Chaguo la CCM kutopiga vita ufisadi


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

UKIWAKUTA walevi wamekaa na kusifiana, unaweza ukashangaa ni jinsi gani wamehitimu katika sanaa ya kupeana ya ujiko.

Ni kama mashindano ya nani anaweza kutoa sifa zaidi kwa mlevi mwingine. Na katika kujua wanavyojua kupeana sifa, walevi huja na nyimbo zenye kuburudisha kilabu na kumfanya kila mmoja, hata mpita njia ajisikie hamu ya kucheza.

Nyimbo zao, zenye vibwagizo vifupi vifupi vyenye kurudia rudia maneno yale yale hadi yanakukaa hadi mifupani huimbwa kwa sauti kali vikisindikizwa na sauti za shangwe.

Ukiwa ni timamu kati ya walevi wenye kusifiana namna hii unaweza ukawa unapata burudani ya kutosha kabisa na kusahau matatizo yako kwa muda kadhaa kwani walevi wanaponegewa katika kusifiana hutoa burudani ya bure kwa kila awasikiaye.

Nilikuwa naangalia mkutano mkuu wa CCM na jinsi ambavyo wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika furaha yao wamethibitisha kile ambacho nilikiandika miaka minne iliyopita kuwa “wamelewa ugimbi wa madaraka”.

Kwa kila kipimo na kwa haki kabisa CCM na wanachama wake wako madarakani, na zaidi ya kuwa madarakani wameshikilia makreti yaliyojaa ‘kilevi cha madaraka’. Lakini nani atawalaumu? Hawawezi kuishi bila madaraka.

Hata hivyo, kuna vitu viwili ambavyo kwa mtu yeyote aliyefuatilia mkutano ule uliofanyika mjini Dodoma, ataona kuwa vimetokea na vyote vinahusiana.

Kwanza, CCM haitambui kuwa kuna tatizo la ufisadi nchini na ni tatizo kubwa. Na pili, CCM haina sera inayoeleweka ya kuushughulikia na kuumaliza ufisadi nchini.

Ninapozungumzia ufisadi, nazungumzia mfumo unaotengeneza, kulea, kudumisha na kuendeleza vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, undugunization, na kubebana katika kutawala pasipo kujali uwezo wa mtu.

Ufisadi kwangu mimi ni mfumo mbovu wa kutawala wenye kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma, kulimbikiza utajiri na njia za kupata utajiri mikononi mwa kikundi cha watu wachache na utawala wenye misingi ya kuleta hofu kwa kila anayeonekana kuupinga utawala huo.

Nimesema kuwa kwa kuangalia mkutano huu mkuu kuna mambo hayo mawili yanayoonekana lakini yanipasa japo kidogo kunyambua hili kwa undani ili tuweze kuelewa kwanini uamuzi wetu wakati wa kupiga kura baadaye mwaka huu unahusiana moja kwa moja na ufisadi.

Ninafahamu kuna watu (wakiwemo viongozi wa juu wa CCM) ambao hawaamini kuwa ufisadi ni tishio kubwa zaidi kwa maendeleo, uhuru na utu wetu kuliko magonjwa, ujinga, na umaskini.

Ufisadi unatishia maisha yetu zaidi kwa sababu unaongeza gharama za maisha, unavujisha uchumi wetu na kutengeneza mfumo bandia wa kiuchumi ambao hauwezi kuelezeka kisayansi.

Jiulize, kwanini licha ya matumizi makubwa ya dola za Kimarekani nchini kwanini bado mfumo wa bei uko chini? Jiulize, inakuwaje fedha zitolewe toka sehemu moja ya uchumi (trilioni 1.7) na kupelekwa kwingine katikati ya bajeti na kusitokee matatizo yoyote yale ya kiuchumi?

Ufisadi unafanya watu waishi kwa kuingia gharama ambazo vinginevyo wasingeziingia. Kwa mfano, imefika mahali katika shughuli zetu za kila siku tunaanza kutengeneza bajeti gharama za ufisadi katika kutafuta huduma na bidhaa mbalimbali.

Mtu anakwenda kwenye ofisi fulani ya umma ambayo anajua kwa mfano ada anayotakiwa ni shilingi 15,000 tu, lakini inabidi aongeze na shilingi 5000 juu yake ili apate huduma pale haraka haraka.

Hii 5000 ya ziada ni “gharama ya ufisadi” ambayo mfumo wetu unaikumbatia. Huu ni mfano mdogo tu lakini katika kutafuta ajira, shule, ununuzi wa vitu fulani fulani au hata kupata nafasi fulani fulani Mtanzania amejifunza kuingia gharama ya ufisadi. Huu umekuwa utamaduni.

Lakini zaidi ni katika kiwango cha juu cha utendaji. Miaka hii kumi na tano ya utawala wa CCM tumeshuhudia jinsi gani makampuni makubwa ambayo yamekuwa makuwadi wa ufisadi yakijipenyeza katika shughuli mbalimbali ambazo zinaitwa “uwekezaji”.

Wengine tena kwa kuwafuata sisi wenyewe na kuwabembeleza. Makampuni haya mengine yameweza kuingia kwa namna ambayo yasingeweza kufanya kwenye nchi zao. Lakini zaidi na la kutisha ni jinsi makampuni hewa ya kifisadi yalivyoundwa kuweza kuchota utajiri wetu.

Yote yametokea mbele na usoni kwa utawala wa CCM. Tangold, Meremeta, Deep Green, Dowans, Richmond na mengine mengi kama tunavyojua katika wizi wa EPA. Yote haya yameweza kusababisha upotevu wa zaidi ya shilingi trilioni 10.

Na kama serikali inapoteza asilimia 30 ya fedha za bajeti kila mwaka kwa mikono ya kifisadi, basi tatizo letu linaweza kuonekana kwa urahisi bila kutumia kurunzi kuwa ni kubwa zaidi. Nilitarajia CCM katika mkutano wao wangeweza kuonesha wanatambua hata kuigiza kuwa tuna tatizo kubwa la ufisadi nchini.

Mungu awaonee huruma kwani hawalioni, hawataki kuliona na hata likiwakodolea macho kama bundi aliyekosa tawi mchana hawawezi kuliona kamwe.

Lakini jambo jingine ni kuwa ni wazi kuwa hawana uwezo wa kushughulikia ufisadi. Sote tunajua kuwa CCM haiwezi kushughulikia ufisadi wala kuuondoa.

Hawawezi kuvunja mtandao mkubwa wa kihalifu (organized crime ring) ambao umejikita nchini sasa hivi ukijihusisha na madawa ya kuleva, usafirishaji silaha haramu na uhamishaji wa fedha kwa njia haramu (money laundering).

Mtandao ambao unahusisha wanasiasa, watumishi wa serikali na hata maafisa wa usalama wa ngazi mbalimbali. Mtandao huu umeweza kujipenyeza hadi kwenye sehemu ambazo tukizitajia tunaweza kuanza kuitana ubaya.

Labda hii ndiyo sababu CCM haiwezi kufanya vita dhidi ya ufisadi kuwa ni ajenda yake kuu ya mwaka huu. Hawawezi kwa sababu hawatambui na hawana uwezo wa kutambua, ufisadi ni sumu mbaya zaidi yenye kurudisha maendeleo nyuma kuliko tatizo jingine lolote.

Watajipitisha pitisha wakiahidi barabara, hospitali, shule na vyuo vingine vikuu vipya. Vyote hivi ni geresha kwani tatizo kubwa zaidi na lenye kuhitaji ujasiri zaidi ni la ufisadi.

Lakini hatuna budi kujiuliza wanapomaliza Bunge lao wiki hii, inakuwaje kama wao wenyewe ndio sehemu na sababu ya ufisadi huo? Itakuwaje kama baadhi yao ndio wanufaika wakubwa wa mfumo wa utawala wa kifisadi?

Itakuwaje kuwa ni ufisadi ndio unawafanya wadumu madarakani? Itakuwaje kuwa ufisadi ukibomolewa na wao vile vile watazibuka kutoka katika ulevi wanaopeana kama kwa kupokezana kama kibuyu cha ulanzi ?

Ndugu zangu, tuna uamuzi katika uchaguzi huu. Wao wameshajua wanachokitaka. Wamechagua kutokuongoza vita dhidi ya ufisadi. Wamechagua kulindana, kubebana, wamechagua kukumbatiana na kupepeana. Huu ni uchaguzi wao. Ni uchaguzi wa CCM na wapambe wake waimbao nyimbo za kufurahishana.

Ni uchaguzi wa taasisi za serikali yake ambazo zinanufaika na CCM kuwepo madarakani. Ni uamuzi wa wana CCM wote nchini. Huu ni uamuzi wao. Ni uamuzi wa watu milioni nne nchini; wana CCM.

Lakini Watanzania wengine nao wanaitwa na historia kufanya uamuzi. Wanaitwa kuchukua uamuzi ambao wanajua ni bora zaidi kwa ajili yao na kwa ajili ya watoto wao. Hata hivyo uamuzi rahisi naujua. Nao ni kujiunga na CCM na kuwa miongoni mwa waimbao “zaidi ya kile kile”.

Uamuzi wa kutopigana na ufisadi kwa nguvu zaidi ni uamuzi rahisi zaidi. Ni uamuzi wa waoga na wasio na ujasiri wa kuita ufisadi ni ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: