibuliwa wiki iliyopita na mwasisi wa mageuzi nchini, Mabere Marando, kwamba vyama vya upinzani vimetia aibu katika uchaguzi huu.

Kilio cha Marando kilitokana na hatua ya vyama hivyo kushindwa kusimamisha wagombea katika baadhi ya maeneo na hivyo kukifanya CCM kupita bila kupingwa.

Katika hilo, Dk. Slaa anasema, “Nimesoma maelezo ya Marando. Namheshimu. Baadhi ya hoja zake nakubaliana nazo. Yale mema aliyotushauri tunayafanyia kazi.”

Lakini muhimu hapa ni kwamba hata yeye (Marando) anajua jinsi tulivyofanya kazi katika mazingira magumu. Anafahamu kwamba uchaguzi umevurugwa kwa makusudi na CCM na serikali yake.”

Anasema, “Kama wameshinda baada ya kuleta polisi, kama wameshinda baada ya kupiga risasi wagombea wetu kama walivyofanya Buselele kule Chato, Biharamulo Magharibi, basi hakuna ushindi.”

Kama wameshinda kwa kutumia mizengwe na vitisho, halafu wanajitapa kwamba wameshinda, “mimi nadhani CCM kinahitaji kutibiwa.” Anasema CCM hakikushiriki uchaguzi, bali dola ndiyo iliyokuwa inapambana na vyama vya upinzani.

Anasema katika wilaya yake mkurugenzi wa halmashauri ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi alikuwa anapokea amri na maagizo kutoka kwa katibu wa CCM wa mkoa, Mery Chitanda. Hata hivyo, anajitapa kwamba pamoja na vurugu zote hizo, chama chake kimeshinda katika maeneo mengi.

“Pale Karatu CCM ni chama cha upinzani. Kuanzia halmashauri ya wilaya hadi katika vijiji na vitongoji. Katika baadhi ya maeneo wameweza kupata wenyeviti wa vijiji, lakini sisi tukiwa ndiyo wenye wajumbe wengi zaidi ya wao. Haya si mafanikio haba. Ni mafanikio makubwa sana,” anasema.

Dk. Slaa anasema hata katika maeneo ambayo CCM inajitapa kwamba imeshinda bila kupigwa, baadhi ya maeneo hayo wagombea wa upinzani waliondolewa kwa hila na mizengwe.

Anataja mfano hai wa jimboni kwake Karatu, akisema baadhi ya wagombea “waliondolewa kwa shinikizo la waziri Kombani.”

Anasema baadhi ya vigezo vilivyotumika  kuwaondoa havikuwa halali na kwamba katika baadhi ya maeneo wamepanga kwenda mahakamani kutafuta haki.

Kwa mfano, Dk. Slaa anasema kwamba katiba za vyama zimekiukwa na wasimamizi wa uchaguzi pale walipoamrisha kuwa wagombea sharti wateuliwe na ngazi ya shina.

“Hili si jambo sahihi. Mwenye uwezo wa kuamua ngazi ya uteuzi ni chama chenyewe. Lakini haya ndiyo yaliyofanyika kuanzia Sumbawaga, hadi Lindi,” anasema kwa sauti ya masikitiko.

Jingine analolitaja kuwa lilichangia chama chake kushindwa katika baadhi ya maeneo ni wagombea wake kukataliwa kuchukua fomu za kugombea hata pale muda ulipoongezwa na serikali, lakini hapohapo msimamizi wa uchaguzi akiruhusu wagombea wa CCM  tu kuchukua fomu.

“Pale Karatu Njiapanda, Buger na Kambi ya Nyoka, wagombea wa CCM waliruhusiwa kuchukua fomu na kurejesha kwa maelekezo ya Kombani. Sasa katika mazingiara hayo, nani anaweza kusema kuwa CCM imeshinda uchaguzi,” anahoji.

Tangazo la awali lilitolewa na serikali halikuwa limeonyesha muda wa kurudisha fomu. Lilizungumzia ratiba ya uchaguzi.

Alipoulizwa uchaguzi huo umetoa fundisho gani kwake na chama chake, Dk. Slaa alijibu haraka: “Fundisho ni moja. Kwamba serikali hii haitaki kuheshimu demokrasia ya wengi.”

Anasema anachokiona ni kwamba “serikali haitaki kuona taifa hili linaendelea kuwa la amani, na kwamba haitaki kuona wananchi wanatumia haki yao ya asili kuweka kiongozi wamtakaye.”

Akiongea kwa uchungu, Dk. Slaa anasema dalili anazoziona ni kwamba CCM na serikali yake wanataka kuingiza nchi katika machafuko. “Hizi ni dalili za nchi kuingia katika machafuko. Na CCM tukifika huko isilaumu mtu, bali ijilamu yenyewe,” anaasa.

Kuhusu sakata la posho mbili kwa wabunge, Dk. Slaa anasema hiyo ni dalili ya kuwa na serikali dhaifu, isiyojali na inayolea rushwa; likifuatiliwa kwa karibu litaumbua wengi.

Hata hivyo, Dk. Slaa anasema kiini cha wabunge na watumishi wengine wa serikali na mashirika ya umma kulipwa posho mbili kwa wakati mmoja, ni kuwapo kwa serikali dhaifu.

Kwa mfano, anasema katika bejeti ya serikali hasa katika fungu la safari za mawaziri, kuna pakeji ya mafuta ambayo kwa ajili ya waziri kwenda katika jimbo lake la uchaguzi.

Anasema, “Lakini kila mbunge, wakiwamo mawaziri, wanapewa fedha na bunge kila mwezi. Lakini mawaziri wengi hutumia magari ya serikali kwa safari binafsi.

Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi, Dk. Slaa anasema hakuna maendeleo makubwa sana, ingawa anasema anafurahi kuona wananchi wengi hivi sasa wanachukia ufisadi kuliko ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita.

Anasema yeye na chama chake wamejiandaa iwapo serikali haitaleta ripoti ya utekelezaji ya maagizo ya Bunge kuhusu mkataba tata wa Richmond, kwenda katika kila kijiji kueleza wananchi kwamba “serikali yao inakumbatia ufisadi.”

“Bunge si mahali pa mwisho. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri mamlaka ya mwisho ya serikali ni wananchi. Hivyo sisi tutakwenda huko kuwaambia kwamba serikali yenu imeshindwa kusimama nanyi, badala yake imebeba mafisadi na kuwalea,” anasema.

Anasema anaamini kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza wajibu wao kwa taifa.

Alipoulizwa watawezaje kufika kila wilaya katika kipindi hiki kifupi wakati nchi ni kubwa, mbunge huyo wa Karatu alijibu, “Si mnatujua. Basi tutafika kila pembe ya nchi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: