CHADEMA yaumbua Pinda


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Yataka afute kauli yake bungeni
Hatima yake mikononi mwa spika
Spika Makinda kumfichia aibu
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

USHAHIDI wa CHADEMA, kuthibitisha jinsi Waziri Mkuu Mizengo Pinda “alivyodanganya bunge,” umesheheni vielelezo ambavyo vinaweza kumjeruhi kisiasa – yeye binafsi na serikali yake.

Jumatatu wiki hii, mbunge Godbless Jonathan Lema (CHADEMA) aliwasilisha kwa spika hoja kumi zenye lengo la kuthibitisha kuwa Pinda alidanganya bunge na taifa alipokuwa akijibu hoja juu ya mauaji ya Arusha.

Lema alikuwa anatekeleza amri ya Spika Anna Makinda aliyotoa Alhamisi iliyopita katika kipindi cha maswali na majibu ya papohapo kwa waziri mkuu.

Wakati Lema aliomba mwongozo wa spika juu ya hatua gani zinaweza kuchukuliwa kwa kiongozi kama waziri mkuu iwapo atakuwa amedanganya bunge na taifa, Makinda alijibu kwa kishindo na kumtaka mbunge atoe uthibitisho kuwa Pinda alisema “uwongo.”

Majibu ya Lema, ambayo yameandaliwa kisheria na wataalam wa chama hicho, yanatajwa kuwa makini, sahihi na yenye ushawishi kwa wabunge, hata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi kwa jumla, kiasi kwamba huenda spika asiyatoe hadharani.

Miongoni mwa hoja kumi kuna inayohusu madai ya waziri mkuu kwamba, kwa vile CHADEMA ilikuwa na madiwani 14 na CCM ikiwa na madiwani 16, hivyo ilikuwa wazi kwamba CCM wangeshinda umeya Arusha. Pinda alisema hata mtoto wa darasa la tatu angeweza kuelewa hesabu hiyo.

Lakini katika majibu ya CHADEMA, kwanza wanaonyesha kuwa wao hawakuwa kwenye ukumbi; hivyo waziri mkuu alidanganya. Pili, walitoa mfano wa naibu meya aliyetoka Tanzania Labour Party (TLP).

Katika majibu wanasema TLP ina mjumbe mmoja huyohyo aliyechaguliwa kuwa naibu. Kama yeye aliweza kuchaguliwa akiwa mmoja tu, vipi Pinda analeta hoja ya madiwani 14 kutopata wengine wa kuwaunga mkono wakati kura ni ya siri.

CHADEMA wanatoa mfano wa halmashauri ya Hai ambako walikuwa wachache, lakini katika uchaguzi wa siri waliibuka washindi kwa kuwa na mwenyekiti. Wanarudia kauli ya Pinda kuwa hata mtoto wa darasa la tatu angeweza kuelewa hilo.

Hoja nyingine ni kwamba Pinda alisema uwongo pale alipoliambia bunge kuwa Watanzania watatu walikufa katika sekeseke la Arusha. CHADEMA wanasema huo ni uwongo kwa kuwa Watanzania waliokufa ni wawili – Dennis Michael Shirima na Ismail Omari; mwingine alikuwa Mkenya – Paul Njuguna. Uwongo.

Kwa kusema uwongo, CHADEMA wanaeleza, Pinda aliliambia bunge kuwa waliamua kufanya maandamano bila kujali utaratibu uliokuwa imekubaliwa kati yao na polizi.

Lakini kauli ya waziri mkuu inapingana na taarifa rasmi ya jeshi la polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011 ikisema polisi walichukua hatua ya kusitisha maandamano “baada ya kuona kwamba yataleta uvunjifu wa amani kutokana na jazba ya waandamanaji…”

Pinda aliliambia bunge kuwa waandamanaji walikataa kutumia njia moja waliyopewa na polisi. CHADEMA wanasema huo ni uwongo.

Wanasema ukweli ni kwamba, 31 Desemba 2010, mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Arusha Mjini alitoa taarifa ya maandishi kwa mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha Mjini yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20/10 iliyobeba kichwa cha habari kisemacho: “Taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara tarehe 5 Januari 2011.”

CHADEMA wanasema waziri mkuu alisema uwongo bungeni kwamba jeshi la polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA kihalali, lakini waandamanaji wakaamua kufanya maandamano. Katika maelezo yao, CHADEMA wanasema utaratibu wa jeshi la polisi kupiga marufuku maandamano ulikuwa ni ukiukaji wa sheria za nchi.

Aidha, kwa mujibu wa sheria ya jeshi la polisi na sheria ya Vyama vya Siasa, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa, ni lazima itolewe na mkuu wa polisi wa wilaya na ni lazima iwe ni ya maandishi.

CHADEMA wanasema hawajawahi kupokea wala kuonyeshwa amri ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha ya kupiga marufuku maandamano ambayo mkuu huyohuyo wa polisi wa wilaya alikuwa ameyaruhusu kwa maandishi.

Majibu ya Lema kwa spika yanasema Pinda alisema uwongo alipoliambia bunge kuwa CHADEMA kingeshirikiana na serikali na kufanya mkutano, kusingetokea maafa.

CHADEMA wanasema mkutano wenyewe uliohutubiwa na Dk. Willibrod Slaa na Philemon Ndesamburo ulishambuliwa kwa mabomu ya machozi na maji ya washawasha na kutawanywa kabla ya makundi ya watu kurudi kwenye mkutano na Dk. Slaa na Ndesamburo kuendelea kuhutubia.

Eneo jingine ambako Pinda anagaragazwa ni pale alipoliambia bunge kuwa mkutano wa baraza la madiwani wa kumchagua Meya, Naibu Meya na wenyeviti wa Kamati ulianza kukiwa na wajumbe wote 31.

CHADEMA wanapinga hilo. Wanasema waziri mkuu alisema uwongo. Wanasema kanuni za Manispaa ya Arusha za mwaka 2003 zinataka kila mjumbe anayehudhuria mkutano wa halmashauri au kamati yoyote ya halmashauri awe kwenye rejesta ya mahudhurio inayotunzwa na mkurugenzi.

CHADEMA wanasema katika orodha ya waliohudhuria mkutano wa tarehe 17 Desemba 2010, hakuna jina hata moja la diwani wa CHADEMA; bali yapo majina ya madiwani wote 16 kutoka CCM.

Maelezo yaliyokabidhiwa kwa spika Makinda yanasema waziri mkuu alisema uwongo pale alipoliambia bunge kuwa CHADEMA walifanya vurugu Arusha.

Chama hicho kinauliza, ilikuwaje chama kilichofanya vurugu, viongozi wake wakafunguliwa mashitaka madogo tu ya kuandamana badala ya makosa makubwa kama kusababisha mauaji au uchochezi au kujaribu kuchoma majengo moto au makosa ya aina hiyo ambayo yana adhabu kubwa zaidi ya kuandamana.

CHADEMA wanasema Pinda aliliambia bunge kuwa utaratibu uliofuatwa kuchagua meya “ulikuwa sahihi kabisa, haukukosewa kitu chochote.” Wanasema huo ni uwongo.

Chama hicho kinanukuu kifungu cha 8(3) cha Kanuni za Halmashauri kinachosema akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na mkutano wa kwanza wa Halmashauri, itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri.

Kwa shabaha ya kukidhi matakwa ya kanuni, mkutano wa uchaguzi wa meya na naibu meya wa Arusha ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa halmashauri hiyo. Lakini walikuwepo wajumbe 17. Hivyo mkutano ni batili na Pinda alisema uwongo.

Katika majumuisho yake, Lema na chama chake, wanasihi bunge lihimize matumizi ya kanuni ya 63(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2007, ambayo inapiga marufuku mbunge kusema jambo la kubuni bungeni, bila kuwa na uhakika.

Hata hivyo CHADEMA wanataka Pinda apewe nafasi ya kufuta kauli yake; jambo ambalo wanasema litasaidia kumpa hadhi Pinda na bunge lenyewe.

0
Your rating: None Average: 4.2 (9 votes)
Soma zaidi kuhusu: