Chagulani: CHADEMA itatoa elimu bure Jiji la Mwanza


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

KATIKA umri wa miaka 25 Chagulani Adams Ibrahim anajiandaa kuweka historia katika Mkoa wa Mwanza kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza.

Chagulani, ambaye ni diwani wa Kata ya Igoma jijini humo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ataweka historia hiyo ikiwa atawapiku atapitishwa na chama chake kati ya wane waliojaza fomu.

“Mwanza sasa ni jiji na changamoto ni nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mkoa wetu,” anasema diwania huyo aliyeshinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Meya ajaye wa Mwanza, na bila shaka nitakuwa mimi, anatakiwa kuwa mtu ambaye yuko tayari kukabiliana na changamoto hizo. Nimezaliwa Mwanza, ninaifahamu Mwanza na ninajua nini cha kufanya ili iende mbele,” anaeleza.

Umri wa Chagulani umezua mjadala mkubwa miongoni wanaowania nafasi hiyo na wananchi wa Mwanza ambao wanasubiri kwa hamu uchaguzi wa Meya wa jiji unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, anasema ujana wake huo hauwezi kuwa kikwazo cha kutimiza majukumu yake ya kikazi kwa vile umeya ni taasisi na si mtu mmoja kama inavyotaka ionekane.

Miongoni mwa watakaowania nafasi hii, hakuna hata mmoja ambaye amewahi kushika wadhifa huo. Kwa hiyo, hakuna anaweyeza kusema ana uzoefu kuliko wengine.

“Umeya ni taasisi na kuna watu wanaofanya kazi kila kukicha kuhakikisha meya anafanya kazi zake vizuri. Kinachotakiwa ni kwa mwenye nafasi hiyo kuwa mwelewa wa mkoa wenyewe, watu wake na mahitaji yao,” anafafanua.

“Anatakiwa meya mchapakazi na mwenye maono safi na sahihi ya nini kinahitajika kuipeleka Mwanza mbele. Kinahitajika pia kiwango toshelezi cha elimu inayokwenda na mahitaji ya kisasa ya dunia hii.

“Mimi ni kijana mchapakazi. Ninaifahamu Mwanza na watu wake. Ninafahamu wanachokitaka wana Mwanza kwa vile nami ni mwenzao.

“Kwa kushirikiana na wenzangu katika halmashauri, tutahakikisha miaka mitano ijayo, watu wanaione Mwanza imebadilika kwa kiasi kikubwa.

“Kuna vitu viwili ambavyo naona watu wanachanganya. Kuna uzoefu wa kazi na taaluma. Mtu anaisomea taaluma, lakini uzoefu anaupata kazini. Ila mtu mwenye taaluma, kama mimi, anaweza kufanya kazi vizuri zaidi kuliko yule asiye na taaluma,” anasisitiza.

Chagulani anasema kero kuu za wananchi wa mkoa wa Mwanza zinaweza kugawanywa katika maeneo makuu mawili; ardhi na miundombinu.

Kuhusu ardhi, anasema kumekuwapo tabia ya watendaji wa Halmashauri ya jiji la Mwanza kujigawia viwanja wenyewe au kuwapa maeneo watu wenye uwezo kifedha katika njia zisizo halali.

Anasema hilo limechangia matatizo makubwa kuhusu upatikanaji wa ardhi kwa watu wenye kipato cha chini, jambo alilosema linaweza kuleta matatizo makubwa katika siku za usoni.

“Kuna njia kubwa mbili za kupambana na hili. Kwanza kuna kuanzisha kamati za ardhi ambazo zitatatua migogoro ya ardhi wakati mwingine bila ya kupeleka kesi mahakamani,” anafafanua.

“Wakati mwingine migogoro ya ardhi inaweza kutatuliwa kiufanisi na katika muda mfupi nje ya mahakama kuliko ikienda huko.

“Lakini la pili ni kuanza kufanya uchunguzi kuhusu hawa watendaji wa halmashauri wanaomiliki viwanja vingi. Kama walivipata kihalali, sawa, lakini kama hawakuvipata kihalali, basi taratibu zilizopo zitafuatwa,” anasema.

Kuhusu miundombinu, Chagulani anasema wakazi wa Mwanza wanateseka sana na tatizo la upungufu na ufinyu wa barabara zilizopo kwa sasa jijini humo.
Alisema wakazi wa jiji hilo wanateseka sana na usafiri kwa vile wanatumia muda mrefu barabarani kwa sababu ya foleni kutokana na ongezeko la idadi ya watu kutoendana na upanuzi wa mindombinu.

Mathalani mtu anayekaa Buhongwa akitaka kwenda Igoma anatakiwa kulipa Sh. 450 kwa sababu inabidi apitie Mwanza Mjini kabla ya kwenda Igoma. Kama mtu huyo angetumia barabara ya moja kwa moja kutoka Buhongwa hadi Igoma angelipa Sh. 250 lakini barabara hiyo si nzuri.

“Kama ikikarabatiwa na ikaanza kutumika, watu watakuwa wanapanda basi kwa Sh. 250 tu,” anasema.

“Na itabidi tufikirie ujenzi wa fly overs (barabara ya juu kwa juu) katika eneo la mabatini ili kupunguza foleni. Tukifanya hivi tutapunguza foleni na tutaokoa muda,” anafafanua.

Mwanasiasa huyo kijana anasema anafahamu kwamba gharama ni kubwa kujenga fly overs lakini anaamini ni jambo linalowezekana iwapo hicho ndicho wananchi wa Mwanza wanachokitaka.

“Bajeti ya halmashauri kwa mwaka inafikia kiasi cha Sh. 21 bilioni. Itategemea vipaumbele vyetu ni vipi kwa wakati husika. Kama tutaona kuna mambo muhimu zaidi ya hilo tutayafanya na kama hilo litakuwa la muhimu zaidi tutalifanya,” anasema.

Rushwa

Chagulani, kijana ambaye ndiyo kwanza anaanza rasmi kutafuta maisha, anasema kwamba ataonyesha ujasiri kupambana na vishawishi vyote kama vile rushwa vitakavyomkabili na kuvishinda.

“Ninaamini ujasiri wa kukataa rushwa uko moyoni kwa mtu na si umri wake. Mimi nilihongwa kiasi kikubwa tu cha pesa ili nisiwanie udiwani lakini sikuchukua.

“Mimi naichukia rushwa. Ndiyo maana nitahakikisha tunakusanya mapato yetu yote tunayopaswa kukusanya ili hatimaye tutoe huduma bora kwa wananchi,” anasema.

Elimu bure

Japokuwa, kwa mfumo wa sasa wanapaswa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema kwa kuwa chama hicho tawala kimekuwa cha upinzani katika Jiji la Mwanza, ilani itakayotekeleza kuhusiana na suala la elimu ni ya CHADEMA.

Kwa hiyo, amesema atahakikisha ilani ya uchaguzi ya CHADEMA inayoahidi elimu kutolewa bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne inatekelezwa iwapo atachaguliwa kuwa meya.

Anasema kitakachofanyika ni kwa halmashauri hiyo kufahamu kiasi cha fedha ambacho serikali huhudumia wanafunzi wa jiji hilo na yenyewe itafute vyanzo vyake vya mapato kulipa kiasi hicho.

“Ninataka Mwanza iwe ufunuo kwamba ile sera ya elimu bure inawezekana. CCM ni chama cha upinzani hapa Mwanza na wakae pembeni waone nini tutafanya,” anasema kwa kujiamini.

Uteuzi

Kwa mujibu wa taratibu, meya huchaguliwa kwa kura za siri na madiwani wote wa halmashauri husika. Madiwani hao ni wale wa kuchaguliwa, viti maalumu na mbunge au wabunge walio katika halmashauri hiyo.

Jiji la Mwanza lina jumla ya kata 21 ambapo jimbo la Nyamagana lina kata 12 na lile la Ilemela lina kata tisa.

Katika uchaguzi uliopita, CHADEMA ilishinda katika kata 11 na hivyo kina idadi kubwa ya madiwani kuliko CCM.

Kwa wingi huu wa madiwani, kuna uwezekano wa meya ajaye wa jiji hilo kutoka katika chama cha upinzani, na hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa hilo kutokea.

Meya wa zamani Leonard Bihondo yuko mahabusu akikabiliwa na kesi ya mauaji ya Katibu wa CCM, Kata ya Ismailo, Bahati Stephano.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: