Chaguzi za CCM lango kuu la ufisadi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) sasa kimemaliza chaguzi za jumuiya zake, kufuatia mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazazi uliomalizika Jumamosi iliyopita.

Wazazi walimchagua Balozi Athuman Mhina ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya uenyekiti, kushika wadhifa huo kwa miaka mitano ijayo.

Katika uchaguzi uliojaa ushindani mkubwa kutokana na kura kupigwa mara mbili, baada ya raundi ya kwanza kushindwa kupata mashindi, kwa kuwa hakuna aliyefikisha asilimia 50 ya wapiga kura wote. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikwenda kwa Dogo Idd Mabrouk wa Zanzibar.

Itoshe tu kusema sasa jumuiya za CCM, yaani Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT-CCM) na sasa Wazazi, zimekamilisha kazi ya kujipanga na zitarejea tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mwaka 2013.

Ni kweli kulikuwa na ushindani mkubwa ndani ya chaguzi hizi zote, kwamba wagombea wengi walijitokeza na kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchaguliwa na kuchagua. Walioshinda wameshinda na walioshindwa wamerejea kujipanga upya kwa matarajio ya kujipanga vema zaidi siku zijazo.

Hata hivyo, chaguzi hizi za CCM zimetufundisha nini? Je, CCM kama chama tawala, chenye ilani ya uchaguzi inayotekelezwa sasa, inaweza kusimama na kujipiga kufua kwamba chaguzi zote hizi zilikuwa huru na haki?  Hili ni swali nitakalolijibu katika uchambuzi wangu wa leo.

Kwanza kabisa, mwishoni mwa wiki Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, alieleza haya: “Siku hizi chaguzi zimegeuzwa kama vita, nasikia hata katika uchaguzi huu kuna watu wamepigana kwenye baa…hii ni aibu sana kwa chama chetu…msituletee wahuni kwenye mikutano kama hii, nawaomba tukio hili liwe la mwisho kutokea kwenye uchaguzi kama hizi.

“Uchaguzi huwa ni suala la ushindani na si kugawa fedha kama njugu, matusi au kutoleana maneno ya fedheha na kashfa kama wanavyofanya katika chaguzi mbalimbali zilizopita za jumuiya.”

Kauli ya Kikwete ni kielelezo cha mwenendo mzima wa chaguzi ndani ya chama hicho. Kwa maneno mengine ndani ya chama tawala, kinachotakiwa kuwa kielelezo cha maadili mema katika uchaguzi.

Si tu kwamba ndio mabingwa wa kuvunja kanuni hizo, bali pia ni kiashirio kwamba katika mchakato wa kusaka madaraka ya dola, CCM haiwezi kusita hata kwa chembe kutumia hila na kila aina ya vishawishi almradi kufanya hivyo kutawahakikishia ushindi.

Ni kwa jinsi hii tunapotafakari chaguzi za jumuiya ya CCM zilizopita, tunapaswa kujiuliza kwa uaminifu kabisa ndani ya nafasi zetu, chimbuko la viongozi wenye hila na kila aina ya michezo michafu ndani ya safu ya utawala wa nchi ni nini, kama si mfumo wa kuchagua viongozi wasioona kinyaa kutumia fedha kununua uongozi?

Pia tunapaswa kujuliza, mtu akinunua uongozi kwa fedha zake, je, atatumika kwa ajili ya umma au kwa ajili ya ama kwanza, kurejesha fedha zake na faida juu, au kuwatumikia waliomdhamini kwa fedha, kwa maana hiyo wenye nguvu za fedha?

Ni kwa kutafakari hali hii tu, ndipo Rais Kikwete angeweza kujua pa kuanzia katika kupambana na rushwa na kila aina ya ufisadi nchini.

Ni jambo la bahati mbaya mno, kwamba vita dhidi ya rushwa inayoendeshwa na Rais Kikwete kwa kofia zote mbili, yaani ile ya uenyekiti wa CCM na ya mkuu wa dola, yaani Rais na amiri jeshi mkuu, anafanya mambo ama kwa huruma mno au kwa njia ya kusubiri nguvu nyingine, mbali naye, ichukue maamuzi magumu na mazito.

Kwa mfano, kama Rais alitambua kwamba katika uchaguzi wa kwanza wa jumuiya zake, yaani UVCCM, rushwa ilifanyika, nini kilimzuia kuchukua hatua ambazo zingedhibiti vitendo kama hivyo kujirudia kwa UWT-CCM na juzi Wazazi?

Rais anaamini kwamba kuonya kutatibu maradhi haya. Anasahau kwamba viongozi waliochaguliwa kwenye jumuiya hizi katika chaguzi zilizopita watakuwa na ushawishi katika utungaji wa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo.

Kwa mfano tu, ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 itakuwa ni zao la fikra za viongozi waliochaguliwa kwenye jumuiya zake zote katika chaguzi zilizopita.

Sasa, kama walipenya kwa hila, rushwa, matusi, ugomvi na kila aina ya uchafu; tuseme nchi imewekwa rehani kwa kiasi gani kwa kuruhusu tu watu hao wakae kwenye vikao vya kutunga sera na mipango ya maendeleo?

Ni kwa jinsi gani watu waliochaguliwa katika mazingira aliyosema Rais Kikwete, wanaweza kuwa na msukumo wa kuwafikiria wananchi wa kawaida juu ya mahitaji yao ya maji, barabara, zahanati, shule na nyinginezo?

Rais Benjamin Mkapa, pamoja na udhaifu wake mwingi sehemu nyingine, alipata kuwakataa watu waliokuwa wamehusika kutumia fedha kutafuta uongozi. Akaongoza kuyakataa majina yao kupitishwa na vikao vya chama.

Alisimamia kukata majina ya baadhi ya wagombea ubunge, wakiwapo watu wenye ushawishi mkubwa wa fedha. Alithubutu, na kwa hili alijijengea heshima ingawa baadaye ‘alitia tembo maji.’

Nini kinamfanya Rais Kikwete, kuanzia mwaka 2005 alipochaguliwa, aendelee tu kueleza kwamba anawafahamu wala rushwa kwa majina na anawapa muda wa kujirekebisha; akasema tena anawafahamu wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya, na kwamba vyombo vya dola vinachunguza.

Alitembelea bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni na kusema wazi kwamba anawafahamu wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaosaidiana na wafanyabiashara kukwepa kodi.

Aliahidi kumpa Kamishna Mkuu wa TRA majina hayo. Hadi leo hakuna kilichotokea.

Tunajiuliza, Rais Kikwete anachelea kuchukua hatua kali, chungu na zinazoumiza wahalifu, nani mwingine ndani ya serikali yake atafanya hivyo?

Katika hali yoyote ile, CCM haiwezi kukwepa lawama za kuwa baba wa ufisadi, kwa sababu ni kupitia chama hicho viongozi mafisadi wanapatikana

Rais amesema wazi, kila uchaguzi hila za fedha zilitumika na watu bila shaka wamepata nafasi za uchaguliwa. Adhabu yao kwa hisia za Rais, ‘wasirudie’ yaani waendeleze uchafu wao kwa miaka mitano, lakini baada ya hapo tutafute viongozi wasafi. Kwa mtindo huu nchi hii itaendelea kuwekwa mikononi mwa mafisadi daima!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: